Kamati ya Sheria na Katiba ya ACT Wazalendo imesema leo Jumanne Oktoba 31,2017 kuwa timu ya mawakili wa chama hicho ipo na Zitto katika mahojiano hayo.
Chama hicho kimesema Jumapili Oktoba 29,2017 akizindua mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani katika Kata ya Kijichi, wilayani Temeke Zitto anadaiwa kutoa maneno yanayoweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Kwa mujibu wa ACT Wazalendo, Zitto anadaiwa kutamka kuwa, wananchi wasiichague CCM kwa sababu Serikali yake imeshindwa kufanya uchunguzi na kuwakamata watu waliompiga risasi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.
Mbunge huyo anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya baada ya kushambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi katika makazi yake eneo la Area D mjini Dodoma Septemba 7,2017.
Chama hicho kimesema Zitto pia anadaiwa kutoa kauli kuwa wananchi wasiichague CCM kwa sababu Serikali yake imeshindwa kueleza chanzo cha miili ya watu wanaookotwa kwenye ufukwe wa Bahari ya Hindi, kama vile Coco Beach.
Kwa mujibu wa taarifa ya chama hicho, Zitto anadaiwa kutamka kuwa, “Hivyo kuichagua CCM ni sawa na kuwaunga mkono waliofanya vitendo vya kumshambulia Tundu Lissu na wanaoua watu wanaookotwa kwenye fukwe.”
No comments:
Post a Comment