Tuesday, October 31

Polepole azungumzia kuondoka Nyalandu


Dar es Salaam. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amemponda aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu akisema walishamweka pembeni kwa kuwa hakuwa mtu wa muhimu kwao.
Akizungumza jana Jumatatu usiku katika kipindi cha Msemakweli kinachorushwa na Channel Ten, Polepole aliyekuwa akizungumzia mafanikio ya Rais John Magufuli kwa kipindi cha miaka miwili, alimtakia heri Nyalandu huku pia akisema amejimaliza mwenyewe.
“Ameondoka mwanachama mmoja wa CCM leo (jana) amekwenda upinzani. Katiba yetu hii ya Jamhuri ya Muungano inasema kila mtu ana uhuru wa kujiunga na chama chochote. Tunaheshimu uamuzi wake, tunamkatia heri katika chama anakokwenda,” alisema Polepole.
“Aliyeondoka leo ni ‘very insignificant’ yaani kwa Kiswahili hatujaona utofauti. Ndiyo maana sisi tumetoa maelekezo kwa Serikali kwamba, watu ambao hawakuweza kutukimbiza katika awamu ya tano kwenye maendeleo ya Taifa letu kwenye uongozi wa awamu ya tano wawekwe benchi kwanza. Sasa wamewekwa benchi,” alisema Polepole.
Hata hivyo alisema Nyalandu ana haki ya kikatiba kuamua kwenda chama chochote anachokitaka na kwa kuwa CCM ni chama cha kidemokrasia hakitamlazimisha kubaki.
“Chama chetu kina watu wengi wakongwe na wa muda mrefu na kitaendelea kuwepo na kinafanya kazi watu wanaona,” alisema.
Alisema kwa kuwa Nyalandu alishawekwa benchi alipaswa ajitafakari na kujipanga upya.
“Unajua unapowekwa benchi uelewe kwamba ama uongeze mazoezi au umeongezeka kilo mbio zako zimepungua, kwa hiyo tunakuweka benchi ujitafakari kwamba hauna msaada kwenye timu,” alisema na kuongeza:
“Sasa ukiwekwa benchi kwa muda mrefu ukapata timu ya mchangani, wanacheza chandimu, wewe unafahamu chandimu? Unatoka daraja la kwanza unakwenda daraja la nne na ndiyo chandimu na ndiyo umekwenda na maji.”
                                                                                                    
Aliendelea kujisifu akisema CCM haina wasiwasi kwa kuwa kiwango chake ni cha juu na wachezaji wake ni wa kimataifa na wametengenezwa vizuri kuwahudumia Watanzania.
Huku akipekua katiba ya CCM, Polepole alimsikitikia Nyalandu akisema anakwenda kwenye chama kisicho na itikadi akiacha CCM yenye itikadi ya ujamaa na kujitegemea.

“Unamtazama mtu amekwenda kutafuta itikadi pahala ambapo kuna itikadi isiyojulikana. CCM itikadi yetu ni nini? Ibara ya nne, ibara ndogo ya tatu, anakwambia itikadi ya CCM ujamaa na kujitegemea ndiyo njia pekee ya kujenga jamii ya watu walio sawa na huru,” alisema na kuongeza:
“Sisi ni wajamaa kwa maneno na kwa matendo. Uliza chama anachokwenda itikadi yao ni nini? Kuna malango ya mbinguni na malango ya jehanam. Sisi tunamtakia mafanikio mema.”

No comments:

Post a Comment