Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Oktoba 31,2017 Meya Bwire amesema jana Jumatatu Oktoba 30,2017 akiwa Uwanja wa Ndege wa Mwanza kwa ajili ya mapokezi ya Rais John Magufuli, polisi wawili walimfuata na kumtaka aongozane nao hadi kwenye chumba maalumu walikomhifadhi kwa muda.
Amesema askari hao walirejea na kumchukua hadi Kituo Kikuu cha Polisi jijini Mwanza.
Bwire amesema askari hao walimweleza amri ya kumkamata na kumweka mahabusu imetolewa na Mkuu wa Upelelezi Mkoa, Faustine Shilogile ambaye naye anadaiwa kuipokea kutoka kwa mamlaka ya juu ambayo hakuelezwa.
Meya Bwire ambaye ni diwani wa Kata ya Mahina (CCM) na mkurugenzi mtendaji wa mtandao wa kampuni ya Alliance inayomiliki shule, kituo cha kuendeleza vipaji na timu ya soka ya Alliance amesema baada ya kukaa mahabusu kwa saa sita, RCO alifika na kumtaka kutafuta mdhamini, agizo alilolitekeleza na kuachiwa huru.
“Sikupewa masharti yoyote zaidi ya RCO kunitaka mimi na viongozi wenzangu tukamalize tofauti zetu ili kuondoa usumbufu kwa Jeshi la Polisi,” amesema.
Meya Bwire amesema, “Ingawa hadi sasa sijaelezwa sababu za kukamatwa na kuwekwa mahabusu katika hali ya udhalilishaji, naamini vita yangu dhidi ya ufisadi ndani ya jiji imechangia.”
Amesema tangu mwanzoni mwa mwaka amekuwa katika mgogoro na Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba kuhusu utekelezaji wa baadhi ya miradi iliyogharimu mamilioni ya fedha kutekelezwa chini ya kiwango.
“Nimeibua tuhuma za ufisadi katika mradi wa dampo la kisasa eneo la Buhongwa ambako zaidi ya Sh400 milioni zimetumika kujenga majengo yasiyolingana na thamani ya fedha; wenzangu ndani ya jiji na Wilaya ya Nyamagana hawafurahii ninapoibua tuhuma hizi na ndiyo chanzo cha mgogoro,” amesema.
Bwire ametaja mradi wa maji wa Fumagila akisema umetekelezwa kwa zaidi ya Sh800 milioni bila maji kutoka.
Amesema kutokana na kupinga ufisadi, madiwani wenzake kutoka CCM waliwasilisha azimio la kutokuwa na imani naye kwenye vikao vya chama hicho wakimtaka ajiuzulu.
Meya Bwire amesema vita yake dhidi ya ufisadi pia imesababisha majengo yake ya zahanati aliyoanza ujenzi mwaka 2008 kabla hajawa diwani kuwekwa alama ya X ili yabomolewa ikidaiwa eneo hilo ni la umma.
Amemshukuru Rais Magufuli kwa kuwaagiza viongozi wa jiji na mkoa kumaliza mgogoro miongoni mwao. Amesema yuko tayari kukaa mezani kumaliza tofauti zao.
No comments:
Post a Comment