Uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Novemba 26, utahusisha kata 43 nchini na kwa Dar es Salaam utazihusu kata za Saranga, Kijichi na Mbweni.
ACT Wazalendo imesema utafiti iliyoufanya unaonyesha kuwa chama hicho kinaweza kuchukua kata za Kijichi na Saranga endapo vyama vingine vya upinzani vitakiachia kisimamishe wagombea watakaochuana na wa CCM.
SOMA ZAIDI-ACT Wazalendo yaomba kuachiwa kata Dar
Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa ACT Wazalendo imeamua kuwasimamisha wagombea wawili na kuiachia kata moja kwa vyama vingine vya upinzani kwa kuwa wamejipima na kuona wanaweza kushinda bila kupingwa Kijichi na Saranga.
Zitto alisema, “Tumejipima na kuona ACT ikisimama peke yake Kijichi na Saranga tuna uwezo wa kuishinda CCM asubuhi kweupe. Tunachoomba vyama vingine vya upinzani vituachie tusimamishe wagombea halafu tushirikiane nao kuhakikisha tunaiangusha CCM.”
Alisema, “Tunawaambia wenzetu upinzani adui yetu ni mmoja CCM, hivyo tuweke kando tofauti zetu tushirikiane lengo ni kuhakikisha katika kata tatu za Dar es Salaam, CCM haipati hata moja.”
Chadema Kaskazini
Kuhusu uchaguzi huo, katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Aman Golugwa alisema juzi kuwa wagombea 16 wa udiwani katika kanda hiyo wameshapitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Katika Kata ya Murieti iliyopo jimbo la Arusha Mjini aliyepitishwa ni Simon Mollel na Kata ya Moita, jimboni Monduli aliyeteuliwa ni Lobolu Lerango.
Golugwa alisema katika Kata ya Musa iliyopo Arusha Mjini aliyepitishwa ni Elihud Laizer. Katika Halmashauri Meru, waliopitishwa na kata zao zikiwa kwenye mabano ni Dominick Mollel (Ambureni), Joyce Ruto (Makiba), Asantaeli Mbise (Maroroni), Daniel Mbise (Leguruki) na Emmanuel Salewa (Ngabobo). Katika Jimbo la Hai, waliopitishwa ni Elibariki Lema (Machame Magharibi), Moses Kalage (Weruweru), Ezra Ngapi (Mnadani) na Heldak Minde (Bomambuzi).
Mkoani Tanga, ni Josiah Shemeta (Lugusa) na Jafari (Ndege Momba).
Kata ya Majengo, Korogwe ni Abdallah Maoga na Kata ya Nangwa, Babati ni Yohana Dafi.
Akizungumza uchaguzi huo, Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari alisema wamejipanga kurejesha kata zote tano katika jimbo lake.
“Tumejipanga kufanya kampeni za kistaarabu na tuna uhakika wa ushindi,” alisema.
No comments:
Post a Comment