Chanzo cha mauaji hayo inadaiwa ni mzozo ulitokea baada ya Regina kumfuata James lindoni kudai fedha za matumizi ya mtoto.
Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Longinus Tibishubwamu alisema lilitokea mjini Babati jana saa 12:30 jioni.
Alisema askari huyo alikuwa lindoni katika Benki ya NMB tawi la Babati, Mtaa wa Usalama, Kata ya Bagara.
Kaimu Kamanda Tibishubwamu alisema marehemu Reginal alikuwa mkazi wa Mtaa wa Ngarenaro mjini Babati.
Alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa kabla ya kifo cha mwanamke huyo, kulitokea mzozo kati ya wawili hao kuhusu fedha za matumizi ya mtoto.
“Wakati wakiendelea na mzozo, ndipo askari huyo kwa kutumia silaha aliyokuwa nayo alimpiga Regina risasi nne kwenye paji la uso, kifuani na shingoni,” alisema.
Baada ya tukio, alisema mtuhumiwa aliitelekeza silaha lindoni na kwenda kujisalimisha polisi na askari waliokwenda eneo la tukio ndiyo walioichukua huku pia wakiokota maganda matatu ya risasi.
Kaimu Kamanda Tibishubwamu alisema mtuhumiwa yupo mahabusu kwa mahojiano kabla ya hatua nyingine kuchukuliwa na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mji wa Babati ya Mrara.
Askari wa FFU mjini Babati, aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina alisema ameshangazwa na tukio hilo kutokana na upole alionao James.
Alisema James ni askari mwenye nidhamu, hivyo hafahamu jambo gani limempata hadi kufikia hatua ya kumuua mzazi mwenzake.
Margareth John ambaye ni jirani wa Regina katika Mtaa wa Ngarenaro alisema mwanamke huyo alikuwa akipata wakati mgumu kumlea mwanawe kutokana na kutopatiwa fedha na mzazi mwenzake na kwamba alikuwa akisaidiwa malezi ya mtoto huyo na wazazi wake.
“Kinachosikitisha ni mtoto huyo mwenye miaka mitatu ambaye ameachwa kwenye wakati mgumu kwa kuwa mama amefariki na baba ndiyo hivyo tena, ila Mungu atamsaidia tu,” alisema.
No comments:
Post a Comment