Chapisho la kwanza la Gazeti la New York Times la Marekani halikuacha kitu. Waanzilishi wake waliokuwa na ushawishi pia ndani ya Chama cha Republican walikubaliana katika hoja. Walijua wanaanzisha safari itakayowavuta wengi.
Ingawa ndani yake kulikuwa na wenye taaluma tofauti kama masuala yanayohusu benki na uchumi na mengineyo, lakini wote baada ya vuta nikuvute walikubaliana kuwa kitu kimoja.
Walijadiliana kwa kina na ilipofika Septemba 18, 1851 siku ambayo gazeti hilo lilitoa nakala yake ya kwanza walitambulisha miiko. Pamoja na maelezo mengi waliyoyaweka kwenye chapisho hilo kipaumbele kikubwa kilikuwa kimoja tu – Walitaka kutuma ujumbe ambao ungeeleweka bayana kwa wasomaji.
Walikusudia ujumbe huo uwe mwongozo. Walitaka kuepuka kuyumbishwa. Walikuwa na mtazamo wa kujitegemea.Hivyo katika moja ya kurasa zake katika chapisho hilo la kwanza waliweka tahariri iliyotafsiri mambo mengi:
“Tutakuwa wahafidhina pale tutakapoona kuwa katika hali yoyote ile yatupasa kuchukua mkondo huo kwa kutilia maanani maslahi ya umma na tutakuwa wenye msimamo mkali katika kila jambo endapo tunaona mageuzi hayawezekani isipokuwa tu kwa kuchukua msimamo mkali.
Waliongeza, “Hatuamini kuwa kila kitu katika jamii ni kikamilifu kwa kiwango chote au kimekosewa kabisa - kile kilicho kizuri kinapaswa kutunzwa na kuendelezwa na kile kiovu kinapaswa kuondolewa au kufanyiwa mabadiliko.” Ndivyo gazeti hilo lilivyojipambanua.
Kilichotokea wakati wa kuanzisha New York Times, kinaweza kufananishwa na hali iliyotokea katika mdahalo uliofanyika juzi katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa, uliokuwa ukijadili “Vyombo vya habari dhidi ya taarifa za uongo”.
Washiriki wa mdahalo huo waligawanyika kwa hoja, lakini walionyesha kukubaliana katika msingi wa hoja unaohusu kuzingatia weledi katika uandishi wa habari.
Mdahalo huo ambao uliandaliwa kwa mara ya kwanza na Idhaa ya Kiswahili ya Deutsche Welle (DW), ulikuwa jukwaa huru kwa wachokoza mada na hata washiriki. Ulitoa nafasi kwa kila mshiriki aliyeweza kuchangia maoni yake kuhusu nafasi ya mitandao ya kijamii na ongezeko la kasi la taarifa za uongo. Pamoja na kwamba wazungumzaji katika meza kuu walikuwa wanne tu, Dk Harrison Mwakyembe ambaye ni Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), Dk Ayub Rioba, Mwandishi wa habari wa siku nyingi, Jenerali Ulimwengu na mmiliki wa mtandao Jamii Forum, Maxence Melo, lakini kwa ujumla washiriki wote walichangamka.
“Karibuni tujadili suala hili la vyombo vya habari dhidi ya taarifa za uongo hasa katika zama hizi ambazo mitandao ya kijamii ndiyo imeshika kasi na kizazi cha sasa kikiwa sehemu kubwa ya mitandao hiyo,” Mohammed Khelef aliyekuwa akiongoza mjadala huo kutoka DW aliwakaribisha washiriki.
Waziri Mwakyembe aliyekuwa wa kwanza kuzungumza anaidadisi mada hiyo na kutoa ufafanuzi. Katika maoni yake anataka washiriki watenganishe kati ya taarifa na habari.
Kwa maoni yake, anaona kuwa taarifa itabakia kuwa taarifa na kamwe haiwezi kukidhi vigezo vya kuwa habari.
Katika ufafanuzi wake, waziri huyo anasema yale yanayojitokeza kwenye mitandao ya kijamii hayapaswi kuchukuliwa kama habari hasa kwa kuzingatia kuwa habari ni matokeo ya kitu ambacho kimechakatwa kwa kuzingatia vigezo vya kitaaluma.
“Mimi naona hapa tunachanganya mambo. Mitandao ya kijamii ni kama vijiwe tu, hata kule kwangu Kawe nina kijiwe pia. Sema tu hapa vijiwe hivyo vimekusanywa na kuonekana kama kitu kimoja.
“Kitu kiwe habari lazima kipitie hatua zote muhimu ikiwamo kujibu maswali ya (nani, nini, wapi, kwa nini, lini (5W) na kwa vipi (H), sasa haya yanayotoa kwenye mitandao hayawezi kuwa habari, hizi ni taarifa tu. Bahati mbaya vyombo vyetu siku hizi vinategemea mitandao hiyo kama sehemu ya kupata habari,” anasema.
Hoja hiyo ingawa haikupingwa moja kwa moja na wachangiaji, lakini ilikosolewa na Ulimwengu ambaye alitambulisha aina mpya ya uandishi ujulikanao kama “Citizen Journalism”, yaani uandishi wa habari wa wananchi. Anasema dunia ya sasa imebadilika na hivyo kila mwananchi anakuwa sehemu ya kutoa taarifa.
Kabla ya kutoa hoja hiyo, Ulimwengu anatumia muda mwingi kuchambua dhana inayohusu kuibuka kwa taarifa za uongo ambazo zimeendelea kuwa gumzo katika kona mbalimbali duniani.
Vyombo vingi vya habari duniani vikiwamo vile vikubwa vimekuwa vikijikuta vikitumbukia katika mtego huo na hivyo kuleta usumbufu kwa wahusika.
Watengenezaji wa taarifa za uongo wanadaiwa kuratibu mambo hayo kwa lengo la kutimiza matakwa yao ikiwamo kuleta usumbufu katika jamii.
Balozi wa Ujerumani nchini, Dk Detlef Waechter anakumbusha namna taifa lake lilivyowahi kutikishwa na taarifa za namna hiyo wakati likishughulikia suala la mgogoro wa wakimbizi wanaoingia nchini humo kutokana na machafuko ya kisiasa na hali ngumu za maisha.
Anaona kwamba wengi wanaoratibu taarifa za namna hiyo wamekuwa na dhamira ya kutaka kuwavuruga watu, hivyo ili kuondokana na usumbufu huo kila mtumiaji wa mitandao ya kijamii anapaswa kuwa mwangalifu.
Lakini, Ulimwengu haamini kama mitandao ya kijamii ndiyo chimbuko kuu la kukithiri kwa taarifa za uongo. Akilinukuu gazeti moja la Buffalo Commercial (Buffalo, NY) anasema kasumba ya kusambaza taarifa za uongozi haikuanza leo wala jana.
Anaeleza kwamba gazeti hilo katika mwaka 1891 liliwahi kulia likiandika kuhusu kuibuka kwa habari za uongo. Lilionya kuhusu hali hiyo ambayo ingeweza kuwaathiri wengi.
“Hili suala siyo kitu kipya ni jambo la tangu miaka hiyo. Kimsingi wakati mwingine unaweza kusema kwamba habari za uongo kwa vile licha ya kwamba kitu kinaweza kuwa cha kweli, lakini kinakuzwa au kutiwa chumvi nyingi.”
Anaamini kuwa jamii iliyoelimika na yenye kupenda kujishughulisha na mambo, kamwe haiwezi kutumbukia kwenye mtego huu wa kuingia kwenye habari za uongo. “Lakini tukiwa na jamii mbumbumbu lazima tutatumbukia tu kwenye mtego huu.”
Ulimwengu anadokeza mbinu za kutambua habari za kubuni kuwa mara nyingi watengenezaji wa habari za kubuni wanakosa umakini hasa katika uandishi wa majina, sehemu au jinsi ya kuoanisha tukio, hivyo kwa yoyote anayechukua muda wake kuikagua habari iliyotungwa ni rahisi kuishtukia.
Hata hivyo, tofauti na wengine, Ulimwengu anasema mitandao ya kijamii ni jukwaa jipya ambalo limetoa fursa kwa watu wengi kufurahia uhuru wa kupashana taarifa na habari.
Kubana vyombo vya habari
Mbele ya Mwakyembe, Ulimwengu anagusia hatua inayochukuliwa za Serikali kubana vyombo vya habari ikiwamo kuvifungia mara kwa mara pale vinapokosea, akisema hilo si jambo jema.
“Wizara iwe na kazi ya kuviongoza vyombo hivi na wala isiwe inachukua hatua ya kuvifungia fungia tu, maana wakati mwingine vyombo hivi vinaweza kufanya makosa yanayoeleweka lakini unakuta wizara inavifunga. Wizara inatakiwa kuwa mlezi kwa vyombo hivi,” anasema.
Kuhusu hilo Waziri Mwakyembe anasema Serikali inazingatia misingi inayoheshimu weledi na baadhi ya magazeti hayo yameonywa zaidi ya mara tano lakini hayabadiliki.
Anapopata fursa ya kuchokoza mada, Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dk Ayub Rioba ambaye taasisi anayeongoza imewahi kutumbukia kwenye mtego wa habari za uongo ilipotangaza kuwa Rais wa Marekani, Donald Trump amempongeza Rais John Magufuli, anaeleza anajitambulisha kama mtu anayekerwa na hali hiyo.
Huku akisema ni vigumu kupata majibu ya moja kwa moja katika mjadala wa “vyombo vya habari dhidi ya taarifa za uongo” kutokana na ufinyu wa muda wa majadiliano, anasema wakati mwingine watu hubuni habari za uongo kwa lengo tu la kutaka kuibua mjadala fulani.
Anasisitiza pia kuwa suala la habari za uongo ni jambo lilikuwapo tangu miaka mingi ya nyuma, na kuna mazingira yanayoweza kusababisha watu kuzusha habari za uongo na mazingira hayo pia yanaweza kuwa katika muktadha wa kisiasa.
“Sisi TBC ni waathirika wa hili suala na nakumbuka taarifa ile ya Trump kumsifia Rais Magufuli nilisoma wakati nikiwa Japan lakini nikasema niwaambie nyumbani, lakini nilidhani wanajua kwa vile taarifa yenyewe ilikuwa na mapungufu mengi na isitoshe Rais Magufuli wakati ule alikuwa amesifiwa na viongozi wengi hivyo wala isingekuwa habari tena. Lakini tulichukua hatua na kufundishana.
Niseme wakati mwingine watu wanaibua habari za namna hii ili kuwajaza wenzao upepo, wengine kulipiza kisasi lakini yote kwa yote mitandao ya kijamii ni mapinduzi makubwa na vijana wetu wanapaswa kuwa wadadisi na kufanya utafiti kabla ya kuwa na haraka ya kila taarifa unayoipata kwenye simu,” anaonya.
Kama hiyo haitoshi, Dk Rioba anaungana na bosi wake Mwakyembe kwamba ili kitu kiwe habari lazima kiwe na sifa inayoendana na maadili ya kazi, misingi na uwajibikaji.
“Kinachotoka kwenye hii mitandao ni taarifa tu na wala siyo habari,” anasisitiza mwalimu huyo wa uandishi wa habari.
Katika hatua ya kwenda na wakati na kujaribu kujitofautisha na mitandao mingine, Melo ambaye anayeongoza mtandao wa Jamii Forum anaeleza changamoto wanayokumbana nayo kudhibiti mtandao huo ili lisiwe jukwaa la kupitisha taarifa za uongo.
Anasema ingawa mara nyingi wamekuwa wakipokea taarifa zenye ukweli ndani yake ikiwamo kutoka kwa wanasiasa, lakini wamelazimika kuajiri wataalamu wa fani mbalimbali wenye kazi ya kujiridhisha na taarifa zote wanazopokea kabla ya kuziruhusu kuwafikia wasomaji.
“ Pale kwetu kutokana na changamoto hii ya habari za uongo tumeajiri wataalamu kama wachumi, watu wa masuala ya benki, wanasheria na wengine ili kuzichuja taarifa zinazotufikia, maana kwa hapa kwetu teknolojia zetu ni ngumu kuchuja moja kwa moja taarifa za aina hii.”
Pamoja na hatua hiyo, anakosoa mtazamo wa Serikali wa kujaribu kubana mitandao ya kijamii kwa kuweka sheria ambazo anahisi haiendani na mazingira ya wakati huu.
Anasema sheria ya makosa ya mitandao haikupaswa kuwepo kwa vile inabana uhuru wa wananchi kuwasiliana na inawaweka wananchi hao katika mazingira magumu.
No comments:
Post a Comment