Pamoja na utunzi wa sheria, wajibu mwingine na wenye thamani kubwa kwa Bunge ni kuisimamia Serikali. Kwamba Bunge lipo kuhakikisha Serikali ambayo ni tawi la utendaji katika dola, haifanyi mambo yake bila uangalizi.
Msingi wa wa Bunge kuwepo ni kuhakikisha sauti za watu zinasikika na zinazingatiwa, muhimu pia ni masilahi ya wananchi yanakuwa ni kipaumbele kwa vipimo sahihi.
Kwa mantiki hiyo, kuwepo kwa Bunge maana yake ni kuhakikisha wananchi wanakuwa na amani ya fikra na utulivu wa kiakili. Bunge lina wajibu wa kuhakikisha wananchi hawatilii shaka uamuzi na utendaji wa Serikali, maana lenyewe lipo kuweka mambo sawa.
Ndiyo maana kunapokuwa na kashfa za rushwa au nyingine zozote na kukiwa na kusuasua kwa Serikali katika kuchukua hatua, Bunge hupaswa kuingia kazini kuchunguza jambo husika kisha kutoa maazimio kulingana na matokeo ya uchunguzi.
Ni kutokana na wajibu huo wa Bunge kwa Serikali, inakuwa dhambi kubwa mbele ya mgawanyo wa nguvu za mihimili mitatu ya nchi, kwa maana ya Serikali, Bunge na Mahakama, endapo itaonekana inafanya kazi kama timu moja au mhimili mmoja kuendesha mingine.
Usimamizi wa Bunge kwa Serikali unahusu pia vyombo vya ulinzi na usalama, kwamba pale inapoonekana kuna kusuasua au kupotoshwa kwa ukweli katika matukio ya kijinai yenye kugusa viongozi, Bunge hupaswa kuendesha uchunguzi wa kibunge.
Sababu ni kwamba matukio makubwa yenye kufanya wananchi kutilia shaka umakini wa vyombo vya usalama na kutenda kwake haki, Bunge ndiyo chombo ambacho hutakiwa kuingia ndani ya tatizo na kutoa majibu.
Wakati mwingine Bunge haliingilii kati ili kuonyesha umma kwamba lenyewe linaweza zaidi kuliko vyombo vya Serikali, la! Kuingia kwake husaidia kuzipatia majibu nadharia nyingi ambazo huzunguka kutokana mfuatano wa matukio yenye kufanana au jambo lililoibua taharuki kubwa kitaifa.
Mkazo wa hilo ni kuwa katika kila kashfa ambayo inaweza kuikumba nchi au matukio ya kihalifu yenye sura nzito, kila nadharia huaminiwa na watu, kiasi kwamba majibu ya kweli yanaweza kupatikana lakini yasiaminiwe na sehemu kubwa ya umma. Ni wajibu wa Bunge kufahamu kiu hiyo na kuikata.
Bunge la Marekani
Kashfa ya Watergate ndiyo iliyomuondoa madarakani Rais wa 37 wa Marekani, Richard Nixon mwaka 1974. Hata hivyo, mafanikio kwa jumla yanabebwa na Bunge (Congress) baada ya vyombo vya usalama kuzidiwa nguvu na ushawishi wa Rais.
Kuelekea uchaguzi wa Rais Marekani Novemba 7, 1972, Nixon wa Republican akiwa anagombea ili kurejea madarakani kwa muhula wa pili, timu yake ya kampeni ilifanya umafia kwa kuingia kwenye ofisi za Kamati ya Taifa ya chama cha Democrats (DNC), zilizokuwapo kwenye jengo la Watergate, Washington DC.
Timu ya Nixon iliwatumia pia maofisa wa idara za ujasusi za CIA na FBI. Uvamizi huo ulilenga kudukua mawasiliano yote ya kampeni za Democrats kwa kuingiza vifaa vya kunasia mazungumzo kwenye simu, vilevile kuchukua nakala ya nyaraka zote za kampeni.
Uvamizi wa kwanza ulifanyika Mei 28, 1972 na kufanikiwa kuingiza vifaa vya kunasa mazungumzo ya simu. Mara ya pili ikawa Juni 17, 1972, wakavunja kabati la nyaraka za DNC, hivyo kunakili siri zote za kampeni za Democrats.
Siku hiyo ya Juni 17, mmoja wa walinzi wa Watergate aliona waya uliotumiwa na makomandoo waliofanikisha operesheni hiyo ya kuvamia ofisi za DNC, akaukata bila kutilia shaka jambo lolote. Baadaye mlinzi huyo akawaona makomandoo wakijaribu kuunganisha waya mwingine, hivyo akatoa taarifa polisi.
Maofisa wa FBI walifika na kuwakamata watu watano waliokuwamo kwenye ofisi za DNC. Ikabainika watu hao ni makomandoo wa Cuba waliopewa mafunzo Marekani ili kumpindua aliyekuwa kiongozi wa Cuba, Fidel Castro.
FBI ilipowapekua makomandoo hao, iliwakuta na vielelezo vyenye kuonyesha wanawasiliana kwa ukaribu na maofisa wa Ikulu, hasa kitengo cha siri cha ujasusi wa kuzuia taarifa nyeti za Serikali zisivuje kwenye vyombo vya habari (White House Plumbers).
Baada ya makomandoo hao kukamatwa, haraka sana Rais Nixon alitumia mamlaka yake kuhakikisha wavamizi hao wa ofisi za DNC hawahusishwi na Republican. Zaidi picha ikageuzwa na kuwa kashfa kubwa kwa Democrats.
Wale makomandoo walijieleza kuwa wao ni wapigania uhuru wa Cuba na walikuwa na taarifa zote kwamba kampeni za Democrats zilikuwa zinafadhiliwa na Cuba chini ya Castro, hivyo walivamia ofisi za DNC ili kukusanya vielelezo.
Maelezo hayo ya makomandoo wa Cuba waliofundwa na Serikali ya Marekani, yaligeuka mwiba kwa Democrats, kwani Nixon alishinda kwa kishindo kwa kubeba kura 520 kati ya 538 za kura za majimbo, wakati mpinzani wake, George McGovern, alipata 17.
Kashfa ya kampeni zake kufadhiliwa na Cuba ya Castro, haikuicha Democrats salama, kwani ilikataliwa kwenye majimbo 49 na kukubaliwa na jimbo moja pamoja na wilaya kuu, yaani Washington DC. Kura za umma, Nixon alimzunguka McGovern karibu mara mbili. Lilikuwa anguko baya kwa Democrats.
Heshima ya Congress
Propaganda za kwamba makomandoo wa Cuba walifuatilia nyaraka za kuonyesha Democrats inavyofadhiliwa na Serikali ya Cuba hazikukata kiu. Bado maswali yalikuwa mengi, ukizingatia uvamizi ulifanyika miezi mitano kabla ya uchaguzi.
Baraza la Seneti liliunda Kamati Teule kuchunguza kampeni za urais 1972. Kamati hiyo kwa kifupi iliitwa Kamati ya Seneti ya Watergate (Watergate Senate Committee) ambayo ilikuja kufichua ukweli wote. Baadhi ya vielelezo vya uvamizi wa DNC vilikutwa Ikulu ya Marekani, White House.
Baraza la Wawakilishi lilipokea ripoti ya Seneti kisha kuungana Bunge zima (Congress) na kuandaa hoja ya kumwondoa madarakani Nixon. Agosti 9, 1974, Nixon alijiuzulu na makamu wake, Gerald Ford alimrithi.
Simulizi ya Watergate ni kuonesha jinsi Bunge lilivyo na nguvu. Idara za usalama Marekani zilikuwa zimeshindwa kukata mzizi wa fitina kwa sababu wahusika wa uhalifu walikuwa watu wazito. Baada ya Congress kukamilisha kazi, siyo tu kwamba Nixon alijiuzulu, bali wasaidizi wake wengi walifungwa.
Mfano kama huo upo maeneo mengi, kama kuna mambo ambayo inaonekana vyombo vya usalama vimeshindwa kukata kiu, Bunge linapaswa kuingia kazini na kupata majibu yenye kutosheleza maswali yanayoibuka.
Mwaka 2013, baada ya kuwepo malalamiko makubwa ya ukiukwaji wa haki za binadamu katika operesheni iliyoitwa Tokomeza Ujangili, Bunge liliingia kati kuchunguza na ripoti yake ilisababisha mawaziri wanne waondolewe kwenye Baraza la Mawaziri.
Bunge linaweza kutekeleza wajibu huo wa kuchunguza na kuibuka na majibu yenye tija kuhusu masuala mbalimbali yenye kuitatiza nchi, kama linakuwa linatambua nguvu zake na mamlaka yake kikatiba.
Tamthiliya ya wasiojulikana
Hivi sasa nchini kumekuwa na neno linaloogopesha lakini linatamkwa kama kejeli au mzaha, “wasiojulikana.” Limekuwa maarufu zaidi likitamkwa na wengi hasa baada ya mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu kupigwa risasi.
Lissu, ambaye ni rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, alipigwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 7, mwaka huu, nyumbani kwakemjini Dodoma, mchana kweupe.
Mwanamuziki wa kizazi kipya, Ibrahim Mshana ‘Roma Mkatoliki’ na wenzake watatu, walitekwa Aprili mwaka huu na watu wasiojulikana kabla ya kujikuta kwenye Ununio ufukweni mwa Bahari ya Hindi jijini Dar es Salaam.
Novemba mwaka jana, kada wa Chadema, Ben Saanane alitoweka na mpaka leo hajapatikana. Tukio la Ben kupotea limezungumzwa mara nyingi na majibu yenye kukata kiu ya jambo husika hayajawahi kupatikana.
Hivi karibuni, kumekuwa na mfululizo wa matukio ya kuvamiwa na kulipuliwa kwa ofisi za uwakili Dar es Salaam na Zanzibar. Taasisi tatu za mawakili zimekumbwa na kadhia hiyo. Vilevile Meja Jenerali mstaafu, Vincent Mritaba ameshambuliwa kwa risasi mchana nyumbani kwake.
Hizi ndizo nyakati ambazo Bunge hutakiwa kuendesha uchunguzi wake wa kibunge, kutafuta kiini cha mfululizo wa matukio nyuma ya tamthiliya ya wasiojulikana. Shambulio la Lissu na Mritaba, milipuko ya Immma Advocates na Prime Attorneys, kupotea Saanane, Roma na mengine.
Huu ni wakati wa Bunge kuwa imara na kutoa makucha yake. Ni wajibu wa Bunge kuhakikisha wananchi hawawi wenye wasiwasi na maisha yao. Lazima lioneshe kuwa nchi ina vyombo ambavyo vinaweza kupokezana. Kimoja kikifikia mahali fulani, kingine kinaweza kwenda mbali zaidi. Bunge limalize huu ukungu wa tamthiliya ya wasiojulikana.
No comments:
Post a Comment