Sunday, October 29

Kenya yagawanyika zaidi baada ya uchaguzi


Kama ilivyoamuriwa na Mahakama ya Juu, uchaguzi wa marudio wa urais ulifanyika Oktoba 26.
Kivumbi hicho kingekuwa na farasi wawili, lakini farasi mmoja alijiondoa kwa madai kuwa zoezi hilo tayari lina mshindi.
Farasi inatumiwa kumaanisha wagombea wenye ufuasi mkubwa kama vile kiongozi wa upinzani Raila Odinga na Rais Uhuru Kenyatta.
Raila alikuwa ameapa kwamba kamwe hawezi kushiriki kinyang’anyiro hicho ikiwa mabadiliko ambayo alitaka yatekelezwe katika Tume ya uchaguzi hayakufanyika. Na kwa hakika, hakushiriki. Hatua yake ilimwachia Kenyatta uwanja uliosheheni ulimbukeni wa siasa na kumhakikishia ushindi bila wasiwasi.
Hatua ya kiongozi huyo wa upinzani iliwaingiza wengi kiwewe kwa sababu karatasi za uchaguzi na kompyuta za kutangaza matokeo ya urais zilikuwa zina jina la Raila.
Si ajabu wanasiasa wa Jubilee walielekea kortini wakiwa na lengo la kumlazimisha Raila kushiriki uchaguzi huo. Mahakama ilisema kikatiba, Mkenya yeyote ambaye anataka kutoshiriki kwenye uchaguzi wa urais ana haki ya kufanya hivyo na korti haina mamlaka ya kumlazimisha.
Hii ilimwacha Rais Kenyatta akiwa farasi wa kipekee miongoni mwa wagombea wasiokuwa na ujuzi wowote kwenye siasa.
Hii inamaanisha kuwa, Rais Kenyatta hana mpinzani anayeweza kupimana naye nguvu. Wagombea kama vile Ekuru Aukot wa Thirdway Alliance, Cyrus Jirongo na Joseph Nyaga ni miongoni mwa wagombea walioingia kwenye mashindano hayo.
Jirongo alikubaliwa kugombea urais siku moja tu kabla ya uchaguzi huo kufanyika. Hii ni kwa sababu, mwanasiasa huyo alikuwa ametangazwa kuwa amefilisika na kwa hivyo kisheria hangekubaliwa kuwania kiti chochote cha kisiasa.
Lakini, Jirongo alijiokoa kwa kwenda mahakamani na kuomba majaji wabatilishe hali yake kwa kutangaza kuwa yeye hajafilisika.
Uamuzi wa mahakama, kwa hivyo, ulimwokoa na kumpa nafasi ya kugombea urais. Wadadisi wa siasa wanasema kanuni za kisheria zinasema mgombea wa urais sharti awe kwenye orodha ya wagombea kwa muda wa siku 21. Jirongo hata hakuwa na wakati wa kufanya kampeni. Aukot pia hakuwa na wakati wa kufanya kampeni.
Uchaguzi huu wa marudio huenda ukakumbwa na vizingiti vya kisheria kutokana na kupuuzwa kwa sheria za uchaguzi.
Mazingara ambayo uchaguzi ulirudiwa yameleta uwezekano wa ushindi wa atakayechaguliwa kupingwa mahakamani.
Lakini, matukio ya siku moja kabla ya kura kupigwa pia yalileta taswira nyingine mpya kwenye pilikapilika za siasa za Kenya.
Mnamo Oktoba 24, raia watatu walienda Mahakama ya Juu kuomba kuwa uchaguzi wa Oktoba 26 uahirishwe hadi wakati ambao mazingara ya siasa ni shwari kwa kupiga kura.
Jaji Mkuu David Maraga alikuwa tayari kusikiliza na kuamua kesi hiyo kwa haraka, lakini majaji wenzake hawakufika kortini.
Kila mmoja wa majaji Jacton Ojwang, Susan Njoki, Smokin Wanjala na Mohammed Ibrahim alijipatia shughuli. Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu hangeweza kufika kortini kwa sababu gari lake rasmi lilikuwa limevamiwa jioni ya Oktoba 24 na mlinzi wake kupigwa risasi mara tatu na kuachwa katika hali mahututi.
Kisa hiki cha kuogofya kilimwacha Mwilu na woga juu ya maisha yake. Inaaminika kwamba uhalifu huo ulikuwa unamlenga
Katiba inasema kuwa, uchaguzi lazima ufanyike katika maeneo 290 yote ya ubunge kote nchini lakini jinsi mambo yalivyo, sheria hiyo haijazingatiwa.
Kuna maeneo kadha na majimbo ambapo uchaguzi haungeweza kufanyika kwa sababu mbalimbali mojawapo ikiwa wapiga kura kulisusia zoezi hilo kufuatia tangazo la Raila kwamba Nasa haitashiriki uchaguzi huo kwa sababu haungekuwa huru wala haki.
Oktoba 25 kiongozi huyo wa upinzani alifanya mkutano mkubwa kwenye bustani la Uhuru Park, Nairobi na kutumia fursa hiyo kutangaza kuwa Nasa itabadilika na kuwa muungano wa kuleta mabadiliko Kenya.
“Muungano huu sasa utapinga uongozi wa Jubilee kulingana na sheria. “Hatutajihusisha na ukiukaji wa sheria, lakini tutaonyesha Jubilee kwamba haiwezi kutuongoza jinsi inayotaka,” akasema Raila.
Kufuatia tangazo hilo, Nasa sasa inaitwa National Resistance Movement (NRM).
Raila pia alitangaza kuwa wafuasi wake wataanza kususia bidhaa na biashara za kampuni na watu wanaounga mkono Jubilee. Tayari baadhi ya Wakenya wameacha kutumia shirika la Safaricom na kuhamia kwa kampuni nyingine kama vile Airtel na Telkom.
Kulingana na takwimu za waliopiga kura, ni wazi kuwa, mamilioni ya Wakenya hawakupiga kura. Wadadisi wa siasa kama vile Miguna Miguna wanasema wapiga kura wamechoshwa na uchaguzi ambao hauleti matokeo yanayofaa.
Kwa kutofika vituoni kupiga kura, asilimia 56 ya Wakenya wanaonyesha wanataka mabadiliko katika jinsi uchaguzi unavyofanyika.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Wafula Chebukati anasema waliopiga kura ni asilimia 48, lakini baadaye alibadilisha na kusema ni asilimia 33. Hii yaonyesha tume hii haijui ni watu wangapi walifika vituo vya kupigia kura.
Vijana walirundika mawe na visiki barabarani kuzuia uchaguzi kufanywa. Hii imelazimisha jeshi na kikosi cha polisi kutumia mbomu ya machozi na bunduki kuwazuia vijana hao kufanya fujo.
Tume ya IEBC imetangaza kuwa uchaguzi ungerudiwa tena katika majimbo ambako haukufanyika, lakini haijulikani jinsi tume hiyo itatekeleza wajibu huo ikikumbukwa kwamba wakazi wa sehemu hizo hawataki kupiga kura kabisa.
Ninavyoona mimi, uchaguzi huu ni kama hekaya za Abunwasi. Hii ni kwa sababu, nusu ya nchi haikushiriki kwenye uchaguzi.
Katika jimbo la Kisumu, watu wawili walifariki dunia baada ya kupigwa risasi na polisi. Wengine wengi wanauguza majeraha katika hospitali mbalimbali.
Katika jimbo la Busia, wakazi walijawa na hamaki kutokana na uchaguzi huo, walikabiliana na polisi na baadaye kuchoma karatasi za kupigia kura.
Mtu mmoja aliyefika kwenye kituo kimoja cha kupigia kura katika eneo hili alikuwa amejihami na nyuki na akawaachia kuvamia maofisa wa IEBC waliokuwa wanasubiri kusimamia shughuli hiyo.
Raila alikuwa amewashauri wafuasi wake wasitoke nje ya nyumba zao kwa sababu vikosi vya jeshi na polisi wanaweza kuwaua kama ambavyo wamekuwa wakifanya tangu kiongozi huyo wa upinzani kutangaza kuwa hawezi kushiriki kwenye zoezi hilo.
Majimbo ya Kakamega na Machakos pia yalikumbwa na rabsha kwa sababu maeneo hayo yana wafuasi wengi wa Raila.
Ingawa Raila alijiondoa kwenye shindano hili, matangazo ya matokeo ya kura yaonyesha amepata kura kadhaa katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Uchaguzi huu wa marudio una dosari si haba. Lakini, kwa sababu ya uchumi kudorora, ukabila kuzidi na wananchi kutaka kusonga mbele na maisha yao bila kujali kura hii ilipigwa vipi, ni muhimu ikiwa viongozi watazingatia amani. Rais Uhuru atakapoapishwa hivi karibuni, hana budi kujaribu kuwaleta pamoja watu wote ili utawala wake katika muhula huu wa pili usikumbwe na matatizo na migogoro mingi.
Kwa muda mrefu sasa, uchaguzi unafanyika lakini tume ya uchaguzi haijaonyesha kuwa inafanya kila iwezalo kuhakikisha kuwa unakuwa huru na haki.
Kenya imegawanyika mwaka huu kuliko miaka mingine yote iliyopita. Kuna haja ya viongozi kutafuta suluhisho ili nchi iweze kupona kutokana na chuki na uhasama wa kikabila ambao sasa ni kama saratani.
Kenya iko kwenye njia panda, lakini viongozi wa siasa hawataki kuketi na kujadiliana kuhusu hatma ya baadaye ya nchi hii.
Rais Kenyatta aliposhauriwa na Chebukati akutane na Raila, alisema hawezi kufanya hivyo hadi marudio ya kura yafanyike .
Sasa marudio yamefanyika lakini sehemu nyingine hazijapiga kura. Hali hii imesukuma IEBC kurudia uchaguzi katika majimbo ya Homa Bay, Kisumu na Migori.

No comments:

Post a Comment