Sunday, October 29

Waziri Ummy aeleza alivyolamba dume

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na Watoto, Ummy Mwalimu (mwenyelemba katikati)akiwa katika matembezi ya hisani ya kuhamasisha uchunguzi wa saratani ya matiti yaliyoandaliwa na taasisi ya Aga Khan Foundation na Taasisi ya saratani ya Ocean Road jana asubuhi. Kulia kwake ni Mkurugenzi Mtendaji wa Ocean Road Dk Julius Mwaiselage na kushoto kwake ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Grace Magembe. Picha na Herieth Magembe  
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ameeleza namna alivyomshawishi Rais John Magufuli kukubaliana naye hadi zikatengwa fedha kwa ajili ya kununulia kifaa cha kupimia saratani.
Kifaa hicho cha PET/CT scan kinatarajiwa kupunguza asilimia 60 ya wagonjwa wanaopelekwa nje ya nchi kwa uchunguzi na matibabu.
Akizungumza jana mara baada ya matembezi ya hisani ya kuhamasisha uchunguzi wa saratani ya matiti yaliyoandaliwa na Aga Khan Foundation na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Ummy alisema bado Serikali inaendelea kuwekeza katika sekta ya afya
“Rais Magufuli amenipa dhamana ya kunisaidia Sh15 bilioni kwa ajili ya kununulia kifaa hiki,” alisema waziri huyo na kuongeza:
“Na nimemwambia ukinipa fedha hii tutapunguza wagonjwa wa rufaa nje ya nchi kwa zaidi ya asilimia 60, amekubali na tunaamini kabla ya Juni 30, 2018 Tanzania itakuwa nchi ya kwanza kupima saratani kwa PET/CT scan.”
Upatikanaji wa kifaa hicho utaifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza Afrika Mashariki na Kati kuanza kutoa matibabu ya juu ambayo hutolewa kwa kutumia kifaa hicho
Ummy alisema kutokana na kukosekana kwa kifaa hicho, asilimia 60 ya wagonjwa 57 waliopelekwa nchini India mwaka huu kwa magonjwa ya saratani, walikwenda kupimwa na kifaa hicho ambacho hutambua zaidi magonjwa ya saratani.
“Vilevile juhudi hizi zimelenga kuongeza vifaa vipya vya kutibu magonjwa ya saratani ikiwa ni pamoja na mashine za LINAC, CT Simulator ambapo vifaa hivi vitaanza kufanya kazi ifikapo Desemba mwaka huu,” alisema Ummy.
Daktari bingwa wa magonjwa ya saratani kutoka Hospitali ya Aga Khan, Harrison Chuwa alisema taasisi hiyo kwa muda mrefu imekuwa ikitoa matibabu ya saratani na tiba shufaa.
“Tuna mpango wa kusambaza huduma hii katika vituo vyetu ambavyo vipo mkoani ili kuisaidia Serikali,” alisema.

No comments:

Post a Comment