Mjini Kibaha, imeripotiwa kuwa miili ya watu wawili imeopolewa mtoni jana ikisadikiwa kuwa watu hao walisombwa na mafuriko yaliyotokana na mvua iliyonyesha mfululizo Jumatano na Alhamisi.
Mwili mmoja uliopolewa jana saa 7:30 mchana katika Mto Kiluvya na umetambuliwa kuwa wa Issa Ally (28) ambaye ni mgambo.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Blasilus Chatanda alisema mgambo huyo alizama akijaribu kumuokoa mtoto aliyetaka kusombwa na maji.
Alisema mgambo huyo hakuonekana hadi maji yalipopungua na mwili wake kukutwa umbali wa takriban kilomita nne kutoka eneo alikozama.
Kamanda Chatanda alisema mwili mwingine ulioopolewa umetambuliwa ni wa Simon Ramadhani (27), mkazi wa Muheza katika Kata ya Pangani mjini Kibaha aliyesombwa na maji akijaribu kuvuka Mto Mpiji na kwamba miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani ya Tumbi.
Mabasi Udart yaharibika
Mbali ya mvua kusababisha vifo, Udart yenye ofisi eneo la Jangwani imepata hasara kutokana na mabasi yake 29 kuharibika.
Majengo ya ofisi za Udart yalifurika maji yaliyoathiri vyumba vilivyo chini na kuharibu baadhi ya vifaa.
Hiyo ni mara ya kwanza kwa ofisi za kampuni hiyo kuathiriwa na mvua ikiwa ni miezi 10 tangu kuzinduliwa kwa huduma zake jijini.
Mkuu wa kitengo cha mawasiliano Udart, Deus Bugaywa akizungumza na waandishi wa habari jana alisema mabasi 29 kati ya 134 yameharibika baadhi ya vifaa. Pia mvua ilisomba matairi.
“Kwanza tunaomba msamaha wateja wetu kwa usumbufu uliojitokeza Alhamisi wakati mvua ikinyesha, kwa sasa watuvumilie hadi Jumapili (kesho) huduma zitakaporejea vizuri, mabasi 29 yalishindwa kuendelea na huduma baada ya kuathiriwa na mvua,” alisema.
Alisema, “Mabasi hayo yalikuwa kwenye marekebisho katika injini, giaboksi na difu. Mvua zilipoanza maji yalijaa na matengenezo yalisimama. Kwa sasa mafundi wanaangalia athari na namna gani zishughulikiwe mapema ili magari yarudi barabarani.”
Bugaywa alisema kwa sasa si rahisi kuwa na makadirio ya hasara iliyotokana na mvua.
Kutokana na athari hizo, ofisa huyo alisema wamelazimika kuhamisha baadhi ya shughuli na kuziondoa katika eneo la Jangwani zikiwamo za kulaza magari, kujaza mafuta na gereji.
Bugaywa alisema vituo vya Gerezani na Kimara vitatumika kutoa huduma ya gereji, huku vya Kivukoni, Gerezani na Kimara vitatoa huduma ya kulaza magari na kujaza mafuta.
Alipoulizwa kuhusu hatima ya kutumia majengo ya ofisi yaliyopo Jangwani, Bugaywa alisema suala hilo linahitaji majadiliano kati ya Serikali na wadau wote wanaohusika katika mradi huo.
“Tutakaa na wadau wote, Udart ni sehemu tu ya wadau, kwa hiyo tutakaa tuone ni kwa namna gani tunazuia au tunapunguza hasara kutokana na mvua.”
Serikali iliwaondoa wakazi wa Jangwani waliokuwa wakiathiriwa na mafuriko kila mwaka kwa lengo la kuwanusuru na majanga lakini mpango huo haukuzigusa ofisi za mabasi hayo yanayoendelea na utoaji wa huduma ya kubeba abiria jijini Dar es Salaam.
Tanesco yawaangukia wateja
Wakati hali ikiwa hivyo Udart, upande wa Tanesco hali pia ni mbaya kiasi cha kulilazimisha shirika hilo kuwaomba radhi wateja wanaokosa huduma ya umeme.
Taarifa iliyotolewa jana na ofisi ya uhusiano Tanesco imesema tatizo hilo limetokana na kuathirika kwa miundombinu kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha ambazo zimesababisha maeneo mengine kuwa vigumu kufikika kwa haraka.
“Mafundi wetu wanaendelea na jitihada usiku na mchana kuhakikisha huduma ya umeme inarejea katika maeneo yote nchini,” inasema taarifa hiyo.
Aidha, Tanesco imetoa tahadhari kwa wananchi ikiwataka wasishike wala kukanyaga nyaya zilizokatika au kuanguka.
Jumatano ya Oktoba 25, umeme ulikatika nchini nzima ikielezwa ni kutokana na hitilafu kwenye gridi ya Taifa.
No comments:
Post a Comment