Leo nitazisema hizi timu kwa kuwa ni siku zao na majina yao hayajayeyuka midomoni mwa mashabiki,
Niliwahi kuyasema haya lakini leo ninarudia kwa ili yawaingie. Unaweza kusema, Simba ni klabu kongwe na kubwa isiyo na maendeleo kama klabu ya Yanga!.
Ndiyo, Simba au Wekundu wa Msimbazi, ukipenda waite Lunyasi au Taifa Kubwa ni miongoni mwa timu mbili zenye mashabiki wengi zaidi siyo tu hapa nchini, lakini katika ukanda mzima wa Afrika Mashariki. Timu nyingine yenye mashabiki wengi ni Yanga, lakini Simba na Yanga hazina maendeleo.
Ukongwe wa klabu hizi mbili na hadhi zao haziendani kabisa na maendeleo yao. Ninasema klabu hizi hazina maendeleo kwa sababu ni kweli hazina viwanja vya mazoezi (Uwanja wa Kaunda haufai licha ya kuzuga kuwa unawekewa vifusi na ule wa Simba Bunju haueleweki), viwanja vya kuchezea mechi zinakodi, hazina wadhamini wengi (klabu inatakiwa kuwa na mdhamini mkuu, washirika katika udhamini, wadhamini kutoka sehemu mbalimbali, wadhamini wa mechi husika), hazina mabalozi wa klabu (zinatakiwa ziwe na angalau wachezaji nyota wanne kwa mwaka waliowahi kufanya vizuri katika klabu hizo, ili wawe wanafanya kazi ya kuwa mabalozi wa klabu hizo), hazina mifuko maalumu kwa ajili ya kuwasaidia wachezaji wao wa zamani (klabu inatakiwa kuwa na harambee za kutafuta fedha kwa ajili ya kulinda historia yake kwa kuwasaidia wachezaji wake wa zamani na wafanyakazi wake), hazina mpango wa kuwawezesha wachezaji wake kupata fursa mbalimbali za kutangaza biashara za makampuni (klabu za Simba na Yanga zina wachezaji wengi wanaochezea timu za taifa na wanaocheza mashindano mbalimbali ya Afrika hivyo zinaweza kuwatumia wachezaji hao kuingia mikataba na makampuni kwa ajili ya kutangaza bidhaa za makampuni hayo), hazina mipango ya bora ya kuibua vipaji na fursa mbalimbali, hazina mipango iliyo wazi ya kibiashara, hazina mipango bora ya kuwasaidia walemavu na watu wenye uhitaji, hazina vituo bora vya kutoa habari (kazi za vituo hivi ni kuelezea matukio mapya ya klabu na mikutano ya habari inayofuata, kutoa taarifa za mechi za klabu, kuelezea mazoezi ya klabu, kuelezea wachezaji n.k), hazitangazi ajira ilizonazo hivyo kuwanyima fursa wanachama na mashabiki wenye uwezo kuomba ajira hizo katika mfumo ulio rasmi, hazina maduka ya bidhaa zao, bidhaa kama Jezi za wachezaji, fulana, skafu, track suit na vitu vingine vingine kwa ajili ya mashabiki wanaume, wanawake na watoto (baadhi ya bidhaa zao zinazouzwa hivi sasa kama vile jezi zinauzwa na wajanja wachache na siyo klabu), hazina rekodi mbalimbali za wachezaji, viongozi n.k.
Hakika kuna vitu vingi vya kimaendeleo ambavyo klabu hizi za Simba na Yanga hazifanyi na hivyo kukosa maendeleo kulingana na umri na mashabiki zilionao.
Ndiyo, Yanga ilianzishwa mwaka 1935 kwa hiyo ina miaka 82 wakati Simba ilianzishwa mwaka 1936 kwa hiyo ina umri wa miaka 81.
Kwa mtazamo wangu, ninawashauri wanachama na mashabiki wa Simba kuwasimamia na kuwafuatilia viongozi wao waweze kuwajibika vya kutosha, wawe na mipango ya muda mfupi na mrefu inayotekelezeka ili klabu ipate maendeleo ya msingi yanayoonekana ili ijitofautishe na watani wao wa jadi Yanga.
Ukweli klabu hazina maendeleo, zinashindwa na Azam!
No comments:
Post a Comment