Adolf Bitegeko ni Kinda la Kitanzania ambalo leo tunalo kwenye rada zetu za Spoti Mikiki ambazo huwa zinawanasa wachezaji wa Kitanzania wanaotafuta maisha ya soka nje ya nchi, nyota huyo anamhusudu sana Paul Pogba wa Manchester United akisema anaweka bidii na anaamini siku moja atafikia kiwango chake.
Tukurejeshe nyuma kabla ya kuendelea mbele na Bitegeko, wiki iliyopita tulikuwa na Aman Kyata ambaye ni Mtanzania wa tatu kuwa naye kati ya wengi wanaocheza Ligi Kuu Kenya. Kyata anaichezea Chemelil Sugar F.C alielezea anavyotamani kuichezea timu ya Taifa Stars.
Leo tunaye Bitegeko ambaye yupo nchini Marekani kwenye Kituo cha Lassen Soccer ambako pia yupo Aboud Doud ambaye tuliwahi kuwa naye miezi kadhaa iliyopita katika ukurasa huu wa wachezaji wa Tanzania wanaokipiga nje ya nchi.
Bitegeko anaamini kupitia siri ambayo amewahi kuisema nyota wa PSG ya Ufaransa, Neymar na ndiyo maana kila siku amekuwa akipambana kuhakikisha anayafikia malengo yake.
Kabla ya kuzungumzia alivyopata nafasi ya kujiunga na kituo cha Lassen Soccer ambacho pia huwajenga wachezaji kwa kuwapatia elimu ya darasani kama kipaumbele cha kwanza alianza kwa kusema ataona fahari siku moja kama akipata nafasi ya kuichezea timu ya Taifa.
“Kuichezea timu ya Taifa ni lengo langu la pili, kwanza kufanikiwa kucheza mpira wa kulipwa, siwezi kuwa mchezaji wa Taifa Stars kama sitokuwa nacheza mpira kwenye ngazi ya ushindani.
“Najua kuwa haitoshindikana kwa sababu ninamwamini sana Mungu, kupitia yeye hakuna jambo ambalo linaweza kumshinda, wote ambao walikuwa na dhamira ya kweli Mungu naye amewasaidia.
“Tanzania sio nchi kubwa kwenye soka hivyo hakuna idadi kubwa sana ya wachezaji wa Kitanzania wanaocheza nje hivyo hata kwenye ufuatiliaji haitokuwa mgumu sana,” alisema mchezaji huyo ambaye anacheza nafasi ya kiungo mkabaji.
Kupata nafasi kwa Bitegeko ya kujiunga na Lassen Soccer haikuwa kwa ujanja na uwezo wake binafsi wa kucheza soka kwa sababu kama uwezo kuna kundi kubwa la wachezaji wa Kitanzania wenye uwezo zaidi yake.
“Nina bahati niseme hivyo kwa kifupi, Mungu amekuwa akinisimamia kuanzia hatua yangu ya kwanza mpaka hapa nilipofika, nimezaliwa 26 Februari 1999 na kukua kisoka nikiwa Karume jijini Dar es Salaam tangu nikiwa darasa la tatu.
“Waliokuwa wakinisimamia ni Eugene Mwasakami, Rogasian Kaijage pamoja na Maalim Salehe. Nimekulia pale mpaka nilipofikakidato cha nne, lakini nilipata nafasi kuchezea timu ya ligi daraja la kwanza ya Ashanti united ila kutokana na shule sikuwa na muda wa kutosha kuwa pamoja na timu.
“Baada ya kumaliza kidato cha sita nikapata nafasi kule Azam FC na nilijiunga na kituo chao na nilikaa kwa takriban mwaka mzima. ni sehemu bora zaidi Tanzania kwa kijana kukaa na kujifunzia soka kutokana na mazingira.
Alijifunza mengi akiwa na Azam na kilichompa nguvu zaidi ya kujengeka, Bitegeko amesema ni ushindani uliokuwepo baina ya wachezaji kwa wachezaji kwa kuwa kila mtu alikuwa anataka kuonyesha uwezo zaidi na kumshawishi kocha wa vijana.
“Ni kwa neema tu ya Mungu nilipata nafasi ya kuchaguliwa kuja kujiunga na hiki chuo ambacho kwa sasa hivi kimetufanya kuwa bize sana na masomo,kila mtu anasomea anachopenda kisha na kucheza mpira.
“Wamerekani hawapendi ujinga kama unakipaji alafu huna elimu ni sawa na bure kama unapenda kucheza mpira basi lazima usome ili maisha ya mpira yakimalizika uweze kumudu kuendesha maisha binafsi nje ya soka.
“Nina miezi minne sasa tangu nijiunge nao, haikuchukua muda kwangu kuendana na mazingira yao japo ni tofauti sana na mazingira ambayo nilikuwa nimezoea kuishi nikiwa Tanzania, kuanzia mwakani nitakuwa kwenye hatua nyingine,” anasema Bitegeko.
Marekani wamelijenga soka lao la chini kwenye mfumo wa vyuo ambao umekuwa ukitambulika sio soka pekee bali hata kwenye upande wa mpira wa kikapu na kwenyewe wanatambua uwepo wa vyuo.
Kuna ngazi tofauti ambazo zimekuwa zikitumika kabla ya mchezaji kuhitimu na kupata timu ya kuichezea ligi (MLS), Ronald Mkaramba naye yupo kwenye mpangilio huo lakini yeye kidogo ni tofauti na wakina Daud na Bitegeko ambao wapo chini yake.
. “Kucheza soka Marekani kunauhitaji wa mambo manne ambayo nimeyaona kupitia vyuoni, usajiliwe kama mchezaji wa kulipwa na timu husika, uanzie kwenye kituo husika cha timu au upitie vituo vichache vilivyopo ambavyo hutoa elimu ya soka tu. “Ubaya wa vile vinavyotoa elimu ya soka pekee sio rahisi mtu kupata timu za MLS pekee.
No comments:
Post a Comment