Wito huo ulitolewa na wataalamu wa mazingira waliokutana jijini Dar es Salaam juzi, kuzungumzia sheria kinzani ambazo zinasababisha hatari za mazingira.
Ambwene Yona kutoka Shirika lisilo la Serikali linalojishughulisha na utunzaji mazingira Mkoa wa Rukwa (Ramso), alisema Ziwa Rukwa lina uwezo wa kulisha wanyama 43,800 lakini mpaka sasa limevamiwa na mifugo 167,900 jambo ambalo ni hatari.
Yona alisema kutokana na uharibifu huo, tayari urefu wa ziwa umepungua kutoka mita tisa hadi tatu na eneo kubwa ni tope.
Aliongeza kuwa iwapo hatua hazitachukuliwa, ziwa hilo wakati wowote linaweza kukauka.
“Hivi karibuni alifika Makamu wa Rais (Samia Suluhu Hassan), akawaambia wananchi wanatakiwa kuendelea na shughuli zao wakiwa umbali wa mita 200 na wasibughudhiwe, kutokana na kauli hiyo wafugaji na shughuli zingine zinaendelea,” alisema.
Akichangia mjadala, Mhadhiri wa Taasisi ya Mafunzo ya Wanasheria Tanzania, Dk Mramba Sist alisema kukinzana kwa vifungu vya sheria mbalimbali za ardhi ndiyo sababu ya uharibifu wa mazingira.
Naye Eden Wayimba kutoka Shirika la Uhifadhi wa Mazingira (Kaeso), alisema migogoro iliyokuwapo Rukwa imesababishwa na wafugaji.
Wayimba alisema kwa sasa kuna uchimbaji holela wa madini, ongezeko la mifugo na shughuli mbalimbali za binadamu.
Alisema jamii kwa namna moja au nyingine ni chanzo kikubwa cha uharibifu wa mazingira, hivyo Serikali ishirikishe jamii kutoa elimu na kutunza mazingira.
No comments:
Post a Comment