Monday, October 16

Msajili wa vyama vya siasa aibua utata sheria mpya ya vyama


Ofisi ya msajili wa vyama vya siasa imeibua utata kuhusu mchakato wa mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa, huku wadau wakitaka iweke hadharani rasimu ya mabadiliko ya sheria hiyo.
Mchakato huo umeanza kunyooshewa vidole na vyama vya siasa na hasa vya upinzani vikidai una lengo la kutaka kuvikandamiza na kuirudisha nchi kwenye enzi cha mfumo wa chama kimoja.
Utata huo unajitokeza katika taarifa kwa umma ya msajili wa vyama vya siasa, Jaji Francis Mutungi aliyoitoa Oktoba 13 akielezea mchakato huo na rejea ya barua yake ya Agosti 28 yenye kumbukumbu namba KA.231/322/01/174 kwenda kwa makatibu wakuu wa vyama kutofautiana.
Katika barua ya Agosti 28, msajili aliwataka wadau kutoa maoni ndani ya wiki mbili baada ya kupokea barua hiyo.
Hata hivyo, katika taarifa ya Oktoba 13, msajili amewataka kuendelea kutoa maoni licha ya muda uliotengwa kupita.
Akizungumzia suala hilo jana, mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano na mambo ya nje wa Chadema, John Mrema alihoji, “Msajili anawezaje kutueleza tupeleke maoni wakati muda aliotupa kwa mujibu wa barua yake ya Agosti 28 umekwisha tangu Septemba 10 na hajaitengua kuwa ameongeza muda.”
Katika barua ya Agosti 28 iliyosainiwa na naibu msajili wa vyama vya siasa, Sisty Nyahoza kwa niaba ya Jaji Mutungi iliyokuwa na kichwa cha habari ‘Maombi ya kupatiwa maoni kuhusu kutungwa kwa sheria mpya ya vyama vya siasa’ ilitoa siku 14 kwa wadau kuwasilisha maoni yao.
Jaji Mutungi alitoa ufafanuzi kwa umma Oktoba 13 baada ya gazeti hili kuripoti kuhusu rasimu ya muswada wa sheria inayopendekezwa kuwa na vifungu vinavyoelezwa na wadau wa siasa kwamba ni kandamizi na unalenga kuviua vyama visivyo na wabunge, madiwani au wawakilishi.
Katika ufafanuzi wake, Jaji Mutungi ambaye hakukana moja kwa moja maudhui yaliyomo kwenye rasimu hiyo ambayo Mwananchi iliiona.
Alisema kilichofanyika kwa ofisi yake ni kuwataka wadau wa siasa kuwasilisha maoni yao kwa ajili ya kutungwa kwa sheria hiyo.
“Ofisi ya msajili wa vyama vya siasa inaelewa kuwa kwa asilimia nyingi sheria inatengenezwa na wadau, hivyo maoni yao ni muhimu katika kutungwa kwa sheria,” alisema Jaji Mutungi akifafanua taarifa iliyoandikwa na gazeti hili kisha akaongeza kuwa;
“Hivyo, kabla ya kuandaa bango kitita la mapendekezo ya kutungwa kwa sheria mpya vya vyama vya siasa, tuliona ni vyema kupata maoni kutoka kwa wadau ili mapendekezo ya sheria yatokane na maoni ya wadau.”
Taarifa yake ilifafanua, “Napenda kutumia fursa hii pia kuwaomba wadau wawasilishe maoni yao kama tulivyowaomba katika barua yenye kumbukumbu namba KA.231/322/01/174. Pia, nawaasa wajiepushe kuzua mijadala na propaganda kwenye vyombo vya habari na mitandao isiyo na tija.”
Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, John Shibuda alisema jana kuwa, “Ile rasimu ilishatoka hata kabla ya maoni kuombwa tupeleke lakini ninachoweza kusisitiza mimi mwenyekiti wa baraza sijui lolote na najiuliza watu wameipata wapi na tena inasambaa mitandaoni.”
Shibuda ambaye ni katibu mkuu wa Chama cha Tadea alisema, “Mawazo au fikra zisizo na malumbano au kusigana hujenga Taifa imara. Mimi ni mwenyekiti na sekretarieti na ofisi ya msajili sasa kama inaandaa kisiri siri wanataka kupanda mbegu gani Tanzania.”
Barua yenye kumbukumbu namba KA.231/322/01/174 aliyoielezea Jaji Mutungi iliyokwenda kwa wadau kuwataka wawasilishe maoni yao ilitoa kipindi cha wiki mbili ambazo ni siku 14 na kwa kuwa iliandikwa Agosti 28, muda wa mwisho kuwasilishwa ilikuwa Septemba 10.
Barua hiyo ilieleza wazo la kutungwa kwa sheria mpya ya vyama vya siasa linatokana na maoni kuhusu mapendekezo ya marekebisho ya sheria ya sasa yaliyowasilishwa na wadau kuwa mengi.
Pia, ilieleza kuwa endapo sheria itarekebishwa bila kuandikwa upya, marekebisho yatakuwa mengi kuliko sheria ya sasa na mtazamo wa sheria ya sasa utabadilika kabisa.
“Aidha, pamoja na ukweli kwamba zoezi la kukusanya maoni ya wadau kuhusu marekebisho ya sheria hii lilianza muda mrefu tangu mwaka 2013, ofisi ya msajili wa vyama vya siasa inaomba maoni yenu yawasilishwe ndani ya wiki mbili kuanzia tarehe ya barua hii ili kuhakikisha mchakato wa kutunga sheria mpya ya vyama vya siasa unakamilika kabla ya kuanza kwa msimu wa Uchaguzi Mkuu unaofuata,” ilieleza barua hiyo.
Zitto atoa ushauri
Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alitoa ushauri kwa ofisi ya msajili kuitisha kikao cha baraza la vyama ili kujadili aina gani ya sheria wanaitaka, lakini hilo halikufanyika.
“Kama msajili anasema si ya kwake basi atoe ya kwake tuone nani mkweli, mimi nimezungumza na viongozi kadhaa wakiwamo wa Chadema na kuelezwa ndiyo yenyewe na mimi nikashiriki kuichambua kidogo, sasa anaposema si ya kwake atueleze yake ni ipi,” alihoji Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Mjini.
“Naendelea kusisitiza kuitishwa kwa kikao cha Baraza la Vyama vya Siasa ili tujadiliane ni aina gani ya sheria tunaitaka, je hii iliyopo imepitwa na wakati au kipi kipungue na kipi kiongezeke.”
Akizungumzia kuvuja kwa rasimu hiyo, mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano na mambo ya mje wa Chadema, Mrema alisema inaweza kuwa imetolewa na watumishi wa ofisi ya msajili baada ya kuona ni mbaya ili izue mjadala mapema.
“Lakini anaposema tupeleke maoni, mbona barua yake ya Agosti 28 ilitoa wiki mbili tu, tukipeleka maoni sasa anayapokeaje wakati muda ulishapita?” alisema Mrema.
“Hiki kilichotokea kimemweka katika wakati mgumu tunasubiri kuona hiyo rasimu atakayoitoa, je itafanana na hii au itatofautiana?”

No comments:

Post a Comment