Thursday, October 5

Viongozi wa dini nchini waeleza wasiwasi wao juu ya hali inayoendelea

Dar es Salaam. Matukio ya uhalifu yanayoendelea nchini yamewaibua viongozi wa dini ambao licha ya kuelezea wasiwasi wao kutokana na kuongezeka, wameitaka Serikali ibuni mikakati ambayo itamhakikishia kila raia usalama wake.
Wamesema kuna haja kwa wananchi kuhakikishiwa usalama kwani woga na hali ya kutokuaminiana iliyoanza kujitokeza miongoni mwao inaweza kusababisha hali kuwa mbaya baadaye.
Viongozi hao wamesema hayo jana walipokutana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba katika kikao kilichofanyika jiji hapa na kuhudhuriwa na Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), James Mbatia.
Ingawa kikao hicho kilikuwa sehemu ya utamaduni wa viongozi wa dini zote kukutana na kujadiliana kuhusu mambo yanayohusu nchi, lakini kwa sehemu kubwa kilitawaliwa na matukio yaliyoanza kuibuka katika siku za hivi karibuni.
Matukio hayo ni pamoja na kushambuliwa kwa Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, vitisho vinavyotolewa kwa baadhi ya makundi ya watu pamoja na tukio la kukutwa kwa miili katika eneo la Coco Beach jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Askofu Alinikisa Cheyo alisema katika majadiliano hayo wamekubaliana kwamba suala la ulinzi wa raia linapaswa kuwa ajenda ya kudumu kwa Serikali bila kujali itikadi.
“Ni muhimu mwanachi ahakikishiwe usalama wake popote pale alipo… potelea yukoje, yuko wapi lakini ahakikishiwe ya kwamba yupo salama,” alisema.
Hii ni mara ya kwanza kwa viongozi hao wa dini kukutana na waziri Mwigulu tangu kuibuka kwa matukio hayo na walitumia fursa hiyo kufanya maombi ya pamoja kumuombea Lissu ambaye anaendelea na matibabu jijini Nairobi.
Sheikh Hassan Said Chizenga kutoka Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata) alisema mikutano ya namna hiyo inawapa fursa waumini wa pande zote kubadilishana mawazo na kisha kukubaliana njia bora zaidi ya kulinda amani ya nchi.
“Huku kukutana tu kwenyewe pia kunasaidia kufuta tofauti zilizopo baina yetu na kuweza kutupa moyo wa kushirikiana sisi kwa sisi na kujua mambo mengine ambayo tulikuwa hatujui,” alisema.
Baadaye waziri Nchemba alimwambia mwandishi wetu kuwa ingawa Serikali inaendelea kuchukua jukumu la kuimarisha ulinzi na usalama, wananchi nao wanapaswa kuchukua tahadhari.
“Wananchi lazima wawe makini maana unaweza ukamkuta mtu anamtuma mtoto kwenda dukani nyakati za usiku wakati sasa kuna haya matukio ya utekaji watoto, kwa hiyo wananchi lazima wazingatie hilo,” alisema.
Alisema Serikali imezipokea hoja zilizotolewa na viongozi wa dini na kwa kuzitilia maanani, inaanza kuangalia namna ya kufanikisha ulinzi wa nyumba kumi.
“Wametupa changamoto na sisi tunazifanyia kazi na tunaangalia uwezekano wa kuanzisha ulinzi wa nyumba kumi,” alisema.     

No comments:

Post a Comment