Thursday, October 5

Kauli ya IGP Sirro yamshangaza Lema


Dar es Salaam. Mbunge wa Arusha Mjini, Gobless Lema amemshangaa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Simon Sirro kwa kauli yake kuhusu dereva wa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.
IGP Sirro akiwa ziarani mkoani Mtwara jana alisema, “Yule kijana ukimuona kwenye picha yuko vizuri tu, sasa wanaposema anapata huduma ya matibabu ya kisaikolojia wakati kwenye magazeti anaonekana vizuri, hii inatupa changamoto.”
Alisema, “Ndugu zangu, mheshimiwa Lissu amepigwa risasi na watu tunaowatafuta, huyo kijana aje. Kuja kwake kutatusaidia kupata majibu ya mambo mengi. Mtu anasema anatibiwa kisaikolojia lakini kila siku nikiona magazeti anaonekana anawaka inanipa tabu.”
Lissu ambaye pia ni mwanasheria wa Chadema alishambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi Septemba 7 akiwa ndani ya gari nje ya makazi yake eneo la Area D mjini Dodoma.
Lema katika video iliyosambaa leo Alhamisi kwenye mitandao ya kijamii ya WhatsApp na Facebook anaonekana akisema kauli ya IGP Sirro ni lugha ya mzaha na hasa kwa familia ya Lissu, dereva aliyeshuhudia tukio hilo na Chadema kwa jumla.
Amesema kauli kuwa dereva wa Lissu anachelewesha upelelezi kukamilika si kweli.

No comments:

Post a Comment