Harare, Zimbabwe. Umoja wa Vijana wa chama cha Zanu PF unataka Rais Robert Mugabe, licha ya umri wake mkubwa, aruhusiwe kufia ofisini hali inayoibua fununu kwamba mzee huyo hana mpango wa kuachia madaraka kwa sasa.
Pendekezo hilo limekuja wakati huu ambao wanachama wengi katika chama hicho tawala kwenye majimbo nchi nzima walikutana mwishoni mwa wiki na kuamua kuitisha mkutano wa dharura Desemba kushughulikia mgawanyiko uliosababishwa na Mugabe kushindwa kumwandaa mrithi wake kwa miaka 37 aliyokaa madarakani.
Mikutano ya kwenye majimbo iliitishwa siku chache baada ya uamuzi toka juu uliofanywa na mkutano mkuu na kamati kuu kutaka uitishwe mkutano mkuu maalumu ili ushughulikie migogoro ya ndani inayotishia kuisambaratisha Zanu PF kuelekea uchaguzi mkuu mwakani.
Mmoja wa makamu wa Mugabe, Emmerson Mnangagwa anadaiwa kuongoza kundi linaloitwa "Team Lacoste" linalohaha kumpigia kampeni aweze kumrithi Mugabe akiondoka madarakani.
Kundi jingine la vijana zaidi linalojiita "Generation 40" linaloungwa mkono na Memsapu Grace Mugabe limeelekeza mashambulizi dhidi ya Mnangagwa wakati jina la Waziri wa Ulinzi Sydney Sekeramayi limeingizwa kwenye vita ya urais na Waziri wa Elimu ya Juu Jonathan Moyo anayemwona kuwa anafaa.
Katikati ya mnyukano huu wa kuwania kumrithi Mugabe, mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Zanu PF, Mubuso Chinguno amesema chama hakina mgombea mwingine zaidi ya mzee huyo mwenye umri wa miaka 93.
"Rais Mugabe ni rais wetu wa maisha. Hatuna tatizo naye hata akifia ofisini kwa hiyo tunakaribisha mapendekezo haya mapya ya kuwepo Kongamano la Mwaka Desemba ambalo litageuzwa kuwa mkutano mkuu maalumu,” alisema Chinguno.
No comments:
Post a Comment