Ni eneo lililotawaliwa na ukimya mkubwa, huku wananchi waishio pembezoni mwa eneo hilo wakituangalia kwa udadisi, kulikoni tunaingia eneo hilo maarufu ambalo hawaruhusiwi kuingia hata kuokota kuni wala kulisha mifugo licha ya kuwa na nyasi nyingi.
Kutokana na ukimya uliopo eneo hilo, Ofisa Mradi wa Tokomeza Ukeketaji wilayani Serengeti, William Mtwazi tuliyeongozana naye analazimika kumpigia simu mmoja wa makatibu wa wazee wa mila kujua waliko ili tuonane nao. Ndipo mzee huyo anamwambia kuwa wapo kwenye msitu wa uamuzi.
Msitu huo au ‘Ikulu’ kama wanavyopenda kuuita, ni sehemu ambayo wazee hao hukutana kufanya vikao na kutoa uamuzi mzito ulioshindikana kutolewa katika vikao vingine katika jamii.
Tukiwa njiani kuingia msituni tunapokewa na mzee wa mila kutoka Kijiji cha Nyamakendo, Ghati Sirirya na kututaka tuache gari letu zaidi ya mita 500 kabla ya kufika msitu wa uamuzi, tunatii agizo na kuanza kumfuata taratibu huku timu yetu ya watu wanne, William Mtwazi, Christopher Genya, Sam Ambokile (dereva) na mimi kila mmoja akiwaza na kuwazua nini kitatokea huko Ikulu tuendako.
Lengo la safari hii ni kwenda kujua msimamo wa wazee hao wa kuachana na ukeketaji baada ya Mei mwaka huu kudai kuwa hawatatoa uamuzi mpaka wawashirikishe wazee wao (mizimu).
Hivyo, kila mmoja anakwenda akijiuliza wazee wao wameamua nini na nini hatima ya usalama wetu.
Mazingira ya nje ya msitu
Mlango wa kuingia msitu wa uamuzi umezingirwa na miti, tunaingia kwa kuinama tukimfuata mzee Sirirya, macho ya udadisi yakiangalia kila kona ili kukariri njia tuliyopitia iwapo kutatokea hali isiyo ya kawaida tuweze kukimbia. Kila tunapopiga hatua utulivu unazidi kuongezeka.
Ghafla tunakutana na jopo la wazee wa mila 23 wenye rika tofauti wakiwa wamekaa nusu mduara wote wamevaa kofia tofauti, pembeni wameweka fimbo zao maalumu, wengi wao mikononi wameshika vikopo vya ugolo.
Mmoja wa wazee aliyeonekana ni kiongozi wao, akainama na kuvuta ugolo kisha akanyanyua macho na kututazama na kuinama tena, harafu akavunja ukimya.
“Karibuni vijana hapa Ikulu, msitu wa uamuzi, tumewaita hapa kuwapa msimamo wetu kuhusiana na suala la ukeketaji,” anasema na kuvuta ugolo.
Anasema kwa utulivu na tahadhari kubwa huku utulivu ukitawala:
“Naitwa Masonoro Marwa, mwenyekiti wa wazee wa mila muungano wa Tanzania na Kenya ukoo wa Inchugu (Wakira) tumewapokea kwa kuwa watu wetu wameonyesha hamna nia mbaya, angalieni juu ya mti mlioegemea kuna nyuki wengi, kama mngekuwa watu wabaya wangewang’ata na kutupa kazi ya kuwabebembeleza.”
“Kwanza mmejipaka marashi mbalimbali hiyo ilitosha kuwafanya wawafuate, lakini kwa kuwa nia yenu ni njema, muwe na amani hao ni walinzi wa eneo inaonyesha wazi kuwa suala la ukeketaji sasa litakwisha, watu wetu wametukubalia kuacha, vinginevyo hata hapa msingefika,” anabainisha kwa mafumbo.
Wakati anamalizia mazungumzo yake, timu yetu yote ilitupa macho juu ya mti tulioegemea tukaona kuna kundi la nyuki, ambao wakati tunaingia hatukuwaona.
Ukimtazama mwenzio unaona jinsi alivyo na hofu, hata hivyo maneno ya mwenyekiti kuwa tusiwe na wasiwasi yanatupa faraja.
Katibu wa wazee wa mila Tanzania na Kenya, Peter Waitacho anaanza kwa kusema: “Muhtasari wa uamuzi wetu wa kikao cha Mei 25, 2017 kilichoshirikisha wazee wa mila 44 tulikuwa hatujautoa kwa kuwa kuna mambo yalikuwa hayajafanyika na kupata ridhaa na baada ya kukutana tumepata kibali.”
Mizimu yagoma picha zisipigwe
Kutokana na maelezo yao ya awali yalinivuta kwa upole nikaomba ridhaa ya kupiga picha na kurekodi mazungumzo yao, baadhi walisema haina shida, lakini mwenyekiti wao akaguna na kisha kuamuru tusubiri kisha akavuta ugolo na kutoka nje ya msitu huku anaongea kwa sauti ya chini.
Maajabu mengine licha ya ukubwa wa msitu huo husikii sauti yoyote hata ya ndege. Baada ya muda mfupi mwenyekiti akarejea akifuatana na wanyama aina ya pimbi na kusogea karibu na wazee kisha wakatulia, kama wangekuwa wameruhusu kupiga picha, ningepata picha nzuri sana.
Baada ya mwenyekiti kuketi anatulia kidogo kisha anasema: “Naomba usipige picha maana wazee wamekataa, nimewauliza wamesema hilo tendo lisifanyike mtapiga tukiwa nje ya msitu, nadhani mmeona watu wetu wamekuja hapa, wamegoma lakini wamekubali tuache ukeketaji,” anasema akimaanisha pimbi.
Anasema msimamo wao wa kukataa ukeketaji hauwezi kupingwa na kundi jingine.
“Wanawake hawana sauti kwenye hili maana ukeketaji unaanzia kwa wazee wa mila na unaishia kwa wazee wa mila na tumekubaliana kuacha, watakaokaidi tutawashughulikia kwa mila na desturi kwa kushirikiana na Serikali,” anabainisha.
Kauli yake inaungwa mkono na mwenyekiti mstaafu wa mila wa ukoo huo, Mwita Taimaha (95) ambaye anaheshimiwa sana, anatoa onyo kwa kauli ya msisitizo.
“Tunakubaliana hapa kuacha, mzee wa mila atakayekiuka na kujihusisha na ukeketaji, ole wake,” anasema.
Kauli yenye msisitizo na amri kutoka kwa mzee Taimaha ambaye ni mshauri wao mkuu wa masuala ya mila inaitikiwa kwa pamoja na wazee wa mila huku baadhi wakisikika wakisema atakayewasaliti hawatamuacha salama.
Wakati mjadala unaendelea akaibuka mzee mmoja wa mila na kudai mpiga picha aruhusiwe sasa kufanyakazi yake huku akiungwa mkono na wenzake kuwa sasa ni ruksa, hata hivyo, kabla sijatoa kamera mwenyekiti wao anauliza swali.
“Mnasemaje, apige picha? Ngoja kwanza,” anadai.
Kisha anamchukua mlezi wake ambaye alimwachia kiti hicho, mzee Taimaha wanatoka nje ya msitu kwa ajili ya kutafuta majibu kutoka kwa watu wao ambao sisi hatukuweza kuwaona, lakini wao walikuwa wanadai wanaongea nao.
Nyuki, ndege wakataa upigaji picha
Wakati wanatoka kuna mambo yasiyo ya kawaida yalitokea, ikiwemo nyuki kama kumi kutoka kwenye mti tuliokuwa tumeuegemea kumfuata mwenyekiti akiwa na mstaafu, huku wazee wakidai kuwa hayo ni baadhi ya mawasiliano na wazee hao.
Wazee hao baada ya kurejea eneo lao ghafla ndege aliibuka na kuanza kulia kwa sauti mbalimbali akiwa juu ya miti tuliyokuwa na baada ya muda wa dakika tatu eneo likawa kimya zaidi na kunifanya niendelee kudadisi maana ya matukio hayo.
Baada ya kurejea mara ya pili, mwenyekiti Masonoro kwa msisitizo akiwa ameshika fimbo maalumu inayoonyesha ukuu wake anasema.
“Majibu yaliyotoka ni kuwa hurusiwi kupiga picha humu ndani, nasema tena hilo halitawezekana watu wetu wamekataa kabisa, utapiga nje ya msitu.”
Tukaambiwa kuwa mlio wa ndege aliyekuwa anasikika tafsri yake anaijua mwenyekiti wao Masonoro na hujitokeza kwa nadra hasa panapokuwa na jambo ambalo linahitaji ufafanuzi baada ya kutokea utata, ndege huyo huleta majibu kwa njia ya milio.
Wasisitiza kutokukeketa
Mwenyekiti wa wazee wa mila, Kata ya Machochwe, Nyandonge Chacha (72) anainuka na kuchukua fimbo ili atoe tamko kwa lugha ya Kikurya akimaanisha.
“Wazee umri wetu umekwenda kusumbuana na Serikali si vizuri, kama mambo mengi ya mila ya kutoboa masikio, kuvaa bangili, kupasua meno tumeacha kwanini hili litushinde?” anahoji.
Anasema kwa kuwa zamani ilikuwa ni lazima watoboe masikio, wavae bangili (vitanki) kwenye mikono na miguu, lakini hayo yote yameisha na hakuna madhara waliyopata, hivyo kuacha ukeketaji hakuna madhara yatatokea kwa jamii zaidi ya faida ikiwamo kusomesha watoto wa kike.
Anasema kabla ya kufanya ukeketaji wao ndiyo hutengeneza dawa zikiwamo za kuzuia damu kuvuja ama kuchezewa, sasa wakishaamua kuacha hakuna mtu wa kupambana nao.
Matumizi ya nguvu ya ziada
Uwezo wa kutafsri ujumbe kupitia milio ya ndege anao mwenyekiti wa wazee wa mila wa koo ya Inchugu (Abhakira) Tanzania na Kenya, Masonoro Marwa pekee yake, anasema utaalamu huo aliwezeshwa na baba yake mzazi ambaye alimwachia mikoba.
Anasema uwezo huo na mwingine ndiyo unamtofautisha na wenzake na ndiyo asili ya kuwa na mikoba ya uongozi, kwa kuwa anatakiwa kuwa na uwezo wa kujua mambo mabaya yanayoweza kutokea katika jamii yake na namna ya kuepusha.
“Kinachoamriwa katika msitu wa uamuzi hakibishaniwi, tunatumia akili yetu na nguvu ya ziada, humu ndani kuna mambo mengi ambayo hamkuweza kuyaona, kuna nyoka mkubwa ambaye tunauwezo wa kumwita akaja, ni sehemu ya walinzi,” anasema na kuzidi kututia hofu.
Anasema tangu Mei walikuwa wakitafuta majibu kutoka kwa ‘wazee’ wao ili kujua kama suala la kuachana na ukeketaji litakwisha. Wakati huo vikao vya wazee wa mila kwenye maeneo yao vilikuwa vikiendelea na mwisho wamehitimisha kwa kukutana wote Ikulu kwa kuwa wamepata ridhaa ya wakubwa.
“Tuna misitu mingi, mikubwa ni miwili huu na Ngarawani, lakini tunapokuja hapa ujue kunatolewa uamuzi makubwa, maana hushirikisha wakubwa wetu kama hawataki jambo wanatujulisha kwa njia wanayoona inafaa, kwa ridhaa yao waliyotupa nasema anayekaidi maagizo kutoka Ikulu hawezi kubaki salama, tutapita kuwatangazia na kuhimiza wasomeshe watoto wa kike,” anabainisha.
Kauli hiyo kutoka msitu wa uamuzi ni ukombozi kwa watoto wa kike wilayani Serengeti ambao msimu wa ukeketaji wamekuwa wakikimbia makazi yao na wanaokeketwa wengi huishia kuolewa badala ya kusoma.
No comments:
Post a Comment