Monday, October 23

Uhuru amgomea Raila


Nairobi, Kenya. Rais Uhuru Kenyatta amesema atakuwa radhi kufanya mazungumzo na kiongozi wa upinzani Raila Odinga baada ya uchaguzi wa marudio Alhamisi.
"Tutazungumza baada ya kupiga kura. Hatuwezi kukaa kujadiliana namna ya kuwanyima watu haki ya kidemokrasia ya kumchagua kiongozi wanayemtaka. Subiri watu waamue,” amesema Uhuru katika mahojiano na vituo kadhaa vya redio vya Kikuyu.
Alipuuza madai ya Raia kwamba wanajeshi wamesambazwa kwenye maeneo ambayo ni ngome ya upinzani akidai ni “propaganda tupu” zenye lengo la kuzusha hofu siku ya uchaguzi.
Rais amesema utawala wake umekuwa akiunga mkono jeshi kulinda mipaka ya Kenya na kushirikiana na nchi jirani kusimamia utulivu wa kieneo.
Uhuru amesema Raila alitoa madai kama hayo kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti lakini alishindwa kuthibitisha. "Hii si mara ya kwanza kwa Raila kutoa madai kwamba serikali ina mpango wa kusambaza askari kwenye maeneo ambayo ni ngome yao. Alifanya vivyo hivyo kabla ya uchaguzi uliopita,” amesema Uhuru.
Raila, ambaye anawahimiza wafuasi wake kususia uchaguzi ujao amedai kwamba utawala wa Rais Uhuru unapeleka majeshi katika ngome zao kipindi hiki unapokaribia uchaguzi wa marudio.
Lakini Uhuru amesema polisi kwa kushirikiana na mashirika mengine ya usalama wa ndani ndiyo yaliyosambazwa kusimamia usalama wa mchakato wa uchaguzi lakini siyo jeshi.
"Hizi ni propaganda na jaribio la kuzusha hofu. Jeshi linasambazwa kulinda mipaka ya Kenya kwa sababu linapaswa kulinda uhuru wa mipaka ya Kenya," amesema.
Uhuru amerudi kusema kwamba hatakaa afanye mazungumzo na kiongozi wa upinzani kabla ya uchaguzi wa marudio na akamshutumu Raila kwa kutumia mbinu ya kutaka serikali ya muungano.
"Nimekataa na nimesema sihitaji mjadala naye. Ninashauku na uamuzi wa Wakenya. Ikiwa anataka kuongoza nchi hii, lazima ukubali kwamba uongozi unapatikana kupitia kura,” amesema.

No comments:

Post a Comment