Urusi imedai majeshi ya muungano ulioongozwa na Marekani ni kama yaliufuta mji wa Raqqa nchini Syria kutoka kwenye uso wa dunia wakati wa vita dhidi ya kundi la Islamic State.
Wapiganaji wa Syrian Democratic Forces (SDF), wanaoungwa mkono na Marekani walitwaa udhibtii wa Raqqa wiki iliyopita.
Kundi hilo hujumuisha wapiganaji wa Kikurdi na wa Kiarabu.
Picha na video zinaonyesha mji wa Raqqa umebaki magofu, na Urusi imefananisha kuharibiwa kwa mji huo na kuharibiwa kwa mji wa Dresden, Ujerumani na majeshi ya nchi za Magharibi wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.
Muungano huo unaoongozwa na Marekani umesema ulijaribu kabisa kupunguza maafa kwa raia.
Urusi yenyewe imetuhumiwa kutekeleza makosa ya uhalifu wa kivita kwa kuangusha mabomu Aleppo mwaka jana.
Wachunguzi wa makosa ya uhalifu wa kivita wa Umoja wa Mataifa mwezi Juni walisema "raia wengi walifariki" Raqqa.
Wanaharakati watetezi wa haki Syria wanasema raia kati ya 1,130 na 1,873 waliuawa na kwamba wengi wa raia waliofariki ni kutokana na mashambulio ya mabomu ya kutoka angani yaliyokuwa yakiangushwa na Marekani kuwasaidia wapiganaji hao wa Kikurdi na Kiarabu kusonga vitani.
Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Urusi amelinganisha uharibifu huo na uharibifu wa Dresden.
"Raqqa imerithi hatima ya Dresden 1945, kufutwa kabisa kutoka kwa uso wa dunia kwa mabomu ya Wamarekani na Waingereza," Meja Jenerali Igor Konashenkov amesema.
Amesema nchi za Magharibi sasa zinaonekana kuharakisha kutuma msaada wa kifedha Raqqa kama njia ya kuficha makosa yao ya kivita.
Muungano wa Marekani umesema ulifuata taratibu zote katika kuamua maeneo ya kushambulia na kwamba walijaribu kadiri ya uwezo wao kupunguza madhara kwa raia.
SDF walitangaza kukomboa Raqqa wiki iliyopita baada ya vita vya miezi minne dhidi ya IS waliokuwa wameudhibiti kwa miaka mitatu.
Wamesema pia kwamba wametwaa udhibiti wa kisima cha mafuta cha al-Omar, chanzo kikuu zaidi cha mapato kwa IS.
Vita vya SDF dhidi ya IS sasa vinaandazia ngome yao ya mwisho Syria katika mkoa wa Deir al-Zour mashariki mwa nchi hiyo.
Jeshi la Syria, likisaidiwa na ndege za kivita za Urusi pamoja na wanamgambo wanaosaidiwa na Iran, limekuwa pia likishambulia IS.
No comments:
Post a Comment