Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango inaendelea na juhudi za kusimamia, kudhibiti na kurahisisha upatikanaji wa taarifa mbalimbali za kifedha ikiwemo mishahara ya watumishi na wastaafu wa Umma. Aidha, Mifuko ya Hifadhi za Jamii, Mashirika ya Bima, Mabenki, Taasisi za Fedha, Saccos na wadau wengine wameendelea kufanikisha utoaji huduma mbalimbali kwa watumishi na wastaafu wa Umma kwa kutumia taarifa za mishahara zikiwa kwenye nakala ngumu.
Hata hivyo, bado kuna changamoto mbalimbali katika upatikanaji wa taarifa hizo ikiwemo kuongezeka kwa gharama za uchapishaji na usambazaji wa nakala ngumu nchi nzima, usumbufu na gharama kubwa kwa watumishi na wastaafu kuzitafuta taarifa hizo Hazina na wakati mwingine kughushiwa.
Kutokana na changamoto hizo, Wizara ya Fedha na Mipango imeandaa mfumo wa kielektroniki wa utoaji wa hati za malipo ya mishahara ya watumishi wa Umma unaojulikana kama “Government Salary Slip Self Service”. Mfumo huu unatumia taarifa sahihi zilizopo kwenye mfumo shirikishi wa taarifa za Kiutumishi na Mishahara (Human Capital Management Information System) wa Serikali ujulikanao kama “Lawson”. Utaratibu wa kujisajili na kutumia huduma hii kwa watumishi wa Umma unatolewa na waajiri wao.
Walengwa na watumiaji wa mfumo huu ni watumishi wa Umma, Wastaafu, Mifuko ya Hifadhi za Jamii, Mashirika ya Bima, Taasisi za Fedha (Mabenki, Saccos) na wadau wengine wanaotoa huduma kwa Watumishi wa Umma na wastaafu kwa kutumia hati za malipo ya mishahara (Salary Slip) ikiwa kwenye nakala ngumu.
Wizara inapenda kuzitangazia Taasisi kuwa, huduma hiyo kwa sasa inapatikana kwa njia ya kielektroniki kwa kutumia internet kwa masharti ya kusajiliwa kwanza ili ziweze kuondokana na matumizi ya nakala hizo ngumu kwa kutumia namba maalum ya mshahara wa mtumishi kwa mwezi husika (salary slip token) inayotolewa na mwajiri wake.
Sifa za kusajiliwa kwa taasisi ni kutuma maombi yanayoambatana na namba za makato (Deduction Codes) za taasisi husika pamoja na orodha ya watumiaji wa mfumo wakiwa na taarifa zifuatazo; Namba ya mtumishi (Employee ID), Majina yake matatu, namba ya simu, anuani pepe, namba ya utambulisho iliyoko kwenye kitambulisho chake cha Taifa au namba iliyoko kwenye kitambulisho cha Mpiga Kura au namba ya hati ya kusafiria.
Taasisi zinazotaka kujiunga na mfumo huu ziwasilishe Maombi kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Barabara ya Jakaya Kikwete, Jengo la ‘Treasury Square’ S.L.P 2802 DODOMA.
Taarifa hii inapatikana pia katika Tovuti ya Wizara (www.mof.go.tz)
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Fedha na Mipango.
No comments:
Post a Comment