Pia, zimesababisha mali za wakazi wa maeneo hayo kusombwa na maji usiku wa kuamkia leo Alhamisi Oktoba 26,2017.
Mvua bado inaendelea kunyesha na imesababisha mitaro na barabara katika maeneo mengi kujaa maji.
Katika eneo la Tegeta Nyaishozi wananchi wamekuwa wakihangaika kutoa maji katika nyumba zao na barabara hazipitiki kutokana na kujaa maji. Mbali na hayo, hakuna huduma za kijamii zinazopatikana.
Akizungumza na Mwananchi mkazi wa Tegeta Nyaishozi, Abuu Magessa amesema mvua imesababisha maafa na hawajui cha kufanya.
"Tumekaa tu, maji yameingia hadi ndani magari yanaelea," amesema.
Mkazi mwingine wa eneo hilo, Said Juma amesema eneo la Ushenzini halipitiki. "Vitu vimelowa vikiwa ndani wananchi wameshindwa kuvitoa, wamebaki wanaviangalia," amesema.
Hayo yakitokea Tegeta, katika daraja la Mbezi Mwisho maji yamejaa hivyo kusababisha magari kushindwa kupita. Madereva wanalazimika kutumia njia ya Goba.
Kutokana na nguvu ya maji, gari la abiria linalofanya safari kati ya Mbezi Mwisho - Makumbusho limesombwa.
Hata hivyo, imeelezwa hakuna mtu aliyedhurika kwa kuwa wote wametoka kwa kupitia madirishani.
No comments:
Post a Comment