Friday, October 27

UCHAMBUZI: Kwa tabia hii ya uchomaji moto nguzo tusitarajie umeme wa uhakika nchini



Lilian Timbuka 
Lilian Timbuka  
Hivi karibuni kuna taarifa zilizotolewa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwamba kuna baadhi ya watu wasiojulikana wanachoma moto misitu na kuharibu miundombinu ya umeme inayojengwa na shirika hilo nchini.
Uharibifu huo umeripotiwa katika mikoa ya Njombe, Ruvuma, Lindi na Mtwara.
Lakini pia, uharibifu huo umebainika kufanyika mkoani Rukwa katika Msitu wa Kirando wilayani Nkasi.
Kaimu Meneja Uhusiano wa Tanesco, Leila Muhaji, anasema uharibifu huo mkubwa wa miundombinu unaathiri upatikanaji wa umeme kwa wateja wa mikoa hiyo wanaopata huduma ya umeme ya njia ya msongo mkubwa.
Mbali ya kukosa huduma, Leila anasema miundombinu hususan nguzo nyingi zinateketea na kusababisha hasara kubwa.
Binafsi nadhani ifike mahali sasa wananchi wote waishio kwenye maeneo hayo wazionee uchungu fedha zao za kodi ambazo zinatumika pia kujenga miundombinu hiyo ya umeme pamoja na kuiokoa kwa manufaa yao na ya Taifa.
Tanesco nao wavitumie ipasavyo vyombo vya ulinzi na usalama vya mikoa kuwabaini wahusika ili wachukuliwe hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.
Kwani kuharibiwa kwa miundombinu hiyo ambayo mingine ni mipya kama ile ya Mradi wa Makambako Songea ni kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.
Kwa mfano katika mikoa ya Njombe na Ruvuma, moto unaounguza nguzo hizo unadaiwa kusababishwa na shughuli za kibinadamu za kuandaa mashamba. Nadhani wataalamu wa kilimo nao waanze sasa kutoa elimu ya uandaaji bora wa mashamba badala ya wakulima kutumia njia ya uchomaji moto, watumie njia nyingine mbadala.
Hivi karibuni, baadhi ya wahariri wa vyombo vya habari waliotembelea Mradi wa Umeme wa Makambako Songea walishuhudia nguzo takribani 19 zikiwa zimeunguzwa huku baadhi zikiwa zimebakia nyaya tu ziking’inia kando ya Barabara ya Songea-Mbinga kwenye Kijiji cha Lipokela.
Sasa vitendo kama hivi vinasikitisha na kutia uchungu. Umefika wakati kwa wananchi kuacha tabia hiyo kwani miradi hii ya umeme inayojengwa kwa kutumia gharama kubwa, inalenga kubadilisha maisha ya wananchi na Taifa kiuchumi.
Kwani kufanya uharibifu huo ni sawa na kuhujumu jitihada za Shirika la Tanesco linalofanya kazi kwa niaba ya Serikali kutatua changamoto ya upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini.
Utamaduni huu wa wananchi mkoani Ruvuma na Njombe wa kuchoma moto nyasi na misitu kwa nia ya kutayarisha maeneo ya kilimo haina tija na ni bora wakaiacha kabisa.
Nilifurahi hivi karibuni nilipomsikia Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dk Binilith Mahenge alizungumzia vitendo hivyo na kuwaagiza viongozi wa serikali kwenye kata na vijiji kuwaelimisha wananchi kuhusu madhara ya vitendo hivyo.
Litakuwa jambo la busara kama viongozi wote wa mikoa wakaweka utaratibu wa kulinda miundombinu hiyo badala ya kulalamika mara umeme unapokatika kwenye maeneo yao bila kujua chanzo cha ukatikaji huo. Hivi karibuni pia ilielezwa kuwa nguzo 101 za umeme ziliteketezwa na kusababisha hasara ya Sh. milioni 121, kutokana na kuwapo kwa vitendo vya uchomaji moto ovyo, vinavyofanywa na baadhi ya wananchi, katika maeneo mbalimbali mkoani Kagera.
Ofisa Mazingira wa Mkoa wa Kagera, Haji Kiselu, alisema jana kuwa nguzo zote hizo zimechomwa moto mwaka huu. Anasema uchomaji huo wa moto unatokana na kutosimamiwa vyema kwa sheria ya mazingira namba 20 ya mwaka 2004, ambayo inaelekeza uundwaji wa kamati kuanzia ngazi za vijiji.

No comments:

Post a Comment