Serikali ilitarajia kuhakiki NGO zaidi ya 8,500 zilizosajiliwa nchini lakini zilizohakikiwa ni 3,186 kwa kipindi cha mwezi mmoja wa uhakiki ulioanzia Agosti 21 hadi Septemba 20.
Akitangaza kuongeza muda huo leo Ijumaa, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Sihaba Nkinga amesema mashirika yatakayoshindwa kufika kwa ajili ya uhakiki yatakuwa yamejifuta.
"Tumeendesha uhakiki wa mashirika katika kanda zote nchini kwa kipindi cha mwezi mmoja, yaliyofika kuhakikiwa ni machache hivyo tunaongeza miezi miwili na watakaoshindwa kuhakiki katika muda wa nyongeza watakuwa wamejiondoa wenyewe," amesema Nkinga.
Katibu mkuu huyo amesema Serikali inapenda kufanya kazi na mashirika yasiyo ya kiserikali kwa sababu ni wabia wa maendeleo lakini wanapaswa kufuata miongozo.
Akitoa taarifa ya uhakiki huo, Tausi Mwilima ambaye ni kaimu mkurugenzi msaidizi ufuatiliaji wa mashirika yasiyo ya kiserikali, alisema yaliyojitokeza kuhakikiwa ni machache kulinganisha na matarajio.
"Katika uhakiki tumebaini mashirika mengi yasiyo ya kiserikali hayatambui sheria na sera zinazoyasimamia, maana hata nyaraka zilizowasilishwa wakati wa uhakiki hazikutimia," amesema.
Mwilima amesema kanda iliyoongoza kwa kuitikia wito wa uhakiki ni ya Mashariki ambayo wamefikia asilimia 34 ya mashirika yote yaliyohakikiwa.
Amesema kanda ya Kati imehakiki mashirika machache ambayo ni asilimia 11 ya yote yaliyohakikiwa.
Ismail Suleiman ambaye ni katibu mkuu baraza la Taifa la mashirika yasiyo ya kiserikali, ameyataka mashirika yasiyo ya kiserikali kutumia vizuri muda wa nyongeza ili kuhakikisha yote yanasajiliwa.
"Tunaomba taarifa za uhakiki huu zitumike kuweka mazingira bora ya ufanyaji kazi kati ya mashirika yetu na Serikali kwa kuwa NGOs zinatoa ajira na zinasaidia jamii," amesema.
Msajili wa mashirika yasiyo ya kiserikali nchini, Masey Katemba amepongeza kuimarika kwa uhusiano kati ya mashirika hayo na Serikali tofauti na ilivyokuwa awali.
Amesema awali, Serikali ilikuwa haikai meza moja na mashirika hayo lakini baada ya kutambua ni wenzao katika kuwaletea wananchi maendeleo wamekuwa wakikaa pamoja.
No comments:
Post a Comment