Wanafanya udhalimu, albino kuwaua,
Tuufanye ukarimu, ni binadamu sikia,
Haki zao tuheshimu, ni wazawa Tanzania,
Mauaji ya albino, acheni mbaya dhamira.
Hiki ni kipande cha ushairi uliotumwa katika gazeti hili na Magdalena Mageresi mwaka 2015.
Hicho kilikuwa kipindi ambacho taarifa nyingi katika vyombo vya habari zilikuwa ni kutamalaki kwa mauaji au kukatwa viungo kwa watu wenye ulemavu wa ngozi.
Ni hatua iliyoifanya Tanzania kuingia katika orodha ya nchi zenye matukio ya aibu na ya kinyama duniani. Wauaji wa albino wakatupa sifa ya uhayawani Watanzania wote.
Duniani kote sifa ikawa Tanzania si mahala salama kuishi kwa watu wenye ulemavu wa ngozi.
Tunakiri zipo juhudi zilizofanyika na ndio maana angalau kwa miaka michache iliyopita, taarifa za mauaji au watu wenye ulemavu wa ngozi kukatwa viungo zilionekana kukoma. Kukawa na kimya kirefu kuhusu taarifa za matukio haya ya kinyama.
Inasikitisha kuwa leo matukio hayo yameanza kurejea nchini. Kumbe kimya kingi kina mshindo!
Kwa mara nyingine vyombo vya habari vimeripoti taarifa ya mkazi mmoja wa Morogoro, Nassoro Msingili (75) kukatwa mkono na kisha walioukata kuondoka nao.
Mkazi huyo mwenye ulemavu wa ngozi, alikutwa na kadhia hiyo Oktoba 3, alipokuwa amelala nyumbani kwake katika Kijiji cha Nyarutanga.
Tukio hili linatudhihirishia kuwa ‘wasakaji’ wa wananchi wenzetu wenye ulemavu wa ngozi, bado wapo na harakati zao zinaendelea. Hatua za kuwadhibiti zilizofanywa miaka iliyopita ama zimefeli au zimepungua nguvu. Ndiyo maana tunapaza sauti tukizisihi mamlaka husika kuamka na kulichukulia suala la mkazi huyu wa Morogoro kwa uzito wa kipekee.
Ni uzito utakaorudisha imani ya wananchi kuwa vyombo vya usalama havijalala na wala havizembei kuwachukulia hatua wasakaji wa watu wenye ulemavu.
Kwetu sisi, ufumbuzi wa kadhia hii wanayoipata wananchi wenzetu, haupaswi kuishia katika kusaka watuhumiwa hasa baada ya matukio na kuwachukulia hatua kali kwa mujibu wa sheria.
Hatuna budi kushughulikia sababu zinazosukuma baadhi ya watu kufanya mauaji au kukata viungo vya watu wenye ulemavu.
Kama uzoefu unavyoonyesha, wapo waganga wa tiba za asili wanaochochea vitendo hivi kwa kuagiza viungo vya watu wenye ulemavu kama sehemu ya tiba zao za kishirikina, kwa fikra kuwa viungo hivyo vinasaidia watu kupata utajiri.
Vyombo vya dola vianze kuwashughulikia waganga hawa.
Kinga ni bora kuliko tiba, kama leo waganga wenye mitazamo ya kishirikina, wanatumika kuagiza viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi, kesho watataka viungo vya watu wanene na wengineo.
Tusifike huko, kama kama Taifa, tusimame kidete kupambana na kila aina ya kiashiria kinachochochea matukio ya kihayawani katika jamii.
Ukiondoa sheria kali dhidi ya watu wanaobainika kuwadhuru watu wenye ulemavu, ni muhimu kuwapo kwa utoaji wa elimu kwa umma kuhusu haki za binadamu.
Lazima Watanzania tuelewe kuwa kila mtu bila kujali hali yake, ana haki ya kuishi na wala utajiri au mafanikio ya kimaisha hayatokani na mtu mmoja kumdhuru mwingine.
No comments:
Post a Comment