Polisi wakieleza namna watu hao walivyouawa walidai kuwa, walipanga kufanya uhalifu nyumbani kwa Meja Makala Erasto wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alidai watuhumiwa hao waliuawa katika majibizano ya risasi na askari usiku wa kuamkia jana.
Mambosasa alidai watuhumiwa waliouawa ni miongoni mwa 20 waliokuwa wamepanga kufanya uhalifu huo.
Alidai wahalifu hao waliokuwa na vifaa vya milipuko na silaha za jadi, walikimbia kusikojulikana baada ya kuona polisi wakisogea eneo la tukio.
Aliendelea kuwa kabla ya kufanya uhalifu, walitega vifaa vya mlipuko ambavyo walipovilipua vilisababisha mshtuko kwa wakazi wa maeneo hayo.
Awali, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Emmanuel Lukula aliliambia gazeti hili kuwa walipata taarifa kutoka kwa wasamaria wema kuwa kuna njama za uhalifu zimepangwa kufanyika maeneo hayo usiku wa kuamkia jana, hivyo walijipanga kwa ajili ya kuudhibiti.
Lukula alidai ilipofika muda walioambiwa, wahalifu hao walifika eneo la tukio na walipambana nao. “Majibizano ya silaha yalikuwa makali kwa sababu walikuwa na silaha nzito, lakini Polisi tulijipanga imara kuwadhibiti,” alisema.
Polisi bandia akamatwa
Polisi imemkamata mtuhumiwa mmoja kwa kujifanya ofisa wa jeshi hilo, huku akidaiwa kuwakamata raia na kupora mali zao kinyume cha sheria.
“Mtuhumiwa alikuwa akifanya uhalifu akiwa na pingu, pikipiki, simu ya upepo na filimbi hii inaonyesha alikuwa anajifanya ofisa wa polisi,” alisema Mambosasa.
Alisema wanaendelea na mahojiano na mtuhumiwa na yakikamilika atafikishwa mahakamani.
Wakati huohuo, Mambosasa alisema katika operesheni waliyofanya ya kudhibiti matumizi ya gongo na dawa za kulevya, wamekamata lita 937 za gongo na mitambo mitatu ya kutengenezea pombe hiyo haramu. Pia, alisema walikamata kete 2,185 za bangi; 35 za cocaine, 32 za heroin na 37 hazijajulikana ni aina ya dawa za kulevya.
“Wananchi waepuke kujihusisha kwa namna yoyote na matumizi ya dawa za kulevya, tunaona madhara yanayowapata wahusika,” alisema Mambo sasa.
No comments:
Post a Comment