Rais Magufuli ambaye hakuwataja wakurugenzi hao, amesema wapo na tayari taarifa zao ameshazipata hivyo waache tabia hizo na badala yake wajikite kuwatumikia wananchi.
Tabia ya ulevi imeonekana kuwa ni dosari kubwa kwa wateule wake, baada ya kutengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwangwa mwaka jana kutokana na ulevi.
Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Kitwanga baada ya kuingia bungeni kujibu swali linalohusu wizara hiyo akiwa amelewa.
“Nimesikia kuna wakurugenzi watatu, wanne waache mara moja na ikiwezekana waokoke kabisa,” ameonya Rais Magufuli wakati wa kufungua Mkutano Mkuu wa 33 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (Alat) unaofanyika Dar es Salaam leo na kesho Jumatano.
Katika mkutano huo uliowakutanisha mameya kutoka mikoa yote nchini, mwenyekiti wa jumuiya hiyo Gulamhafeez Mukadam aliwasilisha changamoto kadhaa ikiwamo hali ngumu ya madiwani hivyo waongezewe posho kutoka Sh350, 000 hadi Sh800,000, ombi ambalo lilikataliwa na Rais Magufuli.
Hata hivyo, Rais Magufuli ameeleza umuhimu wa Alat katika utekelezaji wa Ilani na mikakati yake kwa Watanzania, kubaliana na kuahidi kushughulikia changamoto za uhaba wa watumishi katika halmashauri na ucheleweshwaji na uhaba wa ruzuku za miradi ya maendeleo.
Akijibu mapendekezo hayo, amesema Serikali licha ya kutoajiri mwaka jana, tayari imeshatangaza ajira mpya 52,000 zitakazojaza nafasi zilizoachwa wazi na watumishi hewa zaidi ya 20,000 pamoja na walioondolewa kwa vyeti feki 12,000.
Katika hotuba hiyo, Rais Magufuli alitumia zaidi ya saa mbili kueleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miezi 23 ya uongozi wake, kueleza miradi mipya ya Serikali, dhamira yake katika kudhibiti mitandao ya ufisadi huku akiwataka Watanzania kuvumilia katika mabadiliko aliyoanzisha.
No comments:
Post a Comment