Tuesday, October 3

Kuku mweusi aliyefungwa kitambaa cheupe azusha taharuki


Geita. Ukistaajabu ya Musa utaona ya firauni, ndivyo unavyoweza kusema baada ya watu wasiofahamika kumfunga kuku kitambaa cheupe mithili ya sanda na kumweka nyumbani kwa Emanuel Kabodi, mkazi wa Mtaa wa 14 Kambarage mjini Geita.
Tukio hilo lililovuta watu wengi limetokea leo Jumanne saa 11:00 alfajiri.
Mama wa familia hiyo, Scholastica Nicodemus alipoamka kuanza shughuli za siku alishangaa kumkuta kuku huyo nje ya nyumba yake huku geti likiwa limefungwa.
Akizungumza nyumbani kwake, Nicodemus amesema ni kawaida yake kuamka alfajiri kwa ajili ya shughuli za nyumbani ili baadaye aweze kwenda kwenye biashara zake sokoni.
“Nilivyotoka nje nilikuta kitu kimefungwa na kitambaa cheupe, nilirudi ndani nikamwita mume wangu aje aone. Alitoka kwa hofu nikamwambia asiogope kwa kuwa ameokoka,” amesema.
Nicodemus amesema alimuita mchungaji ambaye baada ya kufungua kitambaa walikuta kuku mweusi akiwa amepitishwa kwenye moto akiwa amefungwa kitambaa cheupe.
Amesema tukio hilo wanalihusisha na ajali iliyotokea juzi Jumapili na mume wake kunusurika kifo baada ya gari lake kuacha njia na kupinduka.
“Kuna mambo ya ajabu, juzi alipata ajali ambayo hata haieleweki. Si mara ya kwanza huwa anakuta chura ndani ya gari kwenye mazingira yasiyoeleweka ila sisi tunamuamini Mungu wala hatuogopi,” amesema Nicodemus.
Askofu wa Kanisa la Pentekoste (TMRC), Stefano Sagada amesema tukio hilo la kuku linaonyesha jinsi watu walivyo na imani haba.
Amewataka wananchi waache kuamini ushirikina na badala yake wamtegemee Mungu.
“Mungu yupo na yeye ndiye zaidi ya kila jambo. Watawatisha kwa vitu vya aina nyingi lakini mkimtazama Mungu yote yatawezekana na adui zenu hawatafanikiwa,” amesema Askofu Sagada.
Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa 14 Kambarage, Justa Fungameza amesema yamekuwepo matukio ya ajabu mtaani hapo yanayohusishwa na ushirikina.
Amesema kwa mwaka huu, tukio hilo ni la tatu baada ya mawili yakihusisha mtoto anayedaiwa kufufuka na mwingine  mchanga aliyezikwa kufukuliwa na mwili kukutwa kwenye boksi pembeni mwa kaburi.
Mjumbe mwingine, Stefano Mayovu amesema kinachosababisha mambo hayo ni chuki binafsi, wivu na wananchi kutoamini Mungu na badala yake kuamini ushirikina.

No comments:

Post a Comment