Tuesday, October 3

Rais Magufuli ataka wakuu wa mikoa waige kwa Makonda


Dar es Salaam. Rais John Magufuli amezungumzia elimu ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa madai kwamba suala hilo lilianzishwa wakati kiongozi huyo alipojaribu kuwakamata wahusika wa dawa za kulevya.
Hata hivyo, alisisitiza kwamba elimu yake (Makonda) siyo kitu kwake na kwamba hata angekuwa hajui kusoma yeye ni bora kwake kwa sababu anafanya kazi nzuri ambayo hata baadhi ya waliosoma hawaifanyi.
Rais Magufuli aliyasema hayo leo Jumanne wakati akifungua mkutano mkuu wa 33 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) uliofanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa pia na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Kauli hiyo ya Rais imekuja ikiwa ni muda mrefu tangu watu mbalimbali walipoanza kuhoji elimu ya Makonda huku akituhumiwa kuwa amefoji vyeti vyake vya elimu. Hata hivyo, Rais Magufuli amesisitiza kwamba mkuu huyo wa mkoa anafanya kazi nzuri na wakuu wengine wa mikoa waige mfano wake.
Rais Magufuli amesema mtu yeyote ambaye atawakamata wauzaji dawa za kulevya ni bora zaidi kwake kwa sababu ataokoa watoto wengi wa Watanzania ambao wanaathirika na dawa hizo huku watoto wa wauzaji wakiwa na maisha mazuri.
“Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alipojaribu kuzungumza kidogo, vita ikawa kubwa kwake, hajasoma hajafanya nini… Mimi hata kama hajui ‘a’ ili mradi anashika madawa ya kulevya huyo ni msomi mzuri.”
“Kwani wenyeviti mliopo hapa wote mmesoma? Kwani halmashauri haziendi vizuri? Kwani hamkupata matokeo mazuri kwenye ripoti ya CAG? Hata wasomi wengine wazuri wametuangusha, kinachohitajika ni uzalendo na kuipenda Tanzania,” amesema Magufuli.
Amesisitiza kwamba wahusika wa dawa za kulevya wakikamatwa nje ya nchi wahukumiwe kwa sheria za huko huko hata kama ni kunyongwa basi wanyonge. Amesema madhara ya dawa za kulevya ni makubwa.
Amesema mtu akishaingia kwenye vita ya dawa za kulevya hawezi kupendwa na wauzaji wa dawa hizo na kuwa yeye hataki wampende bali anataka kuokoa vijana wengi wanaoathirika na dawa hizo.
Rais Magufuli alimpongeza mkuu wa mkoa kwa kazi anayofanya na kuwataka wakuu wengine wa mikoa nchini kuiga kutoka kwake kwa kubuni miradi na kuomba fedha kwa kampuni mbalimbali kwa ajili ya miradi hiyo.
“Waziri mkuu, waambie wakuu wa mikoa wengine waige mfano wa Makonda, anafanya kazi kubwa ya kuomba fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Nimeambiwa kwenye kampeni yake ya nyumba za walimu tayari amekusanya Sh186 milioni,” amesema Rais Magufuli akimwambia Waziri Mkuu Majaliwa.

No comments:

Post a Comment