Wakazi wa eneo la Sabaki kaunti ya Kilifi pwani ya Kenya wamelalamika vikali kuhusu viboko ambao wanawavamia mpaka nje ya nyumba zao, na kuharibu mashamba pamoja na kuingilia mifugo yao.
Kwa kawaidia viboko hao huwavamia usiku kwani wakati huo macho yao huona zaidi ya vile yanavyoona mchana.
Kulingana na mzee wa kijiji, Safari Kadenge Karisa, idadi ya viboko imeongezeka na kuwa zaidi ya mia nne, hivyo basi wengi wao ikifika usiku huvamia wenyeji kwenye makaazi yao.
"Tumechoka na uvamizi huu wa viboko,'' asema Karisa.
"La kusikitisha ni kwamba kila mara tunapopiga ripoti kwa watu wa shirika la huduma la wanyama pori wanachelewa sana kuwasili kutuhudumia tunapovamiwa. Tumeamua endapo KWS hawatatusaidia tutavichinja viboko tupate chakula.''
Spika wa wodi ya Sabaki, Stembo Kaviha anasema: "Tangu lini wanyama wakatawala maisha ya binadamu? Ni binadamu ambaye anatawala lakini sasa wakaazi wa Sabaki tumekuwa watumwa wa viboko. Kufikia saa kumi na mbili za jioni sote tuko ndani ya nyumba na hamna kutoka nje maanake viboko wanazunguka kwenye nyumba zetu. Tumeamua sasa ni vita vya binadamu na wanyama. Na KWS wasiingilie.
"Hapa Kenya tuna janga la Al Shabaab lakini sasa imekua ni Al Kiboko!, wale wengine ni magaidi wa kimataifa lakini hawa viboko ni magaidi wa hapa nyumbani.
"Kuna haja gani watu wa KWS wawe huko Marine Park, kilomita kama kumi na tano kutoka Sabaki. Mbona wasije hapa karibu na viboko wao badala ya kutuachia sisi tuwafanyie kazi yao. Ofisi zao ziko mbali sana.''
Kwa hivi sasa wakaazi wa Sabaki wanaomboleza kifo cha mmoja wao, Kennedy Kenga Charo, aliyeuawa na kiboko kwake nyumbani. Tukio hili limewaudhi zaidi, na wanasisitiza watachukua sheria mkononi mwao kwa kuwaua viboko hao.
Mzee Kenga amemuacha mjane, Sidi Mzungu, na watoto wanane. Mama huyo anawaza na kuwazua jinsi atawalea watoto hao wote, wengine wakiwa bado wako shule ya chekechea.
Mama Mzungu anatueleza jinsi mumewe alivamiwa kwake nyumbani na kiboko.
"Bwanangu alitoka nje aliposikia ng'ombe anapiga kelele, kumbe ni kiboko alimvamia.Kiboko huyo alipomuona bwanangu akamvamia na kumuangusha chini, akamuuma paja na meno yake marefu ya mbele. Alitoa damu nyingi sana hadi akafa.
Mimi nadai malipo ya kiwango cha juu cha kuniwezesha kulea hawa watoto wangu maanake sina mtu mwingine wa kunisaidia.''
Mtoto wake mkubwa, Emmanuel Kenga, anasema huenda ikambidi aache shule (yuke sekondari sasa) amsaidie mamake.
"Tumeachwa na mzigo mzito sana, na kufikia sasa hawa KWS hawajasema lolote vile watatusaidia. Tuko njia panda hatujui tuanzie wapi. Yote haya ni kwa sababu wa viboko.''
Kahindi Safari ni mmoja ya waathiriwa waliovamiwa na viboko lakini kwa bahati nzuri hakumalizwa kabisa.
Safari anatusimulia zaidi: "Mimi nilikua navuka mto Sabaki sehemu ambayo haina maji mengi nikilisha mifugo yangu, ndio nikavamiwa na viboko wawili. Niliamua kujikinga kwa kuingia ndani ya maji, wakanifuata na kunikanyaga kabisa. Naumia sana kwa maumivu ya tumbo, figo, mgongo, shingo na kichwa. Sijapata matibabu ya kutosha. Hata usiku silali kwa sababu ya maumivu."
Mkuu wa shirika la huduma la wanyama pori kaunti ya Kilifi, Jane Gitau, anasema wanajaribu wawezavyo kuwafidia waathiriwa waliovamia na viboko huko Sabaki.
"Kwanza twatoa rambi rambi zetu kwa familia ya mzee Kenga aliyeuliwa na kiboko wetu. Sote tumesikitika mno na tayari tumeanza kushugulikia malipo yake. Tukifuata sheria tutamlipa shillingi milioni tano za Kenya.
"Ni kiwango kidogo kweli lakini hizo ndizo pesa twatoa kuwapa pole waliouliwa na viboko. Hatahivyo twaweza kumsaidia zaidi kulingana na uwezo wetu. Serikali ya kaunti nayo pia itashugulikia familia ya marehemu.''
Hata hivyo baadhi ya waathiriwa wanasema hawajafidiwa na serikali tangu wavamiwe na viboko hao, wakilaumu shirika la huduma la wanyama pori kwa kutilia maanani maslahi ya viboko zaidi ya binadamu.
Jane Gitau amekanusha madai ya wakazi wa Sabaki kwamba wamezembea kwa kuwahudumia ipasavyo.
"Sio kweli tumezembea sisi kama KWS. Tunaelewa shida inayowakabili watu wa Sabaki, na ndio kwa maana kila siku tuko huko. Tatizo ni uchache wa watu wetu wa kazi lakini tutawadumia kikamilifu wakaazi hao.''
Mkuu huyo anasema wanafikiria suluhu ya kudumu kama vile kujenga ua ambalo litawazuia viboko kutoka nje na kuvamia watu kwenye makaazi yao.
Kiboko mkubwa kwa kawaida huwa ana uzani wa kati ya kilogramu 1000 hadi 1,600.
Meno yake mawili ya mbele ni makali sana na ndiyo wanayatumia kung'ata wakaazi wa Sabaki.
Kiboko ni miongoni mwa wanyama hatari zaidi duniani.
No comments:
Post a Comment