Taarifa ya OGP ya Septemba 28 iliyowekwa kwenye tovuti yake inaeleza kuwa licha ya Serikali ya Tanzania kujitoa kwa kuandika barua ya Juni 29, itaendelea kushirikiana na Halmashauri ya Kigoma Ujiji.
Meya wa manispaa hiyo, Hussein Ruhavi aliliambia gazeti hili jana kuwa walipokea barua kutoka ofisi ya OGP ya Washington nchini Marekani Septemba 22, ikiwaarifu kuendelea kushirikiana na halmashauri hiyo.
Alisema mpango wa kwanza wa miezi 15 utakaomalizika Desemba na mwingine utakaoanza mwakani wa miezi 15, utasaidia kutatua changamoto kadhaa kwa lengo la kuwapelekea wananchi wananchi.
“Barua tayari tumeipata, ila mimi nipo Dar es Salaam. Nikirudi Kigoma nitaitisha kikao cha viongozi kikiwamo cha kamati ya fedha tujadiliane tutashirikiana nao (OGP) vipi ikiwa Serikali Kuu imejitoa,” alisema Ruhavi ambaye ni diwani wa Bangwe (ACT-Wazalendo).
“Kwa sasa ni vigumu kusema tutashirikiana nao vipi baada ya Serikali kujitoa. Ila Serikali ituache sisi tuendelee nao kwa kuwa ni jambo jema na linaleta maendeleo kwa wananchi hasa ikichangiwa na uwazi kwa viongozi na watendaji kwa jumla.
“Kama Katiba inasema Serikali Kuu itakaimisha madaraka kwa Serikali za Mitaa, basi hata katika hili.”
Meya huyo alisema Ibara ya 146 ya Katiba inaelezea jinsi Serikali za Mitaa zinavyoweza kuendesha shughuli zake kwa lengo la kuwaletea wananchi maendeleo.
Ibara hiyo inasema, “Madhumuni ya kuwapo Serikali ya Mitaa ni kupeleka madaraka kwa wananchi. Na vyombo vya Serikali za Mitaa vitakuwa na haki na mamlaka ya kushiriki, kuwashirikisha wananchi katika mipango na shughuli za utekelezaji wa maendeleo katika sehemu zao na nchini kote kwa jumla”.
Akizungumzia hilo, mratibu wa OGP Kigoma, Kalila Mchumi alisema wanasubiri barua ya Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
“Siwezi kusema moja kwa moja kwamba tumejitoa. Kikubwa tunasubiri barua kutoka wizarani kwani OGP wamesema wako tayari kufanya kazi na sisi,” alisema.
Mchumi alisema baada ya kujiunga na OGP, utendaji wa viongozi wa halmashauri hiyo kuanzia ngazi za juu hadi chini umekuwa wa wazi na wananchi wanaridhishwa na huduma zinazotolewa. “Ningekuwa mimi, ningeshauri tuendelee kwa kuwa una manufaa sana. Tunapokuwa na tatizo wanatuma wataalamu wanaokuja na vifaa, sasa tukisema tujitoe tutakosa hii fursa. Lakini ngoja tusubiri mkurugenzi na meya tukikutana katika kikao tutajua,” alisema Mchumi.
Taarifa za Tanzania kujitoa OGP zilifahamika wakati wa kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kilichofanyika jijini New York, Marekani Septemba 20 ambako kilieleza kusikitishwa kwake na uamuzi huo.
Tanzania ilijiunga na mpango huo mwaka 2011 hivyo kuwa ya pili barani Afrika ikitanguliwa na Afrika Kusini.
Makubaliano ya OGP yanataka nchi kuondoa kasumba ya kuendesha mambo kwa usiri kati yake na wananchi. Kabla ya kujitoa, Tanzania ilikuwa tayari imepitia hatua mbili za utekelezaji na sasa ilikuwa ikijiandaa kutekeleza mpango mkakati wa tatu uliokuwa uanze 2016/17-2017/18.
Katika mipango hiyo, Tanzania ilikuwa imeainisha maeneo saba ya kuweka mkazo kama Sheria ya Haki ya Kupata Habari, bajeti ya uwazi, Uwazi katika ardhi na madini.
Zaidi ya nchi 70 duniani zimetia saini mpango huo unaohimiza dhana ya uwazi na ukweli, ambao Rais mstaafu Jakaya Kikwete alikuwa mstari wa mbele kuunga mkono na alifanikisha kufanyika kwa mkutano wake kwa mara ya kwanza nchini mwaka 2015
No comments:
Post a Comment