Sunday, October 1

DC apambana na sifuri kwa kuanzisha mfuko maalumu


Siku chache zilizopita, taarifa za kusikitisha katika sekta ya elimu ziliibukia wilayani Mkuranga ambako baadhi ya wana jamii wameshindwa kudhibiti uwapo wa mila hatarishi zinazochangia mdondoko wa wanafunzi wa kike.
Takwimu zinaonyesha wanafunzi 7,151 walioandikishwa darasa la kwanza mwaka 2011 wilayani humo waliotarajiwa kuhitimu mwaka huu kati yao 963 walikatisha masomo.
Hata hivyo, mila inayolalamikiwa kudidimiza elimu wilayani humo ya wasichana wengi kuchezwa ngoma imegeuka kuwa kikwazo na miongoni mwao huishia kufanya majaribio ya mafunzo wanayopewa unyagoni na matokeo yake huacha shule.
“Mwanafunzi anapopelekwa kwenye unyago akili yake inabadilika, ni wachache sana ambao wanaweza kurudisha mawazo yao darasani, wengi wanafikiria jinsi ya kuyafanyia kazi mafunzo waliyoyapata,” anasema mdau wa elimu, Tabia Mohamed.
Ofisa Maendeleo ya Jamii wa wilaya hiyo, Peter Nambunga alieleza kuwa Serikali inaendelea kukabiliana na na suala hilo pamoja na lile la ngoma za vidogoro vinavyofanyika nyakati za usiku vijijini. “Tumeliona hilo na sio hilo pekee kuna suala la vigodoro, kuonyesha video haya yote yanaleta changamoto ila tumeshawapelekea madiwani tunasubiri watunge sheria,” anasema Nambunga
Katika mwendelezo huohuo wa kupambana na ujinga mkoani Pwani, Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Happiness Seneda amesema kwamba nao wapo nyuma kielimu baada ya kugundua idadi kubwa ya wanafunzi wanapata sifuri kwenye mitihani ya kidato cha nne.
Seneda alisema hali ya elimu wilayani hapa inasikitisha, licha ya jitihada za Serikali kutilia mkazo suala la elimu bure nchini.
Alisema mwaka 2016 wahitimu wa kidato cha nne walikuwa 960, lakini waliopata sifuri walikuwa 457 huku mwaka 2015 kulikuwa na wahitimu 820 na waliopata sifuri walikuwa 334, ilhali mwaka 2014 kulikuwa na sifuri 134. Mkuu huyo wa wilaya alisema ili kutatua tatizo hilo kuanzia kesho kutakuwa na akaunti maalumu benki ambazo wadau wa elimu watatangaziwa ili wachangie kuiboresha.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Hamisi Dikupatile alisema fedha zitakazopatikana zitasadia watoto waliopo kwenye kambi za kujisomea na kuboresha miundombinu ya elimu, nyumba za walimu na vifaa vya kujifunzia.

No comments:

Post a Comment