Jinja, Uganda. Polisi juzi ni kama walikuwa wanacheza mchezo wa kujificha na kuibuka ili kupambana na vijana wenye hasira waliovamia nyumba ya mbunge wa Jinja Mashariki, Nathan Igeme Nabeta kwa lengo la kutaka kuichoma moto.
Vijana hao wanamshutumu mbunge wao kwa kupuuza matakwa yao badala yake mbunge huyo amekwenda kuunga mkono mswada tata wenye lengo, pamoja na mambo mengine kuondoa ukomo wa umri wa rais kwenye Katiba ya Uganda.
“Tunamuona mbunge wetu kila siku kwenye TV akizunguka kufanya mashauriano na umma juu ya kampeni ya kuondoa ukomo wa umri wa rais, lakini mbunge huyu hajatenga muda kuja kwetu azungume nasi kuhusu mada hiyo,” alisema Paul Onyango, mmoja wa vijana hao.
Tayari vijana hao walikwisha kufika kwenye nyumba ya mbunge huyo na kuanza kuchoma matairi kwenye lango la kuingilia kabla polisi hawajafika na kuwatawanya. Polisi hao ndio walianza kufanya kazi ya kuzima moto huo.
Naibu kamanda wa polisi wa mkoa wa Kiira Onesimus Mwesigwa alithibitisha kutokea kwa tukio hilo juzi na kwamba mtuhumiwa mmoja amekamatwa na wengine wanasakwa.
Mjini Mbale, Polisi walimtia ndani katibu mkuu wa Forum for Democratic Change (FDC), Nathan Nandala Mafabi kwa madai ya kuchochea vurugu baada ya kuongoza maandamano kupinga Marekebisho ya Katiba yenye lengo la kufuta ukomo wa umri wa rais.
Nandala alikamatwa Ijumaa, mita chache kutoka kampasi ya Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Mbale alipokuwa anaelekea kwenye jimbo lake akiwa amefuatana na kikundi cha wafuasi wake.
Hadi jioni Nandala bado alikuwa anashikiliwa katika kituo cha polisi cha Mbale pamoja na wenzake wawili waliotambuliwa kuwa ni Emmanuel Masaba na Abdulah Magambo.
Nandala ambaye ni mbunge wa Budadiri Magharibi wilaya ya Sironko alitarajiwa kufanya mkutano wa mashauriano jana Jumamosi.
No comments:
Post a Comment