Sunday, October 22

Wanafunzi waanzisha vurugu shuleni


Geita. Vurugu kubwa zimeibuka katika Shule ya Sekondari Geita baada ya wanafunzi wa kidato cha tano na sita kutishia kuchoma shule kushinikiza wenzao wanne wanaoshikiliwa na polisi waachiwe.
Polisi Geita inawashikilia wanafunzi wanne wa shule hiyo tangu Alhamisi baada ya kumpiga, kumjeruhi na kutishia kumuua  mwenzao wa kidato cha tano.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Isaya Busagwe amesema mwanafunzi huyo alipigwa Jumamosi iliyopita na walimu waligundua tukio hilo baada ya aliyepigwa kuugua na kuomba ruhusa ya kwenda nyumbani kutibiwa.
Jana Ijumaa Oktoba 20, wanafunzi hao waligoma kuingia darsani, badala yake, waliandamana kwenda kituo cha polisi kushinikiza wenzao kuachiwa huru.
Baada ya juhudi zao kugonga mwamba kwa polisi kuendelea kuwashikilia wenzao, wanafunzi hao walirejea shuleni na kuanza kurusha mawe wakitishia kuchoma moto majengo wakishinikiza wajumbe wa bodi waliokua wakiendelea na kikao shuleni hapo kutatua suala hilo.
Leo Jumamosi asubuhi, wanafunzi hao walianzisha vurugu zingine, hali iliyolazimisha jeshi la polisi kuingilia kati na kufanikiwa kuzidhibiti.
Mkuu wa Polisi Wilaya ya Geita(OCD), Ally Kitumbo aliyeongoza kikosi cha kutuliza ghasia kudhibiti vurugu hizo hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo akisema yeye siyo msemaji na kazi yake ni kulinda amani na utulivu.
Katika vurugu hizo mwandishi wa habari hii naye amejikuta akiwekwa chini ya ulinzi na kunyang'anywa simu na askari polisi kabla ya kunusuriwa na OCD na kuruhusiwa kuendelea na kazi

No comments:

Post a Comment