Sunday, October 22

Azikwa nyumbani kwao Monduli Juu


Monduli. Mtoto mwisho wa waziri mkuu wa zamani, hayati  Edward Sokoine, Tumaini Sokoine amezikwa leo Jumamosi nyumbani kwao Monduli Juu  mkoani Arusha huku utata wa kifo chake ukiendelea.
Tumaini ambaye ameacha mke na watoto watatu amezikwa na viongozi mbalimbali wa Serikali waliongozwa na Mkuu wa Mkoa Arusha, Mrisho Gambo  na waziri mkuu mstaafu Edward Lowassa.
Akitoa salamu za Serikali katika msiba huo Gambo alieleza kupokea kwa masikitiko msiba huo.
"Kwa niaba ya Serikali na Rais John Magufuli tumepokea kwa masikitiko msiba huu na tunatoa pole kwa familia," amesema 
Amesema kifo ni jambo ambalo litamkuta  kila binadamu kutokana na sababu mbalimbali .
Katika msiba huo ambao ulifanyika kwenye makazi ya hayati Sokoine, waliopata fursa ya kutoa Salamu walikuwa ni Gambo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Lekule Laizer na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Azizi Mlima na wote walitoa pole kwa familia.
Utaratibu huo ulielezwa umewekwa kuepuka msiba kutumika kama uwanja wa kisiasa.
Akitoa shukrani katika msiba huo Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Joseph Sokoine aliwashukuru wote waliojitokeza.
Balozi Sokoine ambaye ni kaka wa marehemu pia alishukuru Serikali  kwa mchango mkubwa tangu umetokea msiba huo.
Hata hivyo kifo cha Tumaini bado kimeacha maswali kwani wakati msemaji wa familia Lembrice Kivuyo akisema alifariki baada ya kuanguka akipanda ukuta kuingia nyumbani kwa Sokoine, polisi inaeleza amefariki kutokana na ugomvi wa familia yake.
Kamanda wa Polisi Mkoa Arusha, Charles Mkumbo amesema watu wawili wanashikiliwa kwa mahojiano kutokana na kifo hicho

No comments:

Post a Comment