Wednesday, October 4

Kaimu rais amjeruhi kwa maneno makamu wa rais


Harare, Zimbabwe. Makamu wa rais anayekaimu urais wa Zimbabwe, Phelekezela Mphoko amemjeruhi kwa maneno makamu mwenzake Emmerson Mnangagwa kwamba haheshimu mamlaka ya Rais Robert Mugabe na kuwa anakuza migogoro ya kisisa.
Shutuma dhidi ya Mnangagwa zimekuja siku chache baada ya Jumamosi kuhutubia watu wakati wa kumbukizi ya kifo cha aliyekuwa Seneta wa Gutu, Shuvai Mahofa, ambako alirejea kauli yake kuwa alipewa sumu.
"Mimi sikuwepo alipofariki dunia lakini kile kilichotokea mama huyu mwaka 2015 eneo la Victoria Falls ndicho pia kilinitokea nilipokuwa Gwanda," Mnangagwa alikaririwa akisema.
Matamshi hayo ya Mnangagwa yanakinzana na aliyotoa mapema na aliyowaji kutoa Mugabe kuhusiana na ugonjwa uliosababisha akasafirishwa kwa ndege hadi Afrika Kusini kwa matibabu.
Mugabe, wakati wa mkutano uliofanyika Gweru mwanzoni mwa Septemba alidai kwamba madaktari wa Mnangagwa walimwambia ugonjwa uliokuwa unamsumbua haukutokana na kupewa sumu.
Siku moja kabla, Mnangagwa mwenyewe alitoa taarifa iliyokuwa inakanusha madai kuwa aliugua baada ya kula ice cream ya Gushungo Dairy, kampuni inayomilikiwa na Grace Mugabe anayehusishwa na kundi la kampeni za urais ndani ya Zanu PF liitwalo Generation 40.
Mphoko na Mnangagwa wote ni makamu wa rais lakini wako kambi mbili tofauti ndani ya Zanu PF. Wakati Mphoko yuko kundi la G40, Mnangagwa yuko kundi la Lacoste katika vita ya kuwania kumrithi kiongozi wa sasa mwenye umri wa miaka 93 na aliyeongoza tangu Zimbabwe ilipopata uhuru mwaka 1980.
Akitaja mgongano huo, Mphoko katika taarifa yake iliyotolewa Jumanne alihitimisha kuwa Mnangagwa anajitahidi kuongeza nguvu katika vita vyake ya kuwania madaraka kupitia siasa za kumchimba chinichini Rais Mugabe.
"Kwa maelezo hayo hapo juu, madai ya Mnangagwa ya hivi karibuni kwamba alilishwa sumu alipokuwa Gwanda hayawezi kupita bila kupingwa, na hiyo ni kwa sababu kila mmoja anaweza kuona ni mawazo yaliyopangwa kupinga maelezo aliyotoa hadharni Mugabe kwamba madaktari wa Mnangagwa walitupilia mbali sababu za Mnangagwa kuugua na kuanza kutapika na kuharisha kule Gwanda," amesema Mphoko.

No comments:

Post a Comment