Wednesday, October 4

Tanzania yaongoza kwa sera bora za uzalishaji nishati


Dar es salaam. Tanzania imetajwa kuwa nchi pekee ya Afrika kwa kuwa na sera bora za uzalishaji wa nishati hivyo kuwavutia wadau duniani kuwekeza.
Akizungumza leo Jumatano wakati wa uzinduzi wa ripoti ya uendelezaji wa vyanzo vidogo vya nishati barani Afrika, Lily Ordano kutoka taasisi ya kimataifa ya rasilimali (WRI) amesema kuna ombwe kubwa la utafiti wa nishati lakini linaweza kuzibwa na sera zilizopo Tanzania.
"Tulihitaji kuwa na nchi yenye sera bora za kusaidia uendelezaji wa nishati endelevu,  ndiyo maana tumeichagua Tanzania kufanya utafiti huu," amesema Ordano.
Amezitaja nchi nyingine zenye miradi midogo ya umeme kuwa ni Kenya, Uganda na Rwanda.
Mkurugenzi wa Shirika la Kuendeleza Nishati Asilia (Tatedo) linaloshirikiana na WRI, Estomih Sawe amesema Tanzania itafaidika kwa kupata taarifa za kutosha kuhusu nishati na kuongeza watumiaji wa umeme katika vyanzo vidogo.
Amesema mbali ya gridi ya Taifa, Tanzania ina vyanzo vidogo vya umeme zaidi ya 100 vinavyosaidia kuongeza watumiaji wa umeme na hasa vijijini.
"Mpaka sasa asilimia 32 ya Watanzania wanapata umeme, tunatarajia itafika asilimia 75 ifikapo mwaka 2035," amesema  Sawe.
Kamishna Msaidizi wa Nishati kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Edward Ishengoma amesema asilimia 75 ya watumiaji wa umeme itafikia mwaka 2030 kutokana na mikakati iliyowekwa na Serikali.

No comments:

Post a Comment