Wednesday, October 18

Kaburi la mfumo wa vyama vingi linapoandaliwa


Historia ya mfumo wa vyama vingi nchini inaanzia miaka ya 1950, wakati Tanganyika ikidai uhuru chini ya chama cha Tanganyika African National Union (Tanu). Vyama vingine vilivyokuwapo ni African National Congress (ANC), All Muslim National Union of Tanganyika (Amnut) na United Tanganyika (UTP).
Uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi uliofanyika 1958 na Tanu ilifanikiwa kupata ushindi mnono baada ya kupata viti 28 kati ya viti 30 vilivyokuwa vikishindaniwa. Mwaka 1960 ulifanyika uchaguzi wa wabunge na Tanu kikaendeleza ushindi wake kwa kupata viti 70 kati ya viti 71 vilivyokuwa vikishindaniwa.
Tanganyika ilipata uhuru wake Desemba 9, 1961 chini ya Tanu iliyokuwa ikiongozwa na Mwalimu Julius Nyerere, awali akiwa Waziri Mkuu.
Uchaguzi wa tatu ulifanyika Novemba Mosi mwaka 1962 baada ya uhuru, kabla ya Tanganyika kuungana na Zanzibar.
Hata hivyo, mfumo wa vyama vingi ulifutwa mwaka 1965 na kuanzia wakati huo Tanu kikawa chama kilichoshika hatamu za uongozi.
Mwaka 1977 Tanu iliungana na ASP ya Zanzibar na kuunda Chama cha Mapinduzi (CCM) kilichoendeleza mfumo wa chama kimoja hadi mwaka 1990.
Tanzania ilirejea katika mfumo wa vyama vingi vya siasa Julai 1992. Kilikuwa kipindi muhimu na cha mafanikio kwa wanaharakati wa mageuzi kama Mabere Marando, James Mapalala, Bob Makani na Edwin Mtei na wengine ambao waliongoza harakati hizo za kupigania mfumo huo.
Harakati za kudai kurejeshwa mfumo wa vyama vingi zilikolea nchi nzima na mwaka 1991, Rais Ali Hassan Mwinyi aliteua Tume iliyoongozwa na Jaji Mkuu, Francis Nyalali kukusanya maoni ya wananchi na kutoa mapendekezo kujua kama taifa lilihitaji mfumo wa vyama vingi au kuendelea na mfumo wa chama kimoja.
Harakati hizo zilisababisha kubadilishwa kwa Katiba ili kurejesha mfumo huo ambao ulikuwa umefutwa Januari 14, 1963 kwa Azimio la Halmashauri Kuu ya Tanu.
Kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi kulisababisha kuanzishwa kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambayo kwa mujibu wa Sheria namba 5 ya mwaka 1992, mbali na kusajili vyama anapaswa kuhakikisha sheria hiyo inafuatwa na vyama vya siasa.
Chama cha siasa kinatakiwa kuonekana kikifanya siasa wakati wote bila kujali vikwazo na changamoto zilizopo. Hii maana kuepuka vyama ambavyo vinaibuka nyakati za uchaguzi vikidai vinaomba vichaguliwe kuongoza nchi.
Lakini, kwa miaka ya karibuni matumaini ya vyama hivyo kufanya siasa kwa uhuru yamekuwa na wakati mgumu, hasa baada ya Serikali kupiga marufuku shughuli za vyama vya siasa ikiwamo mikutano ya hadhara na maandamano.
Wakati vyama vya upinzani vikikosa fursa ya kufanya mikutano, hivi karibuni Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini imeandaa rasimu ya muswada wa Sheria ya Vyama Vingi ambayo itarekebisha sheria ya mwaka 1992.
Hata hivyo, rasimu ya muswada huo ambayo bado haijawekwa hadharani tayari imezua mjadala na baadhi ya vyama vya siasa vimetoa kauli ya kuipinga.
Vyama hivyo vimezua mjadala baada ya kupata mwaliko wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa uliowataka kupeleka mapendekezo ya marekebisho.
Vyama vya siasa
Kiongozi wa kwanza kuujadili muswada huo alikuwa ni Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe ambaye anataja vifungu 71 vya muswada huo akisema ni ‘Hukumu ya Kifo’ Kwa mfumo wa vyama vingi Tanzania.
Katika nadiko lake aliloliweka katika ukurasa wake wa Facebook Agosti mwaka huu, Zitto alionya kuhusu mpango wa Serikali kutunga sheria itakayoweka mazingira magumu kwa vyama vya upinzani kufanya shughuli zake.
“Muswada huo ni hukumu ya kunyongwa mpaka kufa kwa vyama vya upinzani nchini. Ni vifungu 71 vya hukumu ya kifo,” anasema Zitto na kuongeza:
“Kuna watu walipoteza maisha yao kwa ajili ya kupigania uwepo wa demokrasia nchini kwetu. Haikuja tu. Haikushuka kutoka mbinguni, ilipiganiwa. Watanzania wa sasa hawatakubali nchi kurudi kwenye utawala wa chama kimoja kamwe,” anasema Zitto.
Akitaja kifungu cha 45 (1) a-c) vinavyopingana na kifungu cha 45 (2).
“Yaani 45(1) inatoa ruhusa kwa vyama kufanya mikutano halafu 45(2) inasema watakaofanya mikutano ni wabunge na madiwani tu kwenye maeneo yao,” anasema Zitto na kuongeza:
“Tutaipinga sheria hii dhalimu ndani na nje ya Bunge. Tutalinda mfumo wa vyama vingi nchini kwetu kwa gharama yeyote ile kwani uwepo wa vyama ni haki ya kikatiba na haki hiyo haiwezi kunyang’anywa na mtu mmoja.”
Amewataka Watanzania kujiandaa na harakati za kuilinda na kuitetea Katiba.
“Wananchi ndio jeshi la mstari wa mbele la ulinzi wa Katiba. Tusimame kukataa kurudishwa kwenye chama kimoja. Umoja wa ulinzi wa demokrasia (Democratic Front ) Ni muhimu zaidi hivi sasa kuliko wakati wowote katika miaka 25 ya uwepo wa demokrasia yetu.
Vyama vingine vyauzungumzia
Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema anasema wanapinga sheria hiyo kwa kuwa haitekelezeki.
“Hilo jambo tulishalipinga tangu mwanzo, kwa sababu maandalizi ya uchaguzi huanza mara uchaguzi tu unapokwisha. Unapokataza mikutano ya hadhara utakutana vipi na wanachama wako na kutafuta wanachama wapya?” alihoji Mrema na kuongeza:
“Vyama vya siasa ni taasisi zinazoishi, ni sawa na taasisi za dini, huwezi kuzuia mikutano.”
Alisema kama sheria hiyo itapitishwa itasababisha ukabila na ukanda unapigwa vita. “Leo unamtaka Zitto afanye mikutano jimboni kwake Kigoma peke yake wakati yeye ni kiongozi mkuu wa chama chake, atafanyaje? Kwa mfano katika jimbo la Hai CCM haina mbunge wala diwani hata mmoja, kwa hiyo isifanye siasa kabisa? Chadema ina madiwani wanne tu Geita tutafanyaje wakati tunataka kuwaongeza?” alihoji.
Anasema watafanya mkakati wa kuipinga sheria hiyo kwa njia yoyote huku akimtaka msajili wa vyama vya siasa nchini kuachana na sheria hiyo.
“Nchi hii kila mtu yuko huru kwenda kokote anakotaka kwa mujibu wa Katiba, haiwezekani tukawa na sheria ya ajabu kama hiyo. Tunaye msajili ambaye ni jaji hatuamini kama anapeleka sheria mbovu kama hiyo,” anasema Mrema.
Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa Chama cha Wananchi (CUF), upande unaotambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Abdul Kambaya anasema licha ya kutouona muswada huo, hawakubaliani na mapendekezi yake.
“Tulichopewa sisi ni sheria yenyewe ya mwaka 1992 ili tutoe maoni. Lakini, kama ndiyo hivyo hatukubaliani na muswada huo. Kwa mfano, unaposema mkutano ufanywe na mbunge kwenye jimbo lake, kuna vyama ambavyo havina wabunge kabisa, vifanye siasa wapi? kuna vyama havina madiwani vitafanyaje?” alihoji na kuongeza:
“Katika mapendekezo yetu tumepinga kabisa hayo. Halafu unaposema chama kikitaka kufanya mkutano lazima kitoe taarifa kwa ofisa wa polisi aliyepo, hilo pia halikubaliki.”
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, kanali mstaafu Ngemela Lubinga, alipoulizwa kuhusiana na muswada huo alimtaka mwandishi wa habari kumtafuta Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole ambaye naye hakupokea simu licha ya kuita kwa muda mrefu

No comments:

Post a Comment