Wednesday, October 18

Siasa ikitawaliwa na ushabiki matokeo si chanya kwa Wote


Kwa vyoyote vile siasa ni lazima iwe na kiasi fulani cha ushabiki. Na hasa kama ni siasa ya vyama vingi vya siasa kama ilivyo kwa Tanzania. Penye ushindani lazima ushabiki uwepo. Sera na itikadi ni tofauti na tujuavyo vyama vyote vya siasa vinalenga kushika dola. Hivyo huwezi kukwepa ushabiki ndani ya ushindani.
Lakini, ushabiki kama ule wa kushindwa mpira mtu akamalizia hasira yake kwenye viti kama tulivyoshuhudia kwenye uwanja wetu wa taifa, huo ni ushabiki wa kupitiliza. Au ushabiki wa mtu kuyatoa maisha yake kwa vile timu yake ya mpira imeshindwa, ni ushabiki wa kupitiliza. Labda ni bahati mbaya kabisa kwamba hapa Tanzania, tunataka kufananisha ushindani na ushabiki wa kisiasa na ule wa kwenye timu zetu za mpira. Kwa kiasi kikubwa siasa zetu zinatawaliwa na mapenzi na ushindani.
La kuzingatia hapa ni kwamba ni ushindani ndani ya taifa moja. Ni ushindani wa watu wenye haki sawa ya kuishi na kumiliki rasmali za taifa lao. Ni ushindani ndani ya taifa lenye tunu zake; tunu ambazo haziondolewi na utofauti wa sera wala itikadi. Mfano, lugha ya Kiswahili ni tunu ya taifa letu. Hatutegemei ushindani wowote ule wa kuondoa tunu hii! Madini, mbuga za wanyama ni tunu za taifa letu. Hatutegemei ushindani wa kuziongoa tunu hizi mikononi mwa wananchi. Mito, maziwa na bahari ni tunu za taifa letu. Hatutegemei ushindani wa kuuza tunu hizi! Tanzania ina makabila mengi, hii ni tunu ya taifa letu. Hatutegemei ushindani wa kuondoa tunu hii na kufuta makabila ya Tanzania. Umoja wetu, amani na mshikamano ni tunu za taifa letu. Hatutegemei ushindani wa kuondoa tunu hizi. Ushabiki ukiitawala siasa, kuna wasi wasi wa kuacha kuyaona haya.
Mfano tuna Mwenge wa uhuru. Hii ni tunu ya taifa letu. Rais Magufuli, katika hotuba yake ya kuuzima Mwenge wa uhuru kule Zanzibar ameeleza kwa kirefu faida za Mwenge huu na tunaunga mkono. Hatutegemei ushindani na ushabiki wa kufikia kuondoa Mwenge wetu wa uhuru. Na Rais, asiseme wakati wa utawala wake, ni kwamba Mwenge ni tunu ya kudumu. Ni bahati mbaya kwamba ushabiki wa kisiasa umetawala zaidi hadi Mwenge huu umetekwa nyara na CCM. Sherehe za Zanzibar za kuuzima Mwenge zilikuwa ni za kitaifa! Lakini picha iliyojitokeza hapo ni mkutano wa CCM! Hii ni changamoto kubwa iliyo mbele ya Rais wetu ambaye anatamani kuleta mabadiliko ya haraka. Daima anasema maendeleo hayana chama, lakini bado amefungwa mikono na miguu na chama chake. Mpaka sasa ameshindwa kupammbana na ushabiki wa kupitiliza katika chama chake. Kama alivyosema kwa msisitizo kwamba hana mpango wa kuufuta Mwenge, tunaomba aseme wazi kwamba Mwenge huu ni wa Watanzania wote. Avunjilie mbali utamaduni wa Mwenge huu kukimbizwa na vijana wa CCM. Vijana wote, wenye vyama na wale wasiokuwa na vyama vya siasa wawe na uhuru wa kuukimbiza Mwenge wetu wa uhuru.
Hoja ya msingi hapa ni kwamba, siasa iwe na kiwango fulani cha ushabiki, lakini isitawaliwe na ushabiki.Kwa maana kwamba ushabiki usiwe juu ya fikra. Ushabiki usigeuze ukweli, ushabiki usiwafumbe watu macho kuona mambo mazuri na yenye kujenga ya upande mwingine. Ushabiki usilete ubaguzi na ushabiki usijenge utamaduni wa kukataa kusikiliza hoja! Kawaida hoja hujibiwa na hoja .
Majuma mawili yaliyopita nimekuwa nikijadili juu ya mpango wa kutaka kujenga bwawa la kuzalisha umeme kwenye mbuga za Selous. Kwa bahati mbaya, mjadala huu umepokelewa kisiasa na siasa za ushabiki! Kama nilivyosema hapo juu, ushabiki ukitawala siasa hakuna matokeo chanya. Badala ya kujadili hoja zinazotolewa, wale wanaonipinga wanatanguliza “Kupinga”. Kwamba tunapinga mradi wa kuzalisha umeme, kwamba tunapinga maendeleo. Kuna mtu alipiga simu na kufoka akisisitiza kwamba sisi tunaotoa hoja za kutounga mkono ujenzi wa bwawa hili, hatutaki treni ya umeme ya kutoka Dar hadi Mwanza, kwamba hatutaki viwanda na mengine mengi.
Mbaya zaidi wale wanaoiangalia hoja hii kisiasa na kutawaliwa na ushabiki, wanaenda mbali kwa kusema kwamba tunampinga Rais. Wanataka kutuchonganisha na Rais wetu. Hawa ni watu wabaya kabisa. Wangekuwa na nia njema, basi wangejibu hoja kwa hoja na wala si kujificha kwenye kivuli cha “ Mapenzi ya Rais”. Tunampenda Rais wetu alete maendeleo, tunampenda Rais wetu alijege taifa letu. Na tunaamini kwamba ili Rais wetu afanikiwe ni lazima kila Mtanzania atoe mchango wake. Na mwelekeo si kumwangalia Rais, au mapenzi ya Rais, bali kuiangalia Tanzania ya leo, kesho na vizazi vijavyo.
Tunaamini kuna vyanzo vingi vya umeme wa kuendesha treni na viwanda zaidi ya kutaka kuzima kitu kimoja ili kujenga kingine. Kuzima utalii wa Selous, kuharibu mazingira kwa kutaka kuleta maendeleo ya leo, bila kuangalia kesho na keshokutwa ni kukubali kutawaliwa na ushabiki wa kisiasa. Wanaouona ukweli huu, kukaa kimya kuogopa kuitwa wasiliti ni zaidi ya dhambi ya mauti.
Tujifunze kutoka kwenye historia. Tuangalie kule ambako ushabiki uliitawala siasa na kuona matokeo yake. Inawezekana matokeo chanya kwa muda mfupi, lakini si endelevu. Yanaota kama uyoga na kunyauka haraka. Hivyo wale wanaotaka maendeleo endelevu, wamekuwa wakijitahidi kuweka ushabiki pembeni na kuingalia hali halisi. Wengine wanafikia hatua ya kukubali kufanya kazi na wapinzani wao, ili wajenge kitu cha kudumu. Mnapolijenga taifa lenye watu zaidi ya milioni 50, taifa lenye makabila tofauti na imani tofauti, ni muhimu kujenga utamaduni wa kujadiliana, kuchukuliana na kuvumiliana. Tumejikuta Tanzania, hatuna uchaguzi zaidi ya kukubali kuishi pamoja.
Bahati nzuri katika makala zangu si wote wanapinga! Kuna msomaji wa makala zangu ambaye ameamua kuniandikia. Nimetoa jina lake, lakini ninanukuuu kila kitu alichoniandikia:
“Napenda kukuunga mkono katika hili suala la ujenzi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme la Stiegler’s Gorge. Pamoja na historia ndefu ya kulitumia eneo hili kuzalisha umeme lakini uhalisia wa kimazingira unatusuta kwa sasa. Mabadiliko ya Tabia Nchi (Climate Change) katika Ukanda wa Afrika Mashariki unaonesha kinaga ubaga kuwa shughuli za kibinadamu kama vile ujenzi wa makazi, kilimo, ufugaji na nyinginezo zimeleta athari kubwa katika utunzaji endelevu wa mazingira (sustainable environment protection/management). Mito, maziwa na hata mabwawa makubwa yamepungua kina cha maji. Tazama ziwa Manyara, Eyasi na hata Natron kwa upande wa mikoa ya Arusha na Manyara. Kule Mara, kuna athari kubwa katika mto Mara vile vile.
“Tumekuwa tunatumia tu bila kuangalia namna ya kuandeleza. Kama tunazungumzia Maendeleo Endelevu (Sustainabke Development) pia tuzungumzie Matumizi Endelevu (Sustainable Consumption). Vyanzo vya maji vimeharibika, hamna tena ile miti ya asili wala miti ya kupandwa ili kulinda vyanzo vya maji (water resources management). Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere katika hotuba yake kwa viongozi wa Serikali juu ya Umaskini na Uharibifu wa Mazingira alisema Taifa halina mpango wa kufidia misitu inayokwatwa kila siku kwa ajili ya nishati (mkaa),kilimo n.k, aliisauri kuwepo na utaratibu wa kupanda miti kila mwaka kwa kila wilaya, mkoa na hata Taifa. Lakini, kazi hii ilifanyika mara chache mwishoni mwa mwaka 1999 na mwanzoni mwa miaka ya 2000 bada ya hapo hatusikii tena hili suala. Na wazo hili lilipokelewa kwa mikono miwili na Makamu wa Rais, Hayati Dk Omari Ali Juma kabla ya kufariki, waliofuata hamna anayetilia mkazo suala la utunzanji mazingira kwa kuweka mkakati endelevu hususani kuwepo na utaratibu wa kusema katika Wilaya ya Maswa, kwa mfano; tutapanda miti kiasi kadhaa kwa mwaka huu, na iwe hivyo kwa mkoa na Taifa. Ila tumekuwa tunashuhudia matukio ya kustukiza tu na kutoza watu faini bila kuweka mkakati endelevu wa kutunza mazingira.
“Kwa hiyo, kama hatuna mkakati wa kutunza vyanzo vya maji, tutatumia pesa nyingi kujenga bwawa lakini halitakuwa endelevu kwa maana ya kuzalisha umeme uliokusudiwa. Lazima kuwepo na mkakati wa utunzaji wa mazingira unaoenda sambamba na utoaji wa Elimu kwa Jamii juu ya dhana ya kutunza mazingira. Sera na sheria za mazingira zimeshindwa kufanya kazi. Jamii haihusishwi vya kutosha katika kutunza mazingira na wawekezaji ndiyo wamekuwa wa kwanza katika uharibifu wa mazingira, iwe katika vyanzo vya maji, misitu.
Mwisho, Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere alisema uhabifu wa mazingira na umaskini ni ndugu na baba yao ni ujinga!
Kwa hiyo utafiti unaozungumzia katika makala yako ni muhimu sana ila vyuo vyetu vikuu vimekuwa vinakopi na kupesti tu wanapopewa kazi za kuangalia (Environmental Impact Assessment (EIA) mara nyingiine wataalamu hawafiki katika eneo husika ila wanapika data (taarifa)”.
Hoja ya msomaji wangu inajieleza yenyewe na hiki ndicho nimekuwa nikisisitiza kwenye makala zangu mbili juu ya ujenzi wa bwawa la umeme. Kusema kwamba haya ni maneno ya “adui” wa taifa au “adui” wa Rais ni kutotenda haki. Tunaendelea kusisitiza kwa nguvu zote kwamba hata kama uamuzi umepitishwa, maana huwezi kupingana na Rais wa nchi, basi utafiti ufanyike. Tujue kabisa ni athari gani zitafuata baada ya kujenga bwawa hili la umeme. Tuone juhudi za kupanda miti na kulinda mazingira yanayozunguka bwawa hili zikiendelea. Tuone juhudi za kulinda sehemu ya Selous inayobaki zikiendelea. Tuone juhudi za kulinda wanyama kama tembo na wengine wanaopatikana kwenye mbuga hii zikiendelea. Tusipende kutaka kujenga kitu kimoja kwa kuua kingine na tukataee kwa nguvu zetu zote siasa zetu kutawaliwa na ushabiki.
Padre Privatus Karugendo.
+255 754 633122
pkarugendo@yahoo.com

No comments:

Post a Comment