Ukiwauliza wazazi kitu gani wanafikiri kikisitizwa mapema zaidi kwa watoto kitawasaidia kufanikiwa, wengi watakwambia elimu.
Ni kwa kwa sababu hiyo, wazazi hasa wasomi wanaharakisha kuwapeleka shule watoto wenye umri mdogo.
Ninawafahamu watoto wengi wa miaka minne wanaosoma darasa la kwanza. Wazazi wao wanafanya hivyo, wakiamini mtoto akisoma mapema, maana yake uwezekano wa kufanikiwa maishani unakuwa mkubwa.
Shuleni pia, watoto hawa wanakutana na walimu wanaofanya kila linalowezekana kuhakikisha wanafaulishwa mitihani.
Mbali na mtoto kufundishwa mambo mengi yanayomzidi umri wake, kuna hili la walimu kuwapa watoto kazi nyingi wanazotakiwa kuzikamilisha baada ya muda wa masomo (home work).
Faida ya kazi za nyumbani
Kazi za nyumbani zina nafasi ya kutengeneza daraja kati ya mazingira ya shule na nyumbani. Kimsingi, mwalimu anatarajia kumfanya mzazi awajibike kutengeneza mazingira ya kitaaluma nyumbani.
Kufanya hivi kunamlazimisha mzazi kujenga tabia ya kufuatilia maendeleo ya mwanawe kimasomo, na hivyo kutilia mkazo kile ambacho mwalimu amekifundisha darasani.
Hoja nyingine ya watetezi wa kazi hizi, ni kumfundisha mtoto tabia ya kuwajibika.
Inaeleweka kwamba mtoto anaporudi nyumbani na kazi, akili yake inakuwa na kazi ya kuhakikisha wajibu aliopewa na mwalimu shuleni unakamilika.
Profesa Harris Cooper, wa Chuo Kikuu cha Duke amefanya tafiti nyingi kuhusiana na utamaduni huu. Anasema; “Kazi za nyumbani ni utaratibu mzuri wa kujifunza. Kuna faida kadhaa, lakini faida hizo zinategemea umri wa mtoto.”
Kwa watoto wa madarasa ya awali (yaani shule ya awali na msingi), anafikiri inatosha shughuli ya mtoto kujifunza iishie darasani.
Mwalimu akitumia muda wake vizuri darasani, hana sababu yoyote ya kumpa mtoto kazi za ziada, kwa sababu hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya wingi wa kazi za nyumbani na mafanikio ya mtoto kitaaluma.
Nikijitolea mfano mimi mwenyewe, sikumbuki ni lini niliwahi kukaa nyumbani nikifanya kazi za shule nikiwa nasoma shule ya msingi. Baada ya masomo, ratiba ya nyumbani ilikuwa ni kumsaidia mama kufanya kazi.
Baadaye nilipata muda wa kucheza na kwa kuwa nilitumia muda wa shule vizuri, hatimaye nilifanikiwa kitaaluma.
Tafiti tofauti
Etta Kralovec, ambaye ni profesa wa elimu katika Chuo Kikuu cha Arizona anasema; “Utafiti uko wazi kabisa kwamba saa mbili za kufanya kazi za shule baada ya muda wa shule, zinatosha kwa mtoto mkubwa (wa sekondari.) Lakini kwa mtoto mdogo (shule ya msingi), kazi za nyumbani hazina faida ya maana.”
Binafsi nimekuwa nikifuatilia kazi ambazo watoto wengi wa madarasa ya chini wanapewa kuzikamilisha nyumbani. Nyingi, kwa kadri ninavyoziona, hazina ulazima wowote zaidi ya kujaribu kumwaminisha mzazi kwamba kuna kitu kinafanyika shuleni.
Kwa mfano, kazi nyingi ni za kukariri kwenye vitabu, ambavyo mara nyingi havijapitiwa kwa makini na wataalam kujiridhisha ikiwa vinafaa kwa watoto wadogo.
Baadhi ya vitabu vina masimulizi yenye maudhui yasiyolingana na umri wala utamaduni wetu, lakini ndio vitabu ambavyo watoto wetu wanatumia muda mwingi kuhangaika navyo kukamilisha kazi za nyumbani.
Athari kwa ukuaji
Mtoto anayeanza shule, anahitaji kusaidiwa kupenda kujifunza na kuona shule ni mahali pazuri. Utamaduni huu wa kuwapa watoto kazi nyingi, hata hivyo, unawafanya watoto hawa waanze kuchoka shule.
Fikiria mtoto wa miaka mitatu anayehitaji kucheza, anajikuta kwenye mazingira ambayo kuna mtu anamlazimisha kujua kujumlisha na kutoa.
Ingawa ni kweli mtoto anaweza kujifunza kwa lazima, lakini kufanya hivyo kunaweza kumdumaza mtoto kwenye maeneo mengine muhimu ya ukuaji. Mfano mdogo, watoto wengi hujikuta kwenye migororo mikubwa na wazazi wao kwa sababu tu hawajafanya kazi za shule.
Badala ya kukaa na kuwafundisha watoto wao maadili, tunu za maisha na kuwakuza kiroho na hata kujenga mawasiliano ya karibu, wazazi wengi wanaishia kufokeana na watoto kwa sababu tu hawajakamilisha kazi.
Mara nyingi watoto hawafanyi kazi hizi si kwa sababu ni wavivu, jeuri au si wasikivu. La hasha! Mara nyingi sababu ni ukweli kwamba tumewaingiza kwenye mduara wa shinikizo la kitaaluma mapema zaidi kuliko umri wao.
Kujenga utegemezi
Fikiria mtoto ameshindwa kufanya kazi alizotakiwa kuzifanya kwa uzembe. Katika mazingira kama haya, mzazi anageuka kuwa afande anayehakikisha kazi zote zimefanyika hata kama mtoto mwenyewe kimsingi haoni maana ya kile anachotakiwa kukifanya.
Inapotokea mtoto hana uwezo wa kuzifanya, badala ya mzazi kubeba wajibu wa kukazia yale ambayo mtoto alijifunza shuleni, mzazi anaamua kuzifanya mwenyewe kwa niaba ya mtoto, ili mwalimu shuleni asione mtoto hana mtu wa kumsaidia anaporudi nyumbani.
Hapa tunatengeneza tatizo jingine la mtoto kujenga utegemezi kwa watu wazima na kumnyang’anya mtoto tabia ya kuwajibika kwa mambo yanayohusu.
Ingawa kumsaidia mtoto kukamilisha kazi zake inaweza kuonekana kama mchango chanya wa mzazi kwa mtoto, tabia hii inaweza kupanda mbegu ya kuwategemea watu wengine hata atakapokuwa mtu mzima.
Ushauri
Shughuli zisizo za kitaaluma moja kwa moja zina nafasi kubwa ya kumfundisha mtoto vizuri zaidi kuliko kazi za nyumbani.
Kwa mfano, kuwasomea na kuwasimulia watoto hadithi ni namna bora zaidi ya kuwafundisha watoto mambo wanayoyahitaji katika maisha yao ya kila siku. ada ya shughuli ya kujifunza shuleni, ni vyema nyumbani pawe sehemu ya kumfanya mtoto ashiriki shughuli nyingine akiwa na familia yake.
Pia, tuweke mazingira ya mtoto kutumia akili yake katika kuyachunguza mazingira yake kupitia michezo na kazi za mikono.
Shughuli hizi tunazoziona hazina maana, zina nafasi kubwa ya kukuza uwezo wa mtoto kukumbuka, kuzingatia, kufikiri kwa haraka, kukaa na wenzake na hata kuvumbua vipaji vyake ambavyo wakati mwingine hatuvigundui kwa sababu muda wote tunataka afanye hesabu, asome na aandike.
No comments:
Post a Comment