Sunday, October 15

Ajali yaua saba Manyara

Watu saba wamefariki dunia na wengine saba wamejeruhiwa baada ya kutokea ajali ya gari aina ya Noah kugongwa na lori la mizigo aina ya scania kwenye Kijiji cha Getasam Kata ya Masqaroda Wilayani Hanang' Mkoani Manyara. 
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Manyara, Lucas Ole Mukus amesema  ajali hiyo imehusisha watu watano waliokuwa wametoka kwenye harusi.
"Bwana na bibi harusi walijeruhiwa na wamelazwa kwenye hospitali ya Tumaini ya wilaya ya Hanang' na hali zao zinaendelea vizuri," amesema  Ole Mukus.
Akizungumza leo Oktoba 15, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Francis Massawe amesema  ajali hiyo ilitokea juzi saa mbili  kwenye barabara kuu ya Katesh-Babati. 
Kamanda Massawe amesema  ajali hiyo ilihusisha gari aina ya Noah lililogongwa na lori la mizigo aina ya scania la mizigo.
Amesema gari aina ya scania likiendeshwa na dereva aliyetambulika kwa jina la Hamza Hussein lililigonga  Noah lililokuwa likiendeshwa na Simba Daud (46) mkazi wa Endagaw Hanang' na kupinduka na kusababisha kifo cha dereva wa Noah, abiria sita na majeruhi saba. 
Amesema  chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa Noah kupinda kulia akiwa ameongozana na lori bila tahadhari na kusababisha ajali ila upelelezi  bado unaendelea. 
Amewataja  waliofariki dunia kwamba  ni dereva wa Noah Daud, Selina Hindo (35), Amina Shaha (50) wa Duru wilayani Babati na Hiiti Gwande (50) "Wengine ni Elizabeth Hilonga (25), John Timotheo (17) mkazi wa Babati na Abeid Wilson (14) mtoto wa dereva wa  Noah," amesema Kamanda Massawe. 
Amewataja  majeruhi kuwa ni Philipo Nade (21) Samwel Nade (21) Faustine Safari (40) na Lina Isack (29), Flora Baso (27) Nicodem Robert (45) na Halfan Idd (35).
 "Mara baada ya kutokea kwa ajali hiyo majeruhi wa ajali hiyo walipelekwa kwenye hospitali ya Tumaini ya wilaya ya Hanang' na wanaendelea vizuri hali zao," amesema kamanda Massawe. 
Hata hivyo, mkuu wa wilaya ya Hanang' Sarah Msafiri alisema hadi jana mchana majeruhi sita kati ya saba wa ajali hiyo waliokuwa wamelazwa hospitali ya Tumaini ya wilaya hiyo walisharuhusiwa kutoka hospitalini. 
"Mgonjwa mmoja ambaye ni mama aliyeumia mguu na mfupa wa paja, amepata rufaa ya kwenda hospitali ya rufaa ya Haydom iliyopo wilaya ya Mbulu," alisema Msafiri

No comments:

Post a Comment