Mwenyekiti huyo amesema sheria tatu zilizopitishwa hivi karibuni na bunge zinalenga kuongeza mapato ya serikali na si kubinafsisha kampuni za madini nchini.
“Kwa maoni yangu, uadilifu ni jambo muhimu Tanzania kama ilivyo kwingineko. Nina uzoefu wa zaidi ya miaka 20 ya kufanya kazi Tanzania, mabadiliko yaliyofanywa hayana madhara kwa wawekezaji,” alikaririwa Sinclair alipozungumza na The Minng Journal, jarida la nchiniMarekani linaloandika masuala ya madini.
Sinclair amefafanua kwamba kampuni yake inayomiliki asilimia 45 ya Mgodi wa Buckreef haijaathirika kwa namna yoyote na mabadiliko hayo na kwamba ni ukweli ulio wazi kwamba taifa lenye rasilimali lazima linufaike nazo.
Kwa kushirikiana na Shirika la Madini la Taifa (Stamico), Rex inauendesha mgodi huo uliopo Kata ya Lwamgasa mkoani Geita tangu mwaka 2011 lakini taarifa zinaonyesha haijaanza kuzalisha dhahabu.
Mabadiliko yaliyofanywa yameongeza umakini wa watendaji wa serikali hata kufanikisha kukamatwa kwa almasi na dhahabu ya mabilioni huku Kampuni ya Acacia ikipigwa faini kutokana na udanganyifu uliofanywa kwenye kodi kwa zaidi ya miongo miwili sasa.
Acacia imepigwa faini ya Dola 190 bilioni (zaidi ya Sh424 trilioni) huku wakia 70,000 za almasi zenye thamani ya Sh33 bilioni zikikamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na dhahabu wa Sh500 milioni ikikamatwa Bandari ya Dar es Salaam.
Licha ya pongezi za mwenyekiti huyo, Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anayeshughulikia nishati, Amadou Hott amesema Tanzania ipo katika njia sahihi kutaka kuwa na asilimia 16 ya hisa kwenye miradi ya madini na mafuta ili rasilimali hizo ziwanufaishe wananchi.
Ametoa kauli hiyo alipofanya mazungumzo ya kulinusuru Shirika la Umeme (Tanesco) na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango mwishoni mwa wiki mjini Dodoma.
Amesema nchi kadhaa duniani zinafanya hivyo ili pande zote zinufaike. “Jambo la msingi ni kuhakikisha makubaliano yanakuwa wazi, yenye usawa na haki. Ni muhimu wawekezaji wakakubaliana na utaratibu huo” alisema Hott.
Amesema benki yake itaipa Tanesco Dola 200 milioni za Marekani (zaidi ya Sh440 bilioni) kupunguza deni la zaidi ya Dola 370 milioni (740 bilioni) linalodaiwa na taasisi mbalimbali ili liweze kujiendesha kibiashara.
Mpaka mwaka 2019, Dk Mpango amesema misaada na mikopo ya masharti nafuu ya benki hiyo kwenye sekta ya nishati pekee itakuwa ni zaidi ya Dola 1.1 bilioni.
Licha ya kiasi hicho kwa Tanesco, waziri huyo alisema: “AfDB imeionesha nia ya kusaidia ujenzi wa mradi kufua umeme wa Stigler’s Gorge utakaozalisha megawati 2,100.”
No comments:
Post a Comment