Friday, September 22

Waziri ataka uwazi gharama za ujenzi

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi,

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Makame Mbarawa 
Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Makame Mbarawa amelitaka Baraza la Taifa la Ujenzi kuweka viwango vya gharama za ujenzi kama ilivyo kwa nchi nyingine.
Akifungua mkutano wa wadau wa sekta ya ujenzi wanaojadili kuboresha utendaji wa baraza hilo, Profesa Mbarawa amesema nchi nyingi viwango vya gharama za ujenzi viko wazi.
Amesema kwa Tanzania mtu akitaka kujenga nyumba hafahamu gharama zake kwa kuwa baraza hilo halijaweka viwango.
"Katika nchi zilizoendelea ukitaka kujenga nyumba au uwanja wa ndege kuna viwango vimewekwa katika kila mita za mraba," amesema.
Profesa Mbarawa amesema kila mtu akitaka kujenga nyumba, baraza linatakiwa kuweka wazi ni kiasi gani kitagharimu katika kila mita moja ya mraba.
Amesema viwango vikiwa wazi vitapunguza ubadhirifu kwa kuwa vitakuwa wazi.
Waziri amewataka wadau hao kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuimarisha sekta hiyo ambayo inakua kwa kasi.
Amesema mwaka 2016 sekta ya ujenzi ilichangia asilimia 14 katika pato la Ttaifa.
Profesa Mbarawa amesema Serikali itakuwa tayari kupokea mapendekezo yanayowezesha kuifanyia marekebisho sheria iliyoanzisha baraza hilo. Amelitaka baraza hilo kusimamia ubora wa vifaa vya ujenzi na kuwaelimisha wananchi. Mwenyekiti wa bodi ya baraza hilo, Profesa Mayunga Nkunya amesema wamejipanga kuboresha kazi.
Amesema kubomoka kwa majengo kumekuwa kukisababishwa na vifaa duni vya ujenzi.
Mwenyekiti wa bodi amesema wadau hao watajadili na kutoa mapendekezo serikalini ili kuboresha utendaji wa baraza hilo.

No comments:

Post a Comment