Tanzania ni moja ya mataifa ya mfano duniani, kutokana na kustawi kwa amani na utulivu.
Viongozi wa mataifa mbalimbali wamekuwa wakija kujifunza, nini siri ya Tanzania kudumisha amani na utulivu tangu taifa kupata uhuru.
Tanzania kuna makabila zaidi ya 120 ambayo yanaishi pamoja bila vurugu kama zilivyo nchi nyingine.
Haijawahi kutokea ukabila ukawa sifa ya kuchaguliwa viongozi wa ngazi mbalimbali katika taifa hili.
Licha ya dosari kadhaa katika chaguzi zetu, umoja na mshikamano wetu vimedumishwa katika ngazi mbalimbali kwenye jamii zetu.
Tofauti na mataifa mengine ambayo chaguzi husababisha machafuko makubwa, Tanzania tushukuru uchaguzi umekuwa ukipita na kutuacha salama.
Mazingira ya aina hii, hayakuja hivihivi bali tukubali kuna misingi bora iliyoachwa na waasisi wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Aman Karume.
Tanzania kwa miaka mingi, viongozi wamekuwa wakihubiri kuimarisha undugu bila kujali, dini, rangi, kabila wala mitazamo ya kisiasa.
Viongozi wetu wamekuwa wakieleza siasa za vyama ni majukwaa tu ya kuwasiliana na wananchi na si kitu ambacho kinaweza kufanya jamii moja kugombana na nyingine hadi kufikia kumwaga damu.
Lakini kadri siku zinavyoongezea kumeanza kuonekana nyufa katika jamii zetu, tofauti za kisiasa na mitazamo vimeanza kuonekana ni uadui na uasi.
Ufa huu unaongezeka kutokana na kauli za kutuhumiana hadharani na kuitana majina ambayo madhara yake ni makubwa katika siku za usoni.
Uelewa mdogo katika jamii, sasa umeanza kupokea vibaya kauli zetu na kuna Watanzania ambao wanaonekana kama maadui wa taifa.
Mazingira haya ya kutuhumiana ndiyo yamekuwa yakivuruga amani katika mataifa mengi barani Afrika.
Naamini mazingira ya aina hii, ndio ambayo yamemsukuma Rais Mstaafu Jakaya Kikwete kutoa wito kwa vyama tawala barani Afrika kutowachukulia viongozi wa upinzani kuwa maadui.
Rais Kikwete alitoa tamko hilo wakati akichangia mada ya Utawala Bora na Utawala wa Sheria iliyowasilishwa na Profesa Barney Pityana, ambaye ni Makamu Mkuu Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Afrika Kusini kwenye Kongamano la Uongozi barani Afrika.
Kauli hii imezua mjadala mkubwa hapa nchini, hadi kufikia hatua Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Humphrey Polepole kueleza kuwa kauli hiyo haikulenga Tanzania bali ililenga mataifa mengine kwani Tanzania ni ni moja ya nchi vinara wa demokrasia Afrika.
Si vyema kuendelea mjadala huu kwa kutazama ulilenga wapi, lakini itoshe kumpongeza Kikwete kwa kutoa kauli hii, ambayo naamini mataifa mengi barani Afrika yataifanyia kazi.
Katika siku za karibuni, kumeanza kuonekana matukio ambayo yameanza kuwagawa Watanzania kwa misingi ya itikadi zao jambo ambalo ni hatari kwa mustakabali wa taifa letu.
Kukosekana uvumilivu wa kisiasa baina ya viongozi wetu, hali ambayo imesababisha kuongezeka kauli ambazo si nzuri baina ya viongozi wetu wa kisiasa na kamatakamata ya viongozi wa kisiasa wakiwamo wabunge.
Uhasama huu katika jamii, umefikia hatua ya kiongozi wa upinzani mbunge wa jimbo la Singida Mashariki na Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika, Tundu Lissu kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 28 na baadhi ya watu kushabikia.
Nyufa hizi zimeanza kutumiwa vibaya na wale ambao hawataki, kuiona Tanzania inasonga mbele katika kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Ukifuatilia katika mitandao ya kijamii, utabaini tukio hili dhidi ya Lissu limeonyesha nyufa katika jamii na kuanza kujengeana uhasama ambao unaweza kuleta matatizo baadaye.
Tumuombe Mungu, wale ambao walijaribu kutaka kulivuruga taifa kupitia tukio la kumshambulia Lissu washindwe na walegee na vyombo vya dola viwakamate wote.
Lakini pia tukio hili linapaswa kutuunganisha Watanzania badala ya kutugawa, kwani isionekane kuna ambao wanafurahia kwani hawajui kesho nani atashambuliwa.
Kundi la watu hawa wachache, wakiachwa watatumia mwanya huo kuchonganisha Serikali na wananchi jambo ambalo si sahihi.
Hivyo itoshe kutoa wito kwa wanasiasa wote, vyombo vya dola, viongozi wa kijamii na viongozi wa dini kukemea wale wanaotaka kulivuruga taifa letu kwa kujua ama kutojua.
Watu hawa wachache ni vyema kutambua kuwa katika nchi za kidemokrasia, hakuna ushindi wa kweli unaopatikana kwa risasi ama mabavu bali ushindi hupatikana kwa hoja na maridhiano.
Mungu ibariki Tanzania. Mussa juma ni mwandishi mwandamizi wa gazeti la mwananchi anapatikana 0754296503
No comments:
Post a Comment