Wednesday, September 13

Wabunge wanawake wabebeshwa zigo kodi za ‘pedi’


Spika wa Bunge, Job Ndugai amewataka wabunge wanawake kusimamia kuondolewa kodi katika taulo za usafi za kike ‘pedi’
Amesema kodi hiyo imekuwa kero, hivyo amemtaka mwenyekiti wa wabunge wanawake, Magreth Sitta kubeba jukumu hilo.
Spika ametoa kauli hiyo kutokana na majibu ya Serikali kutoeleza moja kwa moja ni lini itaondoa kodi kwa taulo hizo.
Akijibu swali bungeni, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamisi Kigwangalla amesema  maombi ya kuondoa kodi hiyo yamewahi kuwasilishwa na watumiaji na wauzaji wa bidhaa hiyo.
Dk Kigwangalla alikuwa akijibu swali la msingi la mbunge wa Viti Maalumu, Stella Alex aliyetaka Serikali ihakikishe inaondoa kodi kwenye taulo hizo.
Naibu waziri amesema uamuzi wa suala hilo umechelewa baada ya kubaini kuwa bidhaa hiyo haikuwa miongoni mwa orodha ya vifaa vya matibabu (vifaa tiba) ambavyo huondolewa kodi.
Hata hivyo, amesema taulo hizo zimeondolewa ushuru wa forodha lakini aina zingine za kodi zinalipwa kama bidhaa zingine.
Amesema Wizara ya Afya imeshaandika barua kwa Wizara ya Fedha na Mipango kuona namna ya kuondoa kodi katika bidhaa hiyo.
“Majadiliano yanaendelea kuwezesha bidhaa hii iunganishwe katika orodha ya vifaa tiba ili viweze kupata msamaha wa kodi na vifaa vingine vya tiba,” amesema.
Naibu waziri amesema kuondolewa kwa kodi kutawezesha kupunguza gharama za taulo hizo, hivyo kuuzwa kwa bei inayokubalika na wengi kumudu kuzinunua.

No comments:

Post a Comment