Baadhi ya wafuasi wa CUF, viongozi wa chama hicho waliishambulia Tume kwamba ilikuwa na njama kati yake na Spika wa Bunge katika kulishughulikia suala la wabunge hao CUF waliokuwa wamefukuzwa uanachama na upande wa Profesa Lipumba na hatimaye kupelekea uteuzi wa wabunge wapya kujaza nafasi zao.
Katika ufafanuzi wake, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Kailima Ramadhani anasema, “Kwa kweli nadhani tatizo hapa ni ukosefu wa uelewa wa watu kwa upande mmoja, lakini pia kuna upotoshaji wa makusudi.”
Anasema NEC ilizingatia matakwa yote ya kisheria yanayohusiana na viti maalumu vya wabunge wanawake kwa kuzingatia sheria zinazoiongoza Tume zinatambua uchaguzi wa aina mbili, ule wa kupiga kura na ule wa wabunge wa kuteuliwa.
Kailima anasema baada ya NEC kupokea barua kutoka kwa Spika kwamba kuna nafasi za wazi, hatua inayofuata inatekelezwa kwa mujibu wa Ibara ya 74 (4) ya Katiba ambayo inaelekeza kwamba orodha iliyowasilishwa Tume awali na chama husika cha siasa wakati wa uchaguzi mkuu, itumike kujaza nafasi iliyopo wazi au nafasi zilizo wazi.
Hata hivyo, ufafanuzi wa ujazaji huo wa nafasi unafanyika baada ya kushauriana na chama husika cha siasa.
Kailima anasema kutokana na matakwa ya sheria kwa kawaida Tume inaviandikia barua vyama vya siasa kuwauliza ni yupi miongoni mwa wale walioko kwenye orodha anafaa kuteuliwa kujaza nafasi iliyoachwa wazi.
“Vyama hivyo vinatakiwa kujibu barua ya Tume kwa kujaza Fomu namba 8E, na baada ya kuipokea hiyo fomu Tume huendelea na taratibu nyingine za kiutawala kujiridhisha kwamba muhusika au wahusika wana sifa stahiki na kupitisha jina au majina yao,” anasema.
Kailima anafafanua kuwa baada ya kukamilisha utaratibu wa kupitia na kujiridhisha juu ya vigezo vya jina la mwanachama anayependekezwa, wanamwandikia Spika wa Bunge kumfahamisha kuwa wameshafanya uteuzi, barua hiyo pia inatumwa kwa chama cha siasa kwa kunukuu barua yao ya maombi kuwafahamisha kwamba maombi yao yamepokelewa na yameshughulikiwa.
Kwa suala mahususi la CUF, Kailima anasema, “Jioni ya tarehe 26 mwenzi Julai tulipokea barua kutoka kwa Spika kumfahamisha Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi kwamba kuna viti maalumu viko wazi Bungeni vya CUF. Siku iliyofuatia Julai 27 nilimwandikia Katibu mkuu wa CUF. Kwa taratibu za Tume barua ikiandikwa na mwenyekiti wa Tume inatumwa kwa Mwenyekiti wa chama cha siasa na nikiiandika mimi (Mkurugenzi wa Uchaguzi) naituma kwa Katibu mkuu wa chama husika.”
Anasema wakati wa kutuma barua, NEC imekuwa ikitumia anuani zilizotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa kwa sababu Tume haishughuliki na mambo ya usajili wa vyama na badala yake inapokea taarifa zote kuhusu majina ya vyama, majina ya viongozi, namba za usajili na anuani.
Hata hivyo, Mkurugenzi huyo anasema kuna vyama vina anuani zaidi ya moja kama CCM ambacho kina anuani ya Dodoma na Dar es Salaam na CUF ambacho kina anuani ya Dar es Salaam na Zanzibar.
Kailima anasema katika suala la CUF, utaratibu barua kwa chama ilitumwa kwa anuani ya Dar es Salaam (siyo Zanzibar) kwa kuwa barua iliyotumwa Tume ilitoka Dar es Salaam.
Kuhusu madai kwamba majina ya wabunge walioteuliwa hayakuwa kwenye orodha iliyotumwa awali na CUF, Kailima alisema matamshi au tuhuma kama hizo ni mfano kwamba kuna wanasiasa ambao walijipanga kupotosha umma kwa makusudi kwa sababu za kisiasa wanazozijua wenyewe.
“Inashangaza kwa sababu Katibu Mkuu wa CUF, Seif Sharif Hamad ambaye anadai kwamba majina ya wateule hayakuwa kwenye orodha, yeye ndiye aliyesaini karatasi yenye orodha hiyo ambayo iliwasilishwa hapa Tume mwaka 2015,” anasema.
Akifafanua juu ya madai kwamba ni kwa nini Tume ililishughulikia suala la CUF kwa haraka, Kailima amesema sheria ambazo zinaisimamia Tume kwenye mchakato wa uteuzi wa wabunge wa viti maalumu hazijaweka masharti ya muda kwenye uteuzi.
Kailima anaongeza kuwa hakuna kipengele katika sheria ambacho kinaiagiza au kuielekeza Tume kupokea maelekezo kutoka kwa mtu au taasisi yoyote na kwa hiyo, tuhuma kwamba Tume ilifanya maamuzi kwa shinikizo kutoka kwa Spika wa Bunge si za kweli.
“Tume haijawahi, na haitadiriki kamwe kufanya kikao na Spika wa Bunge kwa lengo la kupokea maelekezo yake juu ya utekelezaji wa majukumu ya Tume. Kwa mujibu wa Katiba, sheria, kanuni na miongozo, hatuna utaratibu kama huo.
Hata hivyo, Kailima anasema Tume inashirikiana na Serikali kwenye masuala yanayohusu na uendeshaji wa shughuli zake kwa maana ya bajeti na ulinzi, haswa wakati wa chaguzi mbalimbali na shughuli kama za uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.
“Tumekua tukifanya kazi kwa ukaribu na vyama vya siasa, ni wadau wetu muhimu na tunawajibika kuwashirikisha katika shughuli zetu mbalimbali kama vile uandikishwaji wa wapiga kura na uchaguzi, lakini hii haimaanishi kwamba wanaweza kuingilia au kutushawishi katika maamuzi ambayo tunatakiwa kuyafanya kwa uhuru,” alifafanua Kailima.
Mwandishi wa makala haya ni Afisa Habari wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
No comments:
Post a Comment