Pia, nilifafanua kwa ufupi aina na sifa za viongozi wanaotakiwa na chama, hasa katika uchaguzi unaoendelea, ambayo watatakiwa kuyasukuma mageuzi hayo. Leo katika sehemu ya mwisho ya makala haya tutaendelea kutazama msingi wa mageuzi haya kusonga mbele na kuwa ni mwiko kurudi nyuma.
Kipindi hiki tunapofanya mageuzi haya makubwa, napenda ifahamike kwamba wako baadhi yetu ambao watashindwa kwenda na mwendokasi wa mageuzi haya makubwa.
Baadhi ya wanaoshindwa kwenda na mwendokasi wa mageuzi makubwa ya CCM ni wale ambao walizoea kuishi kwa mazoea, kula visivyo vyao, kudhulumu haki za wananchi hasa wanyonge, walizoea kujimilikisha mali za CCM na kuzifuja watakavyo na walizoea kuwa miungu watu na kuwadharau wanachama.
Katika historia ya chama chetu, watu hawa wamekuwapo katika awamu zote, na ni mapambano kuwaondoa. Wanachama wanawajua, dhamira njema ya CCM mpya inawajua na hakika uongozi wa CCM na vikao vya chama vitahakikisha watu hawa wenye inda hawapati uongozi katika chama chetu.
Watu waovu wana mitandao yao ya uovu, tuwakatae. Chama chetu kimekuwa na desturi nzuri ya kuwakataa, kipindi hiki tutawakataa tena na kwa sauti kuu.
Mitandao imedhoofisha sana chama chetu, mitandao ya watu wabinafsi na wanaotaka kukitumia chama chetu kama kitega uchumi, mitandao ya kidhalimu haina nafasi kwa CCM.
Wakati mwingine hata watu ambao wamepata kuhudumu katika nyadhifa za uongozi wanahusika kuhujumu chama na nchi yetu. Wanatengeneza mitandao na kushirikia na madhalimu, tunawajua, hata utu una kikomo, hatutawaruhusu kuvuruga chama chetu.
Shime wanachama msikubali hata kidogo madhalimu wa kisiasa wakajaribu tena kuteka chama chetu, walishindwa, wameshindwa na wataendelea kushindwa.
Rai yangu hapa, watu wabaya huwa hawagombani, masilahi yao ya kidhalimu ni ya kudumu, wanaweza kuonekana hawako pamoja lakini wanaunganishwa na masilahi yao ya kudumu ya kidhalimu. Hata kwenye chama chetu walikuwapo, wameondoka, wamebaki, kazi yetu ni kuwadhibiti ipasavyo. Wameanza kuzungumza, tuwe macho kulinda misingi ya chama chetu.
Kila mwana CCM asimame kidete, akisemee chama, aisemee Serikali ya Chama Cha Mapinduzi. Ni wajibu wetu kuujuza umma wa wananchi nini Serikali inafanya na kwa nini.
Tunaupinga udhalimu katika chama chetu na tunaupinga udhalimu katika Serikali. Si kazi rahisi lakini tutashinda kwa sababu dhamira yetu ni njema na inasimamia masilahi mapana ya Taifa la Tanzania na watu wake.
Hata mabwana wakubwa wa dunia tumewaonyesha kwa vitendo kwamba tunamaanisha tunaposema tumechoka kuonewa, tumechoka kuibiwa kwa makusudi au kwa kuhadaiwa.
Nchi yetu ni ya kipekee sana na Mungu ametubariki na kila aina ya utajiri wa asili na watu wenye mshikamano.
Kijiografia nchi yetu iko katika eneo la kimkakati katika uso wa dunia. Katika bara la Afrika ni nchi mbili tu ndio zinatengeneza nyonga ya bara la Afrika nazo ni Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Hizi ndizo nchi pekee ambazo zinalikata bara la Afrika katikati na nchi ambazo zina mipaka ya bahari kuu zinazozunguka bara la Afrika kwa maana ya Bahari ya Hindi upande wa Mashariki inayopakana na Tanzania na Bahari ya Atlantiki upande wa Magharibi inayopakana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Ukizungumzia nguvu za siasa za kidunia, Majabali (Mataifa makubwa) ya kidunia na hasa yanayoongozwa na mrengo wa siasa za kiliberali na yenye uchumi uliononeshwa na matunda za udhalimu wa kibepari, utagundua wanatamani sana nchi hizi mbili zisitawalike.
Majabali haya yanatamani nchi hizi zisitawalike ili wapate nafasi ya kudhibiti eneo hili la kimkakati. Lakini, zaidi ya yote ifahamike kwamba katika eneo hili ndiko hazina ya rasilimali madini ya dunia iliko, kwa uchache na kwa kutaja, hapa yako madini yenye thamani ambayo hata duniani hakuna, ndio maana hata Tanzanite ikapewa jina hilo.
Ili majabali wawe na uhuru wa kuchukua hapa watakacho lazima hapa pasiwe na mwenyewe, watapandikiza chuki kwa makundi, watajaribu kutuvuruga kwa tofauti za kiimani na watajaribu pia kupitia vyama vya siasa.
Majabali ya dunia yamefanikiwa kuiangusha Congo au niseme yamefanikiwa kuifanya Congo isitawalike na wamepafanya pawe pahala ambapo wanaingia na kutoka na chochote bila kuulizwa maswali wala kulazimika kutoa majibu.
Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli amebadilisha utamaduni mbaya na desturi zisizofaa.
Amewakatia mirija madhalimu wakubwa na wadogo walioko ndani ya nchi na walioko nje ya nchi.
Imewauma sana sana, na wale walioko ndani wanatafuta kila njia ya kumhujumu asifanikiwe. Uzuri wanajulikana, ni wanaume wavaao baibui, baadhi yao ni watoto wa maskini na wamenufaika kwa fedha za maskini ila wamechagua maisha ya kufuru na ufedhuli, kwao vikao hukutania Dubai. Tunawajua.
Wako wachache katika chama chetu cha CCM, wana CCM na vikao vyake tusaidieni kuwakataa na pale wanapotumia hila kujipenyeza wafichueni.
Hakuna chama makini kama CCM, ndiyo chama ambacho kwa imani yake kinaamini katika ujamaa na kujitegemea, ndiyo chama pekee ambacho kinaamini binadamu wote ni sawa na ndio pekee ambacho kwa imani kinaamini utu wa binadamu unastahili kuheshimiwa.
Kule nje hakuna vyama, kuna vikundi maslahi, ni kama bidhaa sokoni, akifika mwenye bei anachukua bidhaa, na ninyi ushahidi mmeuona mwaka 2015.
Nakomea hapa, kwa kuwa ndoto ya kujenga uchumi imara na madhubuti ambayo Mwalimu Nyerere alikuwa nayo na hakuishi kuiona imeanza kudhihirika katika awamu ya Tano.
Ombi langu kwenu, hivi ni vita vya mwili na roho, ni vita ya haki dhidi ya udhalimu, vita ya mwili tunaimudu na tutaishinda hakika, tusaidieni maombi maana vita ya roho yapaswa ipiganwe na wengi wema na waishio maisha ya kujikana nafsi na wenye hofu ya Mungu.
Humphrey Polepole ni Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwenye dhamana ya Itikadi na Uenezi
No comments:
Post a Comment