Mnyama huyo ambaye husababisha ugonjwa wa kichaa cha mbwa kutokana na virusi kutoka kwa wanyama jamii yake wakiwemo paka, mbweha, fisi na wengineo, humwingia binadamu kwa kumuuma na mate yenye virusi ambavyo huingia katika eneo lenye jeraha.
Katika taarifa yake ya maadhimisho ya Siku ya Kichaa cha Mbwa kwa vyombo vya habari leo Jumatano, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema takwimu hizo hazijumuishi vifo vinavyotokea nyumbani na waathirika ambao hawakufika katika vituo vya kutolea huduma za afya.
“Tatizo hili linaweza kuwa kubwa kuliko tunavyofikiri. Utafiti uliofanyika mwaka 2002 ulibainisha kuwepo na uwezekano wa kuwepo takriban vifo 1,499 kwa mwaka nchini kutokana na ugonjwa wa kichaa cha mbwa,” amesema.
Ummy amesema tafiti pia zimeonyesha waathirika wakuu wa ugonjwa huo ni watoto chini ya miaka 15 kwa sababu wao ndio wanaokuwa karibu na mbwa muda mwingi, pia hupenda kucheza/kuchokoza mbwa wasiowafahamu njiani.
Amesema katika juhudi za kudhibiti ugonjwa huo, Tanzania ilipata ufadhili wa Bill na Melinda Gates na kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) na kuwa moja ya nchi zilizochaguliwa kutekeleza mradi wa majaribio wa kutokomeza kichaa cha mbwa kati ya mwaka 2009-2016, nchi nyingine zikiwa ni Ufilipino na Afrika ya Kusini.
Fanya haya ukiumwa na mbwa
Endapo mtu ameumwa na mbwa, hatua ya kwanza muhimu ni kuosha jeraha kwa dakika 10 au zaidi kwa maji mengi yanayotiririka na sabuni. Kidonda kisifungwe. Kisha nenda haraka kituo cha kutolea huduma za afya ili kupata chanjo ya kichaa cha mbwa.
Madhara ya kichaa cha mbwa
Vimelea vya kichaa cha mbwa vinapoingia katika jeraha hushambulia neva za fahamu kutoka katika eneo la jeraha, kuelekea katika uti wa mgongo na hatimaye kuathiri ubongo.
Dalili huanza kuonekana baada ya kuathirika kwa mfumo wa kati wa fahamu na baadaye ubongo, ambazo ni pamoja na kuwashwa sehemu ya jeraha, homa, kuumwa kichwa, maumivu ya mwili, kuogopa maji na mwanga, kutokwa mate mengi mfululizo, kuweweseka, kupooza na hatimaye kupoteza maisha.
No comments:
Post a Comment