Saturday, September 23

Mungu aliumba watu wanaojulikana, hawa wasiojulikana wametoka wapi?


Ndiyo ukweli wenyewe, usiokuwa na chembe yoyote ya shaka ulivyo. Kwamba, Mwenyezi Mungu kwa huruma, mapenzi, utashi na mamlaka aliyonayo aliumba watu. Watu ambao kwa mujibu wa maandiko, Mungu aliwaumba kwa mfano wake mwenyewe, kwa vyovyote vile ni watu wanaojulika.
Sasa kuna wimbi la watu ‘wasiojulikana’. Pengine swali la kujiuliza ni je, hawa waliumbwa na nani?
Haipingiki na ndivyo ilivyo. Kwa sasa Tanzania imekuwa ni nchi ya kwanza tangu kuumbwa kuwamo watu wanaodaiwa hawajulikani.
Hii ni kwa mujibu wa taarifa za mara kwa mara, zinazodai kwamba wanaotenda uhalifu fulani, unyama fulani, ujambazi fulani ni watu wasiojulikana.
Watu ambao Serikali pamoja na dola yake, mara zote wamekuwa wakipata si kuwatambua tu, bali hata kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria kwa matukio wanayoyafanya kila uchao.
Watu ambao kwa kiwango kikubwa wamekuwa wakiteteresha na kuififisha amani iliyokuwapo kwa miaka mingi.
Tanzania sasa inaelekea kuwa si kisiwa tena cha amani kama ilivyojulikana hapo awali; sifa yake inaanza kumong’onyolewa kwa maana ya ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu, jaribu kuchunguza na kutafiti utajua tu!
Na wala si kimbilio tena, la wenye kuitafuta amani waliyoikosa kule walikotokea; kama ilivyodhaniwa na mataifa mbalimbali huko nyuma. Hii ni kutokana na kuwapo kwa watu ‘wasiojulikana’.
Hakika hawa watu ‘Wasiojulikana’ idadi, ni nani na mahali walipo, wametuathiri kwa kiwango kikubwa na kupausha sifa ya Taifa lililokuwa mfano wa kuigwa na wengine.
Kama kiini macho hivi, watu hawa ‘wasiojulikana’ hivi sasa wamejipatia umaarufu mkubwa kuzidi hata watu wengi maarufu.
Ajabu yake, watu hawa wamepoka na kujitwalia umaarufu, eti wao sasa wanacho kibali walichokipata kusikojulikana cha kuteka, kuua, kuiba, kufungia kwenye viroba, kuteketeza na kufanya uhalifu wote kwa jinsi wanavyojisikia. Kisha hutoweka bila kujulikana bila Serikali yenye mkono mrefu wala vyombo vyake vya dola kuwaona na kuwatia nguvuni.
Wanafanya lolote wanalojisikia kwa wakati wowote, kana kwamba Serikali na dola yake imesafiri kwenda kusikojulikana. Hili ni la ajabu kwelikweli.
Mpaka ninavyoandika makala haya, kijana Mtanzania, Ben Saanane hajulikani alipo na wala hakuna tetesi tu za kujua ikiwa yu hai au la, hakuna ajuaye asilani. Liwe Jeshi la Polisi, Serikali, ndugu, jamaa na hata marafiki; wote hawajui wala kuwa na tetesi za mahali alipo.
Licha ya ndugu zake, wananchi pamoja na wabunge kupaza sauti zao wakitaka dola ichukue hatua kuhakikisha anapatikana akiwa hai au akiwa amekufa, mara zote jitihada hizo zimekuwa ni za bure.
Hata polisi wameshindwa kutoa jibu mujarabu, la wapi alipo au inapodhaniwa aweza kuwa. Imani kubwa ni kwamba, watu ‘wasiojulikana’ peke yao ndiyo pekee wanaoweza kufahamu mpaka sasa ni wapi alipo kijana huyu.
Hilo ni tukio mojawapo lililofanywa na watu ‘wasiojulikana’, linalowashangaza na kuwastaajabisha mamilioni ya wananchi na watu wengine kutoka nchi majirani zetu, wasioamini kama kweli jeshi limeshindwa kufanya kazi yake kikamilifu.
Lakini yapo matukio mengine mbali na hili la Saanane, ambalo sasa limegeuka na kuwa sawa na kutafuta upepo; ambayo hayajapatiwa ufumbuzi wa kina na yamefanywa na watu hao wasiojulikana na Serikali imeshindwa kuwakamata na kuwaleta mbele ya mkono wa sheria.
Miongoni mwa hayo ni tukio la miaka michache iliyopita linalomhusu, Mhariri wa New habari 2006, Absalom Kibanda ambaye alipigwa na kuteswa mateso makali na watu wasiojulikana.
Na mpaka leo, hao watu ‘wasiojulikana’ hawajaweza kupatikana kujibu tuhuma za matendo waliyoyafanya. Hata kama wasingiziwa basi wajitetea kwa tuhuma zinazowakabili.
Kabla ya tukio lililompata Kibanda, kulikuwa na jingine la kumtekaji Dk Steven Ulimboka, Kiongozi wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT). Huyu bada ya kutekwa na kuteswa kadri watesaji walivyotaka alitupwa nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam kwenye eneo la pori la Mabwepande ambako aliokotwa na wasamaria akipigania roho yake.
Hili ni miongoni mwa matukio yenye kuleta simanzi na majonzi makubwa, yanapokumbukwa na kusimuliwa kama hivi.
Tukio la karibuni, nalo kama yalivyo mengine yaliyo na sura ya sintofahamu ni lile la kummiminia mvua ya risasi mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu wakati akitokea kwenye majukumu yake ya kibunge mkoani Dodoma. Alikuwa akirejea kwa mapumziko ya mchana katika eneo la makazi ambalo ni maalumu kwa ajili ya wanasiasa, wakiwamo viongozi wa Serikali na Bunge.
Tofauti kidogo na matukio mengine, hili lilifanywa mchana kweupe, naamini lilishuhudiwa na watu lukuki. Ila kwa woga waliopata watu wengi, hakuna aliyejitokeza kusimulia, labda mpaka baadaye sana.
Inasemekana Lissu alipigwa risasi zaidi ya 28 na kati yake zilimvunja mguu wa kushoto zaidi ya mara tano.
Risasi hizo hazikuishia kumvunja mguu huo tu, ila zilifululiza na kumjeruhi tumboni na kwenye bega, zikimsababishia maumivu makali na matatizo makubwa.
Kutokana na majeraha hayo, kurejea katika hali yake ya awali kunategemea kudra na majaliwa ya Mwenyezi Mungu na juhudi kubwa na madaktari wanaomhudumia.
Bado taarifa za Jeshi la Polisi zinadai kuwa wanaendelea kuwasaka watu wasiojulikana waliomshambulia na kuhakikisha wanawatia nguvuni haraka iwezekanavyo.
Hivi sasa, watu hao wasiojulikana wamezusha tafrani miongoni mwa jamii, kwenye miji na majiji kila mmoja akiwa hamuamini anayeongea naye pasipo kumfahamu kiundani.
Utamaduni ambao kwa Taifa letu umekuwa ni mgeni na haukuwahi kushuhudiwa kwa siku zilizopita; na hasa kutokana na umaarufu iliojijenga nchi yetu, ikijulikana ni kisiwa cha amani atakaye na aje. Ila kwa sasa hali haiko hivyo wasiwasi umetanda kila kona.
Kwa muktadha huo, ndiyo maana nikaanza na kichwa cha habari kama kilivyojinadi hapo juu, nikitaka kila mtu kuona tatizo na kuanza kubadili hali hii.
Swali: Mungu aliwaumba watu kwa mapenzi mema sana na wakawa wanaojulikana.....hawa ‘wasiojulikana’ ambao kila mara jeshi linahaha na kuhangaika kuwatafuta, na mara zote hizo wakiishia kutowapata na kushindwa kuwaleta mbele ya sheria; waliumbwa/wameumbwa na nani?
‘Wasiojuliakana’, wanawezaje kuishi kwenye nchi na kujichanganya na watu wanaojulikana, pasipo kushtukiwa au kutambuliwa na watu wanaojulikana hata wafanikiwe kila mara kufanya unyama na uhalifu wote huo?
Wanathubutuje kuuingilia uhuru na maisha kiujumla ya wanaojulikana, bila kujulikana na au kushakiwa kwa wakati wote huo?
Kila mmoja ajiulize tena, hivi kweli hawa ni watu wasiojulikana au ni watu wanaojulikana isipokuwa tu wameamua kujibadilisha na kuwa watu wasiojulikana?
Je, katika mafunzo askari wetu na kwa muda wanaosomea huko vyuoni, ina maana hawafundishwi kuwabaini na kuwatambua watu wasiojulikana na kuwakamata?
Kama wao wameshindwa kuwabaini na kuwakamata, nani sasa anayeweza kuwabaini na kuwakamata watu wasiojulikana?
Kama yote haya yamekosa majibu. Naungana na wananchi wenye nia njema, wanaotoa ushauri na maoni kwa jeshi letu la polisi, kama lina nia ya kuwajua na kuwakamata watu wasiojulikana liombe msaada kwa vikosi vyenye wataalamu kutoka nje ya nchi; kwa lengo la kusaidia kuwabaini na kuwakamata ili hatimaye wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria.
Nchi imepata kigugumizi cha ukubwani. Watu hawawezi tena kutoa mawazo na maoni yao kwa Serikali, kwa mujibu wa Katiba, inayompa kila mtu uhuru na haki ya kutoa maoni yake bila kupuuzwa.
Hofu imetanda, wakiwaza na kuhofia kuchukuliwa na kusombwa na watu wasiojulikana kwenda huko kusikojulikana.
Maana tulipofikia, hakuna anayejua watu wasiojulikana wanataka nini na wanachukia nini. Tukishindwa yote hayo, tutamshtakia Mungu.
0713/0765 937 378.
amwambapa7@gmail.com

No comments:

Post a Comment