Tuesday, September 5

Kampuni zamwagia klabu Sh3.7b


“Tumeamua kuidhamini Mbao FC tukiamini kuwa itafanya vizuri zaidi katika ligi na Ifahamike  kampuni yetu imekuwa na idadi kubwa ya wateja Kanda ya Ziwa inapotoka Mbao hivyo kupitia udhamini huu nadhani tutazidi kujiweka karibu na wateja wetu.” Kulwa Bundala- Ofisa Masoko GF Trucks & Equipments. 
Dar es Salaam. ‘Chema chajiuza…’ ndiyo hali inayoonekana kwa sasa kwa katika Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya klabu nane kuvutia udhamini wa kampuni 13 wenye thamani ya Sh 3.7 bilioni.
 Tofauti na misimu iliyopita ambayo kampuni tano tu ndizo zilikuwa zinadhamini timu za Ligi Kuu kwa kuwekeza kiasi kisichozidi Sh2 bilioni, msimu huu kuna ongezeko la kampuni nane ambazo zimemwaga kiasi hicho cha Sh3.7 bilioni  na kuvunja rekodi ya tangu kuanzishwa kwa ligi hiyo miaka 50 iliyopita.
Fedha hizo za udhamini ni tofauti na udhamini wa jumla wa ligi unaotolewa na kampuni ya mawasiliano ya Vodacom sambamba na ule wa haki za maonyesho ya televisheni wa kampuni ya Azam Media.
Katika kundi hilo la timu nane zilizovutia idadi kubwa ya kampuni kuzidhamini, Singida United inaongoza ikiwa chini ya udhamini wa kampuni sita tofauti na kuingizia  klabu hiyo Sh630 milioni.
Singida United iliyopanda daraja msimu huu, inapata Sh250 milioni kutoka kampuni ya utengenezaji na usambazaji wa mbolea ya Yara na pia inapata kiasi kama hicho kutoka kampuni ya SportPesa.
Kampuni nyingine nne ambazo zimeimwagia fedha Singida United ni Oryx Energy walioipa Sh100 milioni, NMB (Sh.10 milioni), Halotel (Sh10 milioni) na Puma Energy wameipa timu hiyo kiasi cha Sh10 milioni.

Wanaoifuatia Singida United kwa kuvutia idadi kubwa ya wadhamini ni Mbeya City inayoingiza Sh350 milioni kutoka na udhamini wa kampuni tatu ambazo ni Binslum Tyres inayotoa Sh150 milioni kwa mwaka, Coca-Cola (Sh.80 milioni) pamoja na Sports Masters inayoipa Sh120 milioni.
Mbao FC ina udhamini wa jumla wa Sh 165milioni kutoka kampuni mbili, baada ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja wenye thamani ya Sh140 milioni kutoka GF Trucks & Equipments pamoja na ule wa zaidi ya Sh25 milioni kutoka Hawaii Products Supplies Limited wazalishaji wa maziwa ya unga ya Cowbell.
Simba na Yanga kila moja inalamba udhamini kutoka SportPesa wakati Azam inapata udhamini wa Benki ya NMB huku Ndanda ikipigwa jeki na kampuni ya Motisum inayojishughulisha na uuzaji wa vifaa vya ujenzi na maji ya kunywa. Lipuli ina udhamini wa kampuni ya ubunifu wa mavazi ya Speshoz.
Hata hivyo licha ya kudhaminiwa na kampuni moja, Yanga na Simba zimekuwa vinara wa kukusanya fedha nyingi za udhamini  kila moja inapata kiasi cha Sh950 milioni kutoka SportPesa, zikifuatiwa na Singida United (Sh 650 milioni) huku Azam wakivuna Sh600 milioni.
Mbeya City wanashika nafasi ya tano wakiwa wanapokea kiasi cha Sh.350 kupitia udhamini wa kampuni za Binslum, Coca-Cola na Sports Masters, wakifuatiwa  na Mbao FC inayovuna Sh. 165 milioni, Ndanda wanavuna zaidi ya Sh100 milioni kwa mwaka huku Lipuli FC wakipata Sh17.5 milioni.
Ofisa habari wa TFF, Alfred Lucas alisema shirikisho hilo litaendelea kutengeneza mazingira mazuri kwa lengo la kuvutia zaidi kampuni kudhamini timu za Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili.
“Kama inavyofahamika kuwa shirikisho limekuwa likifanya juhudi za dhati kuvutia wadhamini, lakini tutakuwa wachoyo wa fadhila iwapo tukishindwa kuwashukuru wadhamini wetu wakuu wa ligi ambao ni Vodacom na Azam Media wamekuwa chachu ya kuvutia wawekezaji wengine kujitokeza na kudhamini klabu.
Bado tunaendelea kukaribisha kampuni kujitokeza kuzidhamini klabu zetu nyingi zinakabiliwa na ukata na kwa kuthibitisha hilo, tumeweka kanuni ambayo inazipa nafasi klabu kuweka matangazo ya wadhamini wao katika mechi zinazocheza viwanja vya nyumbani,” alisema Lucas.
Kanuni hiyo inayosemwa na Lucas ambayo inatoa fursa kwa klabu kumtangaza mdhamini ni ile ya 13 (6) ambayo inafafanua hivi,” Klabu Mwenyeji itakuwa na nafasi ya kuweka hadi mabango 10 ya mdhamini/wadhamini wake.” 
Ofisa masoko wa kampuni ya GF Trucks & Equipments, Kulwa Bundala alisema: “Hii ni mara ya kwanza kwetu kudhamini michezo.
Tumeamua kuidhamini Mbao FC tukiamini kuwa itafanya vizuri zaidi katika ligi. “Ifahamike  kampuni yetu imekuwa na idadi kubwa ya wateja Kanda ya Ziwa inapotoka Mbao hivyo kupitia udhamini huu nadhani tutazidi kujiweka karibu na wateja wetu,” alisema Bundala.
 Mkuu wa idara ya masoko wa kampuni ya Motisun wanaoidhamini Ndanda FC, Edward Mlyansi alisema udhamini wao kwa timu hiyo utanufaisha pande zote mbili.
“Udhamini huu bila shaka utakuwa na faida kwetu sisi kama Motisun pamoja na Ndanda na ndio maana tunawadhamini kwa mwaka mmoja,” alisema Mlyansi.

No comments:

Post a Comment